Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Una uhakika Robertinho ni Mbrazili

Chama X Robertinho.jpeg Una uhakika Robertinho ni Mbrazili

Thu, 26 Jan 2023 Chanzo: Mwananchi

Clatous Chota Chama ndiye mchezaji mbunifu zaidi pale Simba. Pengine ndiye mchezaji fundi zaidi kwenye eneo analocheza kuliko mchezaji mwingine yeyote kwenye ligi yetu ingawa hili linaruhusu mjadala.

Hakuna namna unaweza kumueleza shabiki kuwa mchezaji huyu hana kasi na inabidi atolewe kabla ya dakika 30 za mchezo. Hakuna namna utamueleza mpenzi wa mpira mzuri tena dhidi ya timu kama Mbeya City kuwa Chama amechemsha na akaridhika.

Unapozungumzia ufundi, basi Chama ndiye ufundi wenyewe. Nadhani kuna muda makocha huwa wanatudanganya. Nadhani kuna namna makocha wanatulazimisha kuamini kuwa tunachoona sisi uwanjani ni tofauti na wanachoona wao.

Unamkumbuka fundi wa mpira Mesut Ozil? Unakumbuka wakati Real Madrid wanamuuza kwenda Arsenal namna Cristiano Ronaldo alivyokasirika? Unakumbuka namna alivyoshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka nchini Ujerumani mara tano? Alipofika Arsenal kuna kocha alijaribu kutudanganya kuwa Ozil hakuwa na kasi. Kuna kocha aliamua kutudanganya kuwa Ozil hana nguvu. Huku ni kudanganyana kiufundi.

Pale Simba, Chama ndiye Ozil wao. Ndiye kilainishi wa magari yote. Ndiye mchezaji ambaye kila kocha ungetegemea timu yake itaanza ujenzi kumzunguka yeye.

Kitendo cha Kocha Robertinho kutuaminisha kuwa Chama hana na alimhitaji zaidi Kibu Dennis ni kutudanganya kiufundi. Kocha anaheshimiwa kwa uamuzi wowote wa kiufundi, lakini hatukatazwi kutoa maoni yetu. Unamkumbuka Juan Mata yule wa Chelsea? Unamkumbuka fundi wa mpira aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa Chelsea kwa misimu miwili mfululizo kabla ya kuhamia Manchester United? Aliwahi kutudanganya kocha mmoja pale Manchester United kuwa Mata hana kasi.

Aliwahi kutudanganya kocha mmoja kuwa Mata hakabi. Huku ni kutudanganya kiufundi. Mata wote tunamjua. Fundi kwelikweli wa Kihispania. Tunaheshimu mtazamo wa makocha, lakini hatukatazwi kutoa maoni. Chama ni aina ya mchezaji ambaye anastahili kuanza na kumaliza mechi kwenye timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu nchini kwa sasa.

Ni mchezaji ambaye anaanza kikosi cha kwanza kwenye timu yoyote. Wachezaji wa namna hii huwa wanalindwa na makocha wengi ili kuchezesha timu. Sio rahisi kuwaeleza mashabiki wa Simba kuwa Chama hana kasi. Sio rahisi kueleweka unapomtoa mchezaji wa aina hii kabla ya dakika 30 za mechi. Sio rahisi. Hawa ni aina ya wachezaji ambao sababu pekee watu wanayoweza kuielewa ni ugonjwa tu.

Chama ana utulivu na ufundi ndani ya boksi la mpinzani pengine kuliko mchezaji mwingine yeyote wa kizazi hiki nchini. Timu inapokuwa na maswali magumu uwanjani Chama ndiye mwenye majibu. Wachezaji wa namna hii huwa hawatolewi mapema kwa sababu za kiufundi kwa sababu wao ndiyo ufundi wenyewe.

Kukaba sio kazi ya Chama. Kazi yake ni kuzifungua timu pinzani na kutengeneza nafasi za kufunga. Kazi yake ni kupasia mpira kwenye nyavu. Hapo makocha kuna namna huwa wanatudanganya kiufundi. Ubora wa Chama haujaja kwa sababu anajua kukimbia sana.

Dunia haijamtambua Ozil kwa sababu ya kukaba. Dunia haimheshimu Mata kwa sababu ana nguvu za kugongana na wapinzani, hapana. Hawa watu wana ufundi miguuni. Hawa watu wako fasta vichwani. Hawa watu wanarahisisha kazi kwa wafungaji wao. Watumike kwenye eneo hilo tu. Huku ndiko ufalme wao ulipo.

Haiwezekani mchezaji bora wa Ujerumani na Real Madrid aje akose kasi akiwa Arsenal. Haiwezekani mchezaji bora dhidi ya timu kama Al Ahly aje akose kasi mechi dhidi ya Mbeya City. Hapa kuna namna makocha huwa wanajaribu kutudanganya kiufundi. Tunawaheshimu sana, lakini hatukatazwi kutoa maoni.

Niliposikia Robertinho kutoka Brazil anakwenda kujiunga na Simba SC nilijua sasa Chama anakwenda kuzaliwa upya. Watu wa Brazil na staili ya Chama ni damdam, lakini imekuwa tofauti. Robertinho anahitaji mtu tofauti wa kuleta kitu tofauti.

Ukitazama mechi mbili za Simba chini ya Robertinho kwenye ligi bado huoni kilichoongezeka. Bado ni ngumu kuamini kama Simba iko imara bila Chama. Nadhani makocha kuna muda huwa wanajaribu kutudanganya kiufundi.

Chama bado anahitajika sana kwenye uchezaji wa Simba. Kama Chama hana kasi, basi wengine wakimbie na yeye alete ufundi tu uwanjani. Soka ni mchezo wa mbio, lakini huwezi kushinda mechi kwa sababu tu unakimbia sana.

Soka ni mchezo wa nguvu lakini huwezi kushinda tu mataji kwa sababu una wachezaji wenye nguvu. Unahitaji kuwa na uwiano sawa wa wachezaji wenye kasi na akili. Wachezaji wenye uwiano sawa wa nguvu na unyumbulifu. Kama Robertinho anamhitaji sana Chama, bado Simba inamhitaji mno Mwamba wa Lusaka.

Columnist: Mwananchi