Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Madalali wa wachezaji wameshajua udhaifu wetu

Madalali Data UCHAMBUZI: Madalali wa wachezaji wameshajua udhaifu wetu

Sat, 7 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

NGOJA nikupe hii kwanza. Juzijuzi hapa, Yanga wamemtuliza mchezaji mmoja wa kigeni wa Simba akiwa njiani kwenda Dar es Salaam kusaini Msimbazi. Unajua kilichofuata wakamcheki Kocha wao.. tunae fulani hapa mkononi anacheza namba Fulani na fulani, tumsainishe? Nikasikia kwamba akawachomolea. Wakamuachia.

Simba wakapiga kimya. Wakajibu mapigo. Wakapindua meza kwa beki mmoja wa kigeni vilevile ambaye alikuwa ameshamalizana na Yanga bado kusaini tu. Wakamshusha Yanga wakaja kushtuka tayari yuko mikononi mwa Simba hotelini Dar es Salaam. Wakala anajiumauma tu. Ndio mambo ya usajili wa Simba na Yanga.

Kuna mambo yanayofanyika yanafikirisha sana kwamba Simba na Yanga hazibadiliki kwenye mfumo wao wa kusajili wachezaji. Inakuwaje Simba na Yanga zinagongana kwa wachezaji kama wanne wa kigeni kwa wakati mmoja? Hapa kuna tatizo.

Tafsiri yake ni kwamba kuna sehemu pana tatizo,kama si kwa viongozi moja kwa moja ni mawakala na madalali wenye asili ya Kifaransa ambao tayari wameshajua akili zetu na wanacheza nazo kupitia mashabiki na wachambuzi kujipatia cha juu. Na kwa hali hiyo inakuwa ni ngumu sana kupata kitu kizuri, yaani ushabiki unakuwa mbele Zaidi kuliko suala la msingi ambalo madhaifu ya timu husika.

Haiwezekani klabu zote mbili ziwe na matatizo yanayofanana na matakwa yanayofanana. Simba ile au Yanga ile ni vitu viwili tofauti, sasa unapoona wanagombea wachezaji kwa pamoja inafikirisha sana. Hata kama ikitokea lakini siyo kwa wachezaji watatu mpaka wanne. Kinachoonekana ni kwamba klabu hizi za Simba na Yanga bado zina aina ya baadhi ya viongozi ambao hawajitambui au wako kwa masilahi Fulani haswa wakati huu.

Kuna sehemu pana tatizo nje ya mabenchi ya ufundi. Kwavile naamini wachezaji wa Afrika ni wengi kuna machaguo mengi ya walioko kwenye mikataba na ambao imemalizika.

Hali ya kugongana kwa wachezaji kadhaa inamaanisha kwamba kuna viongozi ambao bado wanajishughulisha na ishu za usajili kwenye klabu hizo pengine bila hata ya kuzingatia matakwa ya Makocha.

Matokeo yake hata baadhi ya mawakala hususani kutoka DR Congo, Ghana, Burkina Fasso wameshaelewa michongo iliyopo kwenye klabu hizo ndio maana wanaamua kucheza akili zao kwa kujua wanaweza kunufaika na chochote mwisho wa siku.

Kwavile wao wapo sokoni na pengine wameshajua kwamba kama wakicheza dili na vigogo wa klabu za Simba na Yanga kuna neema fulani wanaweza kuipata na mambo yakaenda, upenyo ambao kwenye nchi zingine ni ngumu kuupata kwa karne hii.

Viongozi wa Simba na Yanga hata kama wanahusishwa na usajili wawe makini kwa masilahi ya klabu zao, ishu ya kusajili kwa fasheni waachane nayo kwavile haina faida kwa soka letu na kuboresha ushindani kwa timu hizo kimataifa msimu ujao.

Kama wanasajili wageni waje wenye vigezo na uwezo stahiki ambao wataongeza ushindani kwa wazawa na kuziboresha klabu zetu ndani na nje kimashindano. Kitendo cha kuleta tu wachezaji wanakula fedha za klabu na kuondoka si picha nzuri kwa uchumi wa klabu hizo hata maendeleo ya soka letu.

Viongozi wa Simba, Yanga pamoja na klabu zingine za Ligi Kuu Bara waweke msisitizo kwenye vigezo vya benchi la ufundi katika usajili mpya, bora wapatikane wachezaji wachache wa gharama kubwa na wenye uwezo wa kubadili kitu kwenye soka letu kuliko kuwa na lundo ambalo hata mwisho wa siku linagharimu kwenye kuvunja mikataba.

Klabu zitumie usajili huu mkubwa kuimarisha mapungufu yao na kufanya maandalizi mazuri kuliko kugeukia kwenye ushabiki na kugombea vitu vidogovidogo ambavyo havina hadhi ya klabu. Muda huu utumike vilevile kutengeneza njia mpya za kujikwamua kiuchumi na kupata vyanzo mbadala vya mapato ya kujiendesha msimu ujao. Haya tusubiri leo tuone nani atashuka huko Uwanja wa Ndege.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz