Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Unawajua au unawaskia wachezaji wa Kikongo?

Kaliua Pic.png Unawajua au unawaskia wachezaji wa Kikongo?

Thu, 3 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Yanga walitakata kwa Mkapa kisha Simba wakapoteana kule Morocco. Yanga wanazidi kupaa kileleni mwa msimamo wakizidi kukaribia kumaliza safari ya kuusaka ubingwa walioukosa kwa muda mrefu.

Simba wao walikufa Morocco na kuwaruhusu RS Berkane kushikilia usukani katika kundi lao. Niliandika hapa wiki iliyopita Simba walipaswa kusaka walau alama moja Morocco kwa sababu matokeo ya ASEC na USGN yanaweza kuliathiri kundi zaidi kama mechi yao haitaisha kwa sare.

Bahati mbaya nilichotabiri na kukihofia kilitokea, USGN wamepata alama tatu na kundi limezidi kuwa wazi kwa yoyote. Hili suala la kundi kuwa wazi limezidi kuwaumiza mashabiki wa Simba.

Mashabiki wa Simba wanaumia kwa sababu kuu mbili, kwanza ni hii niliyoieleza ya matokeo ya kipigo yanayozidi kuifanya njia ya robo fainali kuwa nyembamba zaidi. Pili ni wapinzani wao wa karibu Yanga wanafanya vizuri kwenye Ligi Kuu na wanatishia kuwanyang’anya ubingwa wanaoushikilia.

Kibaya zaidi ni tambo wanazokutana nazo kutoka kwa Yanga, utawaambia nini Yanga wakati wanacheza soka safi la kitabuni linalomruhusu Fiston Mayele kutetema kila mechi?

Jumapili alitetema mara mbili na kufikisha mabao tisa yaliyomweka bao moja nyuma ya kinara Reliant Lusajo wa Namungo. Hiki ndicho kinachowapa furaha Yanga na kuwaumiza Simba.

Yanga wana haki ya kufurahi kwa kilichotokea Jumapili lakini kipo kitu kimoja zaidi nilikiwaza kikanikatisha tamaa. Nitakueleza baadae kidogo.

Mayele alifunga bao lake la nane na tisa dhidi ya Kagera Jumapili. Ulikuwa mwendelezo wa kile alichozoea kukifanya mara zote. Pasipo ubishi Mayele ndiye mshambuliaji hatari zaidi ligi kuu msimu huu. Achilia mbali Lusajo na mabao yake, hakuna mshambuliaji anayewashughulisha mabeki kama Fiston Mayele.

Unaona kabisa sura za mabeki zina wasiwasi Mayele anapokuwa uwanjani, ni kwa sababu wana uhakika muda wowote atawapiga bao.

Mayele hafungi pasipo kusaidiwa! Anategemea pasi nzuri za mwisho na ‘krosi’ za uhakika. Moja kati ya watu ambao humpigia krosi za uhakika ni swahiba wake wa karibu Djuma Shaban.

Jumapili Djuma hakumpigia krosi yoyote ya bao lakini bado alikuwa hatari kutokea upande wa kulia wa Yanga, kando ya Djuma alikuwepo Yanick Bangala akicheza beki wa kati. Ni raia mwingine wa Congo anayewapa Yanga utawala wa mchezo akichezeshwa kama kiungo au beki kama ilivokuwa Jumapili.

Wacongo hawakuwepo mechi ya Yanga na Kagera tu, kule Morocco kwenye mechi ya RS Berkane na Simba walikuwa wakiliwakilisha taifa lao kupitia klabu zao, Simba walikuwa na Henock Inonga aliyekazana kuwaweka hai muda mwingi wa mchezo. Alilihami lango la Simba vema.

RS Berkane nao hawakuwa nyuma, walikuwa na mawinga wawili kutoka Congo, alikuwepo Tuisila Kisinda ambaye Simba wanamfahamu vyema. Upande wa pili walikuwa na Chadrack Lukombe aliyekuwa anawapa mateso mabeki wa pembeni wa Simba.

Kila aliposhika mpira uliona kabisa kwamba Simba wapo matatizoni, achana na Kisinda ambaye nina uhakika Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ atamtaja kama winga msumbufu zaidi aliyewahi kukutana nae.

Baada ya kumaliza kuvutiwa na wachezaji wacongo nilitamani kufahamu utumishi wao katika timu yao ya taifa. Huwezi kuamini! Licha ya ubora na sifa zote nilizozungumza kwa hawa wacongo hakuna hata mmoja anayetegemewa na taifa lake.

Hawa kina Djuma, Mayele, Inonga na Bangala wamewahi kuitwa timu ya taifa ya Congo lakini sio kwa sababu wanawategemea. Ni kwa sababu labda ilikuwa mechi ya kirafiki na hawakuwa na uwezo wa kuwapata wachezaji wao waliopo Ulaya au waliwaita katika mechi ya kimashindano ili kutimiza idadi ya wachezaji lakini hawakuwa sehemu ya kikosi kilichocheza mechi.

Ni hiki kitu kilinikatisha tamaa. Kumbe na ubora wote huu tunaouona kwa akina Mayele bado kwao ni wachezaji wa kawaida sana. Vipi kama wangekuwa Watanzania? Lazima wangekuwa wachezaji wanaotegemewa zaidi timu ya taifa kama tu ambavyo sasa wanategemewa kwenye klabu zao.

Vipi tungekuwa na mchezaji anayeanza RS Berkane? Lazima angekuwa staa timu yetu ya taifa. Unapokaa chini na kujihoji maswali kama haya, ndipo unagundua kuwa kumbe bado tuna safari ndefu sana ya kwenda.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz