Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Yanga wamemchunguza kweli Musonda?

Kennedy Musonda Jr Mshambulaiji mpya wa Yanga, Kennedy Musonda

Thu, 19 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwenye soka la kisasa ambalo linahitaji vitu kumfuatilia mchezaji sio jambo dogo. Kumsajili mchezaji ni mchakato mrefu sana. Ni kama ndoa za zamani. Wazee wetu walikuwa hawaoi tu kwa sababu wamekutana na mwanamke disko! 'Scouting' ya kutosha ilikuwa inafanyika.

Vikao vingi vya Wazee vilitumika kujiridhisha na mienendo ya Msichana husika. Hakuna tofauti sana na Usajili wa Wachezaji. Unapaswa kufanya 'Scouting' ya kutosha ili kujiridhisha na ubora mchezaji kabla ya kufanya uamuzi wa kumsajili. Wapo wanaomtazama mchezaji kila mechi uwanjani. Wapo wanachunguza historia yake. Wapo wanaochunguza maisha yake nje ya uwanja. Haya yote yanaweza kufanyika na bado mchezaji anashindwa kuisaidia timu. Je, tunaofanya bila kuchunguza chochote kabisa? Riski ni kubwa sana. Wakati Fernando Torres anataka Liverpool na kwenda Chelsea, njia za sayansi zote zilifanyika lakini usajili ulibuma!

Utamaduni wa soka unaonyesha kuwa wachezaji wengi ambao wamefanikiwa, huwa wanadumu katika klabu kwa muda mrefu angalau misimu mitano na kuendelea. Angalia Cristiano Ronaldo alikaa Man United miaka sita na kufanikiwa kushinda tuzo ya Ballon D'or pamoja na kuwa mfungaji bora wa EPL. Baadaye akaenda Real Madrid ambako nako alikaa kwa muda mrefu sana na kushinda mataji yote kwa ngazi ya klabu na tuzo binafsi Ballon D'or nne.

Achana na Ronaldo, hebu tumtazame Lionel Messi ambaye ameshinda Ballon D'or saba akiwa na FC Barcelona. Hapa utaona kuwa wachezaji wengi walikaa muda mrefu na klabu zao. Hii ni mifano tu ili wapo wengi ambao wamefanikiwa hasa wale ambao wanacheza eneo la ushambuliaji.

Tukirudi hapa nyumbani bado kuna wasiwasi wa aina ya wachezaji wanasajiliwa na klabu zetu kongwe za Simba na Yanga. Angalia huu usajili wa Mzambia Kennedy Musonda ambaye ametua pale Jangwani. Huu usajili unanipa maswali mengi kichwani! Je ni kweli Yanga wamemchunguza kabla ya kumsajili? Sina majibu.

Ukimtazama Musonda ana wastani wa kukaa na timu kwa msimu mmoja tangu msimu wa 2015/20/6. Pale Power Dynamos ndiyo amekaa misimu miwili tena kwa awamu mbili. Kila msimu mchezaji amekuwa na timu mpya. Kila msimu mchezaji anahama!

Hapa unakuja na kukaa chini kisha unajiuliza, huu utaratibu wa kuhamahama kwa Musonda unaleta utakuwa na tija kwa Yanga? Sina majibu. Hebu ziangalie klabu kubwa Afrika kama vile Al Ahly, Wydad Casablanca, Zamalek na Esperenace De Tunis ambazo zinafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, wachezaji wao ambao wanacheza eneo la angalau wanakaa kwa misimu miwili hadi mitatu.

Sisi bado hatuna Pesa ya kununua kweli Wachezaji wa maana. Sisi bado hatuna pesa ya kusajili Wachezaji vijana. Sisi bado hatuna pesa ya kuleta watu wa ubingwa. Kiwango chetu kwa kiasi kikubwa ni kupata wachezaji huru na wale wanaokaribia kustaafu!

Ukimuangalia huyu Musonda mwenyewe umri wa miaka 28, utaona mwenendo wake wa kuhamahama unaibua maswali kwa sababu kama mchezaji anayefanya vizuri katika klabu aliyopo ni mgumu kumuona akiondoka.

Inawezekana Musonda hakuwa na takwimu nzuri ndiyo maana tangu mwaka 2015 hadi 2023 ameshacheza timu saba haiwezekani mchezaji mzuri tangu msimu wa 2015/2016 ameshacheza Lusaka Dynamos, Nakambala Leopards, Zanaco, Kabwe Youth Academy, Green Eagles na sasa Yanga. Kuna kitu hakipo sawa.

Uzuri ligi yetu bado sio ya ushindani kiivyo kwa hiyo anaweza kuja kufanikiwa lakini kumtegea kimataifa, sio kweli. Ni kamari kubwa sana Yanga wamecheza. Usajili Dunia kote ni kubahatisha lakini sisi tunabahatisha mno.

Hatuna uhakika na Usajili wowote. Wachezaji wengi wa kigeni hapa kwetu wanakuja bure au kwa bei chee! Vitu vya bei rahisi vinagharama kubwa sana! Lazima timu zetu zianze kuweka bajeti zao za kutosha kama kweli tuna ndoto za kutwaa ubingwa wa Afrika siku moja. Haya mambo ya kupiga ramli yanaturudisha nyuma.

Ukienda mbali zaidi utaona hata takwimu za Musonda katika ufungaji sio za kutisha. Ni msimu huu tu ndiyo amefunga amefunga mabao 11 katika mechi 17 pale Ligi Kuu ya Zambia. Katika misimu mitano iliyopita, hakuna hata mmoja ambao amewahi kufikisha mabao 10.

Ni mchezaji wa kawaida mwenye takwimu pia za kawaida. Ukitazama namba za mchezaji, inakuonyesha kuwa Yanga hawakumchunguza Kennedy Musonda. Wameangalia kiwango chake cha sasa na kufanya maamuzi.

Ni 'riski' kubwa wamefanya lakini kwenye mpira wakati huu huwa kuna muujiza. Anaweza kuja kwa kusuasua lakini akageuka kuwa staa mkubwa. Musonda katika kipindi cha misimu mitano amefunga mabao 21 tu ambayo ni wastani wa mabao manne kwa kila msimu.

Kilichobaki ni kusubiri kuona nini ambacho atakitoa kwa Yanga ambao wanashiriki Ligi Kuu, michuano ya FA na Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini kwa kumtazama mchezaji, miujiza mikubwa inasubiriwa.

Columnist: Mwanaspoti