Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Simba hakikisheni kwamba mnalipa deni la Magufuli

MAGUSIMBA UCHAMBUZI: Simba hakikisheni kwamba mnalipa deni la Magufuli

Fri, 2 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MACHI 17, mwaka huu itakuwa ni siku ya kukumbukwa kila mwaka kuondokewa na kipenzi cha wanyonge, Rais wa tano, John Magufuli aliyefariki dunia kwa maradhi ya moyo.

Usiku wa tarehe hiyo Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitangaza kutokea kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa tano, Dk Magufuli.

Wengi walitaharuki kufuatia kifo hicho, hata mimi nikiwa miongoni mwa watu waliokosa usingizi wakitafakari juu ya taarifa hiyo ambapo kama asingetangaza Rais Mama Samia, basi ingechukua muda kuamini juu ya kifo hicho.

Baada ya taarifa hiyo, kila mahali ambapo niliangalia iwe kwenye televisheni au mitandao ya kijamii taarifa ilikuwa ni hiyohiyo. Ilinibidi kukubaliana na ukweli wa jambo namna lilivyotokea.

Hayati Magufuli amefariki dunia kipindi ambacho Tanzania ilikuwa inamhitaji, lakini mapenzi ya Mungu hayawezi kupingwa na inabidi kukubaliana nayo na kuyapokea japokuwa mapokezi yake ni ya uchungu mkubwa. Mapokezi yanaumiza mioyo kuliko jambo lingine katika maisha ya binadamu.

Hayati Magufuli alikuwa ni Rais wa nchi mwenye mapenzi na nchi yake katika nyanja tofauti. Aliweka usawa ambapo wakati mwingine tuliona maisha yako sawa kwa walionacho na wasiokuwa nacho.

Ukiachana na mambo ya kisiasa na mengineyo yaliyogusa jamii, pia alikuwa ni kiongozi aliyependa michezo na burudani kwani tasnia hizi nazo hakuziacha nyuma.

Aliunganisha wasanii wa fani mbalimbali akisikiliza na kutatua kero zao kiasi kwamba nao walijiona ni miongoni mwa Watanzania wanaothaminiwa na kazi zao zinathaminiwa.

Alikuja upande wa michezo. Dk Magufuli hakuwa mbaguzi aligusa kote. Kuanzia klabu hadi timu za taifa. Aliwahi kushuhudia mara mbili mechi za Ligi Kuu Bara ambazo zote timu ya Simba ilihusika.

Ni ile mechi waliyocheza na Kagera Sugar ambayo Simba walifungwa bao 1-0 ingawa walichukuwa ubingwa aliibuka tena uwanja wa Mkapa kushuhudia pambano la watani - Simba na Yanga ambapo Simba ilipoteza.

Lakini bado Hayati Magufuli pamoja na kutoonyesha wazi mapenzi yake yapo timu ipi, lakini aliwahi kutamka anatamani siku moja timu ya Tanzania ichukue ubingwa wa Afrika na wakati huo Simba ndiyo ilikuwa mwakilishi wa michuano hiyo mikubwa barani Afrika ya Ligi ya Mabingwa.

Simba katika uongozi wake iliwahi kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa - hatua ambayo kwa timu zetu ni kubwa mno na sasa wapo hatua ya makundi ingawa mwenendo wao unaonyesha wazi kwamba watatinga tena robo fainali.

Binafsi sioni wapi Simba wanaweza kukwama kufika hatua ya michuano hiyo ya fainali ya michuano hiyo mikubwa na kutwaa ubingwa.

Bado sioni ule upinzani wa timu za nje ambazo zilikuwa tishio miaka ya nyuma kwani katika mechi mlizocheza Simba ndiyo imeonyesha kiwango bora kuliko wapinzani wao.

Awali tulishuhudia wakipigwa tano wanapokwenda ugenini, lakini hivi hakuna kitu kama hicho hiyo inaonyesha ni namna gani Simba wameimarika, namna gani nao wamewekeza nguvu kutengeneza kikosi bora.

Simba mna kila sababu ya kuyaenzi maneno ya Hayati Magufuli kwa vitendo.

Kama sio leo basi isichukue muda mrefu kuutwaa ubingwa huo wa Afrika kwani inawezekana maana kila klabu inafanya maandalizi hata kama kuna kuzidiana kiuchumi, lakini kwa wachezaji wanaokuwepo wanapaswa kupambania malengo ya klabu yao.

Maneno ya Magufuli yalikuwa ni mchango tosha wa maendeleo kwa Simba na hata kwa timu zingine kupambana kufikia hatua kama ilivyofikiwa na Simba, ingawa tumeshuhudia japo timu za taifa zimekuwa zikifanya vizuri katika uongozi wake.

Magufuli ameondoka lakini tumeachiwa Mama Samia, mwanamke shupavu na hodari, mpambanaji na mwenye kutambua nchi yake inahitaji nini katika kuleta maendeleo, tunampongeza na kuamini kwamba yale aliyoyaacha Magufuli atayaendeleza na pengine zaidi ya pale.

Mafanikio ya Simba kwenye michuano ya Afrika itakuwa ni kumuenzi Hayati Magufuli lakini kumuonyesha Rais Samia kuwa kwenye michezo hususani soka inawezekana kutwaa ubingwa wa michuano mikubwa ili naye ashawishike kuwa

kipenzi maradufu kwenye michezo.

Simba ni kama mmeachiwa deni na Magufuli, hakikisheni mnalilipa lakini wanamichezo wote mnapaswa kumuenzi Rais huyo ambaye amefanya mambo mengi nchini ikiwa ni pamoja na kubadilisha taswira mbovu iliyokuwepo kwenye michezo.

Katika uongozi wake hata utendaji kazi kwenye taasisi mbalimbali ulikuwa umenyooka watu walifanyakazi kwa weredi wakihofia tu kwenda tofauti na mwongozo wa Magufuli juu ya uongozi bora.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz