Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Vijana wanavutia usajili wa wazee Ligi Kuu

Wazee Pic Data (600 X 337) Haruna Moshi "Boban"

Sun, 23 Jan 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani misimu miwili, nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Haruna Moshi ‘Boban’ amerejea tena uwanjani na sasa ataonekana katika Ligi ya Championship akiwa na kikosi cha Kengold ya Mbeya.

Katika kipindi chote hicho cha misimu miwili tangu alipoachana na Yanga, Boban alijikita katika kuinoa timu iliyomlea na kukiweka hadharani kipaji chake, Friends Rangers ya Magomeni.

Unajua kwa nini Kengold imeamua kujilipua na kumsajili mkongwe Boban licha ya kwamba hakuwa akicheza soka la ushindani? Jibu ni rahisi tu kuwa hawajaona mchezaji mwingine ambaye anaweza kutimiza vyema jukumu la kucheza nyuma ya mshambuliaji au namba nane kumzidi Boban.

Ukiondoa Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambao wote wako Yanga tena wakiwa na mikataba mirefu, hakuna mchezaji mwenye ubora wa juu mwingine anayecheza nafasi hizo ambaye anamuacha kwa ubora Boban.

Nchi kwa sasa inakosa wachezaji wengi wanaoweza kuzalisha mabao na kupiga pasi zinazofungua ukuta wa wapinzani kama ilivyo kwa Boban hivyo sio jambo la kushangaza kuona Kengold ikiamua kujilipua na kumsajili.

Inaamini kwamba kwa sasa kazi kubwa iliyopo ni kurudisha ufiti wa Boban lakini vigezo vingine vyote vya kiufundi bado mkongwe huyo anavyo.

Mbali na Boban, timu hiyo pia imemsajili mkongwe mwingine, Mrisho Ngassa ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 32.

Hawa wote wawili wanaenda kuungana na nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Danny Mrwanda mwenye umri wa miaka 38 ambaye ndiye nahodha wa timu hiyo.

Huyu Mrwanda ndiye mfungaji tegemeo wa Kengold kwenye ligi hiyo, ameifungia jumla ya mabao saba katika michezo 15 za mzunguko wa kwanza lakini kiujumla anashika nafasi ya tatu katika chati ya ufungaji bora wa ligi hiyo inayoongozwa na Amissi Tambwe wa DTB FC mwenye mabao 11.

Huyo Tambwe mwenyewe anayeongoza kwa ufungaji katika ligi hiyo ana umri wa miaka 33 ambao katika soka anahesabika kama mkongwe.

Ukitazama kile kinachofanywa na wachezaji hao wenye umri mkubwa na mchango wanaotoa kwenye timu zao, huwezi kushangaa viongozi na makocha wa timu mbalimbali wakiendelea kuwapa kipaumbele badala ya vijana ambao kiuhalisia ndio walipaswa wawe lulu katika dirisha la usajili.

Ufanisi na mchango wa wakongwe umekuwa mkubwa kwenye timu mbalimbali huku wale waliotegemewa kufanya makubwa kutokana na umri wao wakishindwa jambo linalosababisha wapoteze fursa muhimu ya kuvuna fedha licha ya umri walionao.

Huwezi kuzilaumu na kuzishangaa timu kwa kutowapa nafasi kubwa vijana wakati wahusika bado hawaonyeshi kutofurahishwa na hali hiyo na kuamua kupambana ili kufanya vizuri ndani ya uwanja kujenga imani kuwa wanastahili kupewa kipaumbele badala ya wale wenye umri mkubwa.

Vijana bado wanaonekana kulala kwenye usingizi mzito na hawatambui wajibu wao kwa timu hivyo hakuna kosa kwa timu kuwageukia wakongwe ambao wanawatimizia kile ambacho wanakihitaji.

Bado wachezaji wenye umri mdogo hawajapa sababu viongozi za kuachana na nyota wenye umri mkubwa na badala yake wanaendelea kubweteka wakiamini kuwa watapata nafasi na fursa kwa sababu ya umri wao na sio ufanisi na kiwango bora cha uwanjani.

Katika nchi ambayo idadi kubwa ya wachezaji wenye umri mdogo wanajielewa na kutambua thamani ya umri wao, ni vigumu kuona kundi kubwa la wachezaji wenye umri wa zaidi ya miaka 32 wakitamba na kugeuka lulu katika dirisha la usajili kama ilivyotokea kwa Boban na Ngassa.

Lakini kwa hapa nyumbani ni rahisi kutokea kwa sababu wakongwe ndio wameshika hatamu na vijana wameendelea kuwa wachezaji wasio na mchango mkubwa katika timu.

Kama Selemani Kibuta ambaye leo hii ana umri wa miaka 35 ni miongoni mwa washambuliaji tishio Ligi Daraja la Pili huku Mrwanda na Tambwe wakitamba kwenye Chmpionship, haupaswi kuona wao na wakongwe wenzao wakiendelea kuwa lulu katika vipindi vya madirisha ya usajili.

Badala ya kushangaa usajili wa wakongwe hao, tunapaswa kuwashangaa vijana ambao wanashindwa kutumia vyema wakati wao na kuwaachia wale wenye umri mkubwa kutamba.

Columnist: Mwanaspoti