Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Wajumbe chagueni viongozi sahihi kuongoza TFF

TFF?fit=800%2C445 UCHAMBUZI: Wajumbe chagueni viongozi sahihi kuongoza TFF

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KUNA msemo huwa unatumiwa kwenye chaguzi mbalimbali hasa watu wanapofyekwa ‘Wajumbe si watu wazuri’. Hutumika sana kwa wale wanaokosa nafasi kwenye uongozi husika.

Wikiendi hii ya Agosti 7, Shirikisho la Soka nchini (TFF) linafanya uchaguzi wake mkuu ingawa kwenye nafasi ya Rais haina mpinzani kwani Rais wa sasa anayetetea nafasi yake Wallace Karia ni mgombea pekee baada ya wapinzani wake kuenguliwa hatua za awali kwa kukosa sifa.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilishatangaza kuwa Karia ni amepita moja kwa moja kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi na kilichobaki ni kuidhinishwa tu na mkutabo mkuu wa uchaguzi utakaofanyika Tanga.

Shughuli sasa imebaki kwenye hizo kanda sita ambazo zina wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo ambao wanatakiwa kuwa sita pekee.

Ni wagombea wengi kwenye nafasi hiyo, upinzani ni mkubwa ingawa uchaguzi wenyewe umepooza huku kampeni tayari zikiwa zimeanza Agosti Mosi. Kila mtu ana namna ya kujinadi na walio wengi sasa hutumia njia ya mitandao ya kijamii kama Instagram. Ni lazima wafanye hivyo kwasababu hivi mikusanyiko isiyokuwa ya lazima ama isiyo na kibali maalumu hairuhusiwi kutokana na kuwepo kwa janga la maambukizi ya virusi vya Corona linalosababisha ugonjwa wa Covid-19. Ndiyo maana ile vita ya kampeni haisikiki wala haionekane, ni kampeni za kimyakimya.

Ukiachana na hilo pia kupitishwa kwa Karia pekee nako kumepunguza ule msisimko wa uchaguzi huo kwani unaonekana sasa hauna nguvu na hata wakati mwingine nawaza kama vile umefanyika kwa maana ya watakaokuwa wajumbe.

Lakini hiyo bado haitoshi kuwa uchaguzi umemalizika bali watakaoamua nani awe mjumbe wa Kamati ya Utendaji kwa miaka minne ijayo ndani ya TFF ni wajumbe wa mkutano mkuu ambao ndiyo wameshikilia maamuzi ya wagombea wote.

Wajumbe sio watu kama watu wanavyosema, hawa wakiamua kukumaliza unamalizwa kimya kimya bila wewe kujua kuwa unamalizwa yaan wanakukata huku wakikuchekea na kukuonyesha tabasamu kubwa, pia wakikukata wanaungana na wewe kwenye masikitiko hivyo huwezi kujua ni mjumbe gani amekubaliza ndani ya box la kupiga kura.

Wagombea wanakwenda sambamba na wapiga kura lakini wapiga kura ambao ni wajumbe hata si wa kuwaamini kwa asilimia kubwa kuwa tayari umepata nafasi ya kuwemo kwenye jopo la wajumbe wa Kamati ya Utendaji hata kama unajiona unakubalika kwa asilimia kubwa lakini asilimia hizo zinaweza kuwa kwenye usoni tu na si mioyo yao ambayo imejificha. Nashauri kila mgombea aingine ukumbini akiamini na kuyapokea matokeo ya kuchinjwa, kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuiachia mioyo yao pasipokuwa na maumivu makali kuliko kuingia ukiwa umejiamini kupita halafu wajumbe wakakukata juu kwa juu, hiyo itawafedhehesha mioyo yenu na mtaumia sana na kuwalaumu wajumbe.

Hakuna asiyejua tabia za wajumbe kwamba ni vigeugeu na hawana misimamo ya kutoka moyoni, mjumbe anaweza kugeuka akiwa mbele ya box akisahau kabisa kuwa amemuahidi rafiki yake kumpigia kura halafu akauterezesha mkono wake na kwenda sanduku lingine la mtu ambaye alimuweka moyoni.

Lakini hilo lina madhara makubwa kwani ni mara nyingi wajumbe huchagua machaguo ambayo si sahihi kwa sababu tu alimbeba mtu ambaye si sahihi moyoni na yule sahihi akimuweka usoni tu na kumchinja kwa haraka pasipo kuangalia maendeleo ya nafasi anayokwenda kuitumikia.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni wasaidizi wakubwa wa Rais huko juu yaani ni kama mawaziri wake watakapoaharibu basi kila kitu kitaharibika kwani watashindwa hata kutoa ushauri kwa bosi wao maana akili hiyo haitakuwepo kwani watakuwa wameingia kijanja janja tu TFF.

Hivyo basi nawasihi wajumbe kuwa makini na watu mtakaowachagua kwa kuwapigia kura, miaka minne ya kukaa ndani ya TFF ni mingi sana, mkichagua wajumbe ambao si sahihi basi mtambue kuwa mnaenda kurudisha nyuma maendeleo ya soka pale TFF na kuanza kupeana lawama ambazo hazitasaidia kwa wakati huo.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz