Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Unaiona wapi Yanga kimataifa?

Yanga Full Squad 2022 23.jpeg Unaiona wapi Yanga kimataifa?

Thu, 6 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna uoga wowote kusema Yanga ndiyo timu bora kwa sasa nchini. Sio kificho tena. Kikosi cha kwanza kimesheheni watu. Ukitazama benchi lao nalo limejaa watu wa maana. Unatazama mechi yao na Ruvu Shooting ndani unawaona Fiston Mayele, Salum Aboubakar na Bakari Mwamnyeto. Ni mechi hiyohiyo ambayo kwenye benchi unamuona Kibwana Shomary, Khalid Aucho na Herritier Makambo.

Ni kwa miaka mingi sana Yanga haijawahi kuwa na ubora huu wa wachezaji. Ukitazama benchi la ufundi unamuona Nasreddine Nabi na Cedric Kaze. Hii ni Yanga kubwa kuliko. Lakini baada ya hayo yote kama kuna kibarua kigumu kwa Yanga msimu huu, basi ni walau kwenda hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hayo yote niliyotangulia kusema hapo juu hayatakuwa na maana kama Yanga itatolewa mapema zaidi kwenye michuano ya hiyo ya Afrika. Hayo yote yatakuwa hayana maana kama Yanga watangĂ­olewa na Al Hilal kutoka Sudan.

Ukiwatazama kwenye michuano ya ndani bado Yanga watasumbua sana. Watasumbua michuano ya FA. Watasumbua michuano ya Ligi Kuu. Wakati wanaipasua Ruvu Shooting juzi walikuwa wanafikisha siku 527 bila kupoteza mechi yoyote Ligi Kuu Bara. Ni wafalme wa ligi yetu kwa sasa. Hawakamatiki kabisa. Hawashikiki kabisa.

Imepita miaka 24 tangu mara ya mwisho Yanga ilipofika hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni muda mrefu sana. Ni umri wa mtoto aliyehitimu elimu ya chuo kikuu. Ni umri wa kijana aliyeoa au kuolewa na kupata watoto.

Huu ndiyo mtihani mkubwa kwa Yanga msimu huu. Wamekuwa wa kawaida sana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hapa ndipo mtihani kwa Nasreddine Nabi ulipojificha. Hapa ndipo ubora wa Fiston Mayele unakwenda kujaribiwa.

Itakuwa haina maana yoyote kama timu inaweza kuitwa bora kama itashindwa kwenda hatua ya makundi. Itakuwa haina faida yoyote kama usajili wa wachezaji 12 wa kigeni utatumika kushindana michuano ya ndani tu.

Najua mafanikio ya Simba kimataifa pia yatakuwa yanawanyima usingizi, lakini Simba hawajafanikiwa kwa bahati mbaya. Simba waliwekeza kwenye kutengeneza wachezaji. Simba waliwekeza kwenye kusaka makocha bora.

Pamoja na kuwa ubora wa Yanga bado haujafikia ule wa Simba ya Clatous Chota Chama na Luis Miquessone, lakini wanatakiwa kuvuka walau hatua ya makundi. Pamoja na kuwa Yanga bado hawana watu kama Meddie Kagere, Chris Mugalu na John Bocco wa kiwango kile kikubwa, lakini wana ubora wa kusonga mbele.

Hakutakuwa na kujitetea kokote kama timu itaondolewa mapema. Bado ile Simba iliyofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika naiona bora kuliko Yanga hii, lakini bado Yanga wanatakiwa kuvuta hatua ya makundi.

Unaiona wapi Yanga kimataifa? Kama unajibu tafadhali usisite kunitumia kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Pamoja na ubora wote wa Yanga hii lakini kuna mahali nadhani wana changamoto. Bado napata mashaka makubwa na ubora wa safu yao ya ulinzi pale kati. Nimefurahi kumuona nahodha Bakari Mwamnyeto akianza kurejea kwenye kiwango kizuri. Mwamnyeto hakuwa kwenye kiwango kizuri siku za hivi karibuni. Inawezekana ni uchovu baada ya kutumika sana miaka ya hivi karibuni. Inawezekana pia ndiyo asili ya mchezo wenyewe. Kuna kipindi mpira unakataa. Kuna kipindi mpira unakubali.

Eneo la ulinzi wa kati kumekuwa na shida kidogo ndiyo maana mechi zote dume Kocha Nabi analazimika kumtumia Yannick Bangala na mchezaji mmoja ama Dickson Job au Mwamnyeto. Ligi ya Mabingwa Afrika unakwenda kukutana na mabingwa. Sio Geita Gold. Sio Ihefu SC. Ni pagumu sana ukilinganisha na Ligi Kuu Bara. Ni michuano ambayo wakati mwingine utakazimika kusafiri kwa zaidi ya saa nne. Ni michuano ambayo kuna muda utalazimika kubadili hata ndege mbili kufika unakotakiwa kwenda kucheza. Sio jambo dogo.

Unahitaji ukomavu wa wachezaji kwelikweli. Kama mara ya mwisho kwa Yanga kucheza hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni 1998, huu ni muda muafaka wa kuwapa furaha mashabiki wao. Wana kila kitu kuwapeleka mbele. Tajiri Ghalib Said Mohammed yupo. Wachezaji wazuri kama Fiston Mayele wapo kikosini. Benchi zuri la ufundi nalo lipo. Timu inaweza isifike mbali sana, lakini makundi inapaswa kuwa lazima. Inawezekana hawana ubora kama ule wa Simba ya Miquessone na Chama, lakini bado Yanga itabakia kama timu bora nchini kwa sasa.

Unaiona wapi Yanga kimataifa? Ukiniuliza swali hili jibu litakuwa ni hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Kama Mwamnyeto na Job watarudi kwenye ubao wao Yanga itasumbua sana msimu huu. Wamejaa ubora kwenye kila kona. Unapokuwa na watu kama Stephano Aziz KI, Bernard Morrison na Fiston Mayele hakuna kingine unachoweza kutarajia tofauti na hatua ya makundi.

Unapokuwa na walinzi kama Joyce Lomalisa na Djuma Shaban hatua ya makundi ndiyo picha pekee unayoiona. Baada ya kupita miaka 24 hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ndiyo zawadi kubwa mashabiki wa Yanga wanayostahili. Timu ifike kwanza hatua ya makundi, huko robo fainali au busu inapaswa kuwa ziada tu msimu huu. Kwa ushindani wa ndani Yanga watasumbua sana. Ni kama wanataka kurejesha heshima yao, lakini kimataifa sio wa kuwaamini sana. Wamekaa muda mrefu sana bila kuonyesha maajabu. Wamekuwa wanyonge sana, lakini naamini huu ndiyo wakati wao. Yanga Afrika dume imerejea na huu ni wakati wao wa kutuonyesha ufalme wao kimataifa.

Columnist: Mwanaspoti