Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UCHAMBUZI: Hili la miundombinu JPM hatasahaulika

Miundombinu Pic Data UCHAMBUZI: Hili la miundombinu JPM hatasahaulika

Sun, 28 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KIPENZI chetu Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ambaye mwili wake ulipumzishwa jana nyumbani kwao Kijiji cha Mlimani wilayani Chato mkoani Geita, huku Watanzania wakitakiwa kuendelea kumuombea kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi chake kifupi cha uongozi.

Kama mwanadamu yeyote aliyepo duniani makosa ni sehemu ya maisha, hivyo tumuombee kwa Mungu amsamehe makosa aliyofanya duniani enzi za uhai wake.

Ni vyema tufanye hivyo huku pia tukiendelea kumuenzi kwa kutenda kile alichotuachia chenye mchango mkubwa kati maisha ya vizazi vijavyo vya Watanzania.

Miongoni mwa vitu alivyotuachia na vizazi vyetu vitaendelea kumkumbuka na kumtaja kwa miaka mingi hasa eneo la miundombinu ambalo ni moja kati ya mahitaji ya msingi kwa sekta zote.

Hii ni kwa sababu miundombinu ni muhimu kwa kuwa ni sekta inayogusa kila nyanja yenye mchango mkubwa.

Miundombinu katika uchumi wa taifa huchangia kukua kwa sekta nyingi kama vile za nishati, kilimo, mifugo, uvuvi na nyingine ambazo zote zinaguswa na miundombinu.

Vilevile huku kwenye mchezo wa soka pia miundombinu ni kitu cha muhimu kwa maendeleo ya soka ndio maana katika sheria 17 za soka uwanja mzuri wa soka unapaswa kuwepo.

Namba moja inazungumzia uwanja wa kuchezea soka na wala sio mchezaji au kocha ama mwamuzi kutokana na umuhimu wake.

Hali hiyo inathibitisha walioandaa sheria hizi miaka ya 1800 walitambua umuhimu wa miundombinu. Ndio maana sheria ya uwanja wa soka wakaifanya namba moja kabla ya kuingia ya pili inayozungumzia vifaa vya kuchezea soka.

Sheria namba tatu ndio inayomhusu mchezaji, kuthibitisha kuwa uwanja wa kuchezea mpira ni muhimu kuliko mchezaji au mpira wenyewe.

Nimeizungumzia miundombinu na kumzungumzia namna bora ya kumuenzi kiongozi wetu mpendwa aliyetuacha na kutangulia mbele ya haki ni kuishi ndoto zake kwa kutekeleza maono ya maendeleo ya soka nchini.

Hii ni kwa vile katika soka la Tanzania ukiachilia mbali mchango wake wa uongozi wa nchi kwa ujumla, eneo la miundombinu ya soka ni miongoni mwa maeneo iliyokuwa mipango yake ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa baadhi ya viwanja vya soka vilivyopo mikoani na ujenzi wa viwanja vipya vya soka katika jiji la Dodoma na Chato mkoani Geita.

Nazungumza hivi kwa kuwa hata serikali ya China chini ya Rais Xi Jing Pin mwaka 2016 iliandaa mpango wa maendeleo uliotokana na ndoto za rais huyo baada ya kufanya ziara barani Ulaya na kutamani kuiona nchi yake inatawala soka la ulimwengu ifikapo 2050 kwa kutwaa Kombe la Dunia.

Ndoto hizo au maono hayo ya Xi Jin Ping yachangia kuandaa mpango wa maendeleo ya soka uliogusa maeneo mawili muhimu ambayo ni kushiriki Fainali za Dunia na kuandaa fainali za michuano hiyo ifikapo 2050.

Mipango yote hiyo iliainisha kipaumbele kuwa ni miundombinu ya soka  kwanza serikali ya China ilipanga hadi mwaka 2030 kuwe na vituo vya mafunzo ya soka la vijana 20,000 na viwepo jumla ya viwanja 70,000 ambapo viwanja 30,000 vikiwa ni katika jamii huku 40,000 vikiwa vya vyuo na shule kwa matumizi ya wanafunzi.

Utekelezaji wa ndoto hizo ulishaanza muda mrefu tangu 2016.

Na hata kikao cha Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kilichofanyika China miaka mitatu baadaye yaani 2019 kiliamua nchi hiyo iwe mwenyeji wa michuano mipya ya Klabu Bingwa ya Dunia iliyopangwa kufanyika mwaka huu.

Hata hivyo baadae iliahirishwa kutokana na hofu ya janga la corona.

Uamuzi huo ulitokana na uwepo wa miundombinu rafiki nchini China ulitokana na matokeo ya ndoto za Xi Jin Ping ya kutaka 2050 China itawale soka ulimwenguni.

Ni kutokana na hali hiyo, hivyo hili kuwa ni somo kwetu nasi kama Watanzania tunatakiwa kujifunza kwa kumuenzi kiongozi wetu, Dk Magufuli kwa kuziishi ndoto zake tukianzia na uwanja wa soka wa kimataifa katika Jiji la Dodoma.

Pia tuendeleze ndoto zake za kujengwa uwanja wilayani Chato huku tukiendelea na mipango mingine mitamu katika sekta ya michezo.

Kwa leo naomba niishie hapo nikisubiri mrejesho kutoka kwako msomaji.

Imeandikwa na Ali Mayay

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz