Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Simba ilipotelea hapa Morocco

Potea Pic Data Simba ilipotelea hapa Morocco

Wed, 2 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Simba ilipoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika juzi, baada ya kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji wao RS Berkane ya Morocco.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kupoteza kiti cha kuongoza kundi D kwa Berkane ambalo Wekundu wa Msimbazi walikuwa wanaliongoza mpaka saa chache kabla ya mchezo huo.

Simba haikucheza vizuri mchezo huo hasa kipindi cha kwanza ambacho iliruhusu mabao hayo na kidogo ilirejea mchezoni katikati ya kipindi cha pili.

MFUMO ULIIGHARIMU

Simba ilibadili mfumo wake katika kikosi cha kwanza ikianza na mabeki sita na kuifanya timu kucheza zaidi nyuma na kupoteza nidhamu ya kushambulia. Hatua mbaya zaidi ni kwamba utitiri wa mabeki ulishindwa kuisaidia timu na kufanya makosa mengi ya kuruhusu kona nyingi na mipira ya adhabu.

MABEKI KURUKA

Ukiachana na bao la kwanza ililofungwa ambalo lilitokana na kuzalisha mipira mingi ya adhabu, lile la pili mabeki wa Simba wakishindwa kufanya kazi vyema na kuwaacha Berkane wakiruka bila kusumbuliwa.

Charki el Bahri wa Berkane alifunga bao la pili kwa kichwa akiwa amezungukwa na mabeki wasiopungua watatu, lakini hakuna aliyeruka naye kumsumbua. Makosa ya namna hiyo ni mabaya unapocheza na timu za Kaskazini mwa Afrika ambazo zina watu hatari katika mashambulizi ya aina hiyo.

BOCCO BADOBADO

John Bocco, nahodha na mshambuliaji wa Simba hakuwa na msaada katika kutengeneza mashambulizi, bali alifanya kazi nzuri ya kuwatuliza mabeki wa Berkane alipopata mpira, lakini haikuwa na maana kufuatia kukosa msaada wa kuwatengenezea mashambulizi wenzake waliotawanyika sana na hatimaye akadhibitiwa kirahisi.

Katika mechi tatu ambazo Simba imecheza hadi juzi ilishindwa kupiga shuti lolote lililolenga lango ikionyesha udhaifu mkubwa dhidi ya wapinzani wao.

Simba ilipiga mashuti mawili tu ndani ya dakika 90 na yote hayakulenga lango wakati Berkane ilipiga mashuti 19 na matano kati ya hayo yalilenga lango na moja lilizalisha bao.

BAHATI YA INONGA

Beki Henock Inonga alikuwa na bahati kumaliza mechi hiyo na awali alistahili kadi nyekundu ingawa kuna wakati alifanya kazi bora kuwadhibiti Berkane. Shida ya Inonga ni kucheza vibaya katika kipindi cha kwanza na tayari alikuwa ameshafanya makosa matatu akimkanyaga mchezaji wa Berkane na pia alishika mpira.

Kama mchezo huo ungekuwa na usaidizi wa teknolojia ya video, beki huyo ingekuwa ngumu kumaliza mchezo huo na anatakiwa kubadilika na kuboresha nidhamu.

Mabadiliko ya kocha Pablo Franco kumtoa Peter Banda na kumuingiza Bernard Morrison ulikuwa ni uamuzi mzuri na timu ilionekana kuhitaji huduma yake. Hata alipoingia alionekana kuwa na kitu katika kutengeneza kasi eneo la mbele.

SIMBA INA NAFASI

Licha ya kupoteza mchezo huo, bado Simba ina nafasi na sasa inarudi nyumbani kujiuliza dhidi ya Waarabu hao ambao itakipiga nao Machi 11 kisha itasafiri kuwafuata Asec Mimomas Machi 18 ukiwa mchezo wake wa mwisho ugenini kabla ya kuja kumalizana na US Gendarmerie nyumbani, Aprili Mosi.

Simba inapaswa kushinda mechi mbili za nyumbani ili kurudisha matumaini ya kufuzu robo fainali ukizingatia ina rekodi nzuri ya kushinda nyumbani, lakini pia ikiwa ndio timu ambayo imeambulia pointi moja katika kundi ugenini.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz