Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Una tatizo na uzee wa Ntibazonkiza?

Saidoo Simba Una tatizo na uzee wa Ntibazonkiza?

Thu, 5 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Saido Ntibazonkiza inasemekana amezaliwa Mei Mosi 1987. Ukifanya hesabu utagundua kuwa ana umri wa miaka 35, lakini nani anajali kama bado anaweza kufunga hat trick? Hakuna. Ukiondoa Clatous Chota Chama, Ntibazonkiza anaweza kuwa mchezaji wa pili mbunifu zaidi kwenye ligi yetu. Haya ni maoni huru tu ambayo unaruhusiwa kuyabishia.

Wanaoupa heshima mpira wetu ni wachezaji wakubwa. Sisi sio EPL. Sisi sio La Liga. Sisi sio Bundasliga. Madhara ya kuwa na umri mkubwa kwenye soka yanaonekana zaidi kwenye ligi zenye mishemishe. Ligi zenye wachezaji wanaokimbia. Ligi zenye matumizi makubwa ya nguvu. Tanzania bado tuna ligi ambayo wachezaji wanakuwa bora zaidi wanapokaribia miaka 30 au juu ya hapo. Wachezaji wanakuwa wakomavu zaidi wanapokuwa juu ya miaka 30. Tanzania wachezaji wanachelewa sana kukomaa.

Watu kama Dennis Nkane, Abutwalib Mshery, Abdul Sopu, Crispin Ngushi walipaswa kuwa mastaa wakubwa kwenye ligi yetu kwa sasa. Lakini bado hawajakomaa. Walau Sopu anaanza kujipambanua pale Azam FC.

Vijana kwenye ligi yetu wanachelewa sana kubalehe. Angalia Peter Banda pale Simba. Anaonekana ni kijana mwenye kipaji cha hali ya juu, lakini amechelewa sana kukua. Chama Inasemekana amezaliwa Juni 18, 1991. Ukifanya hesabu hapo utagundua kuwa ana umri wa miaka 31. Sio mtoto kabisa.

Hakuna mchezaji yeyote wa kizazi hiki anayefikia uwezo wake. Wapo Wachezaji wachache ambao hukua mapema, lakini sio kuwa wafalme wa ligi yetu ni wachezaji wakubwa. John Bocco Inasemekana amezaliwa Agosi 5, 1989 kimahesabu atakuwa na miaka 33, lakini huoni mshambuliaji mzawa kijana anayefikia moto wake.

Ndiyo mpira wetu. Ndiyo kiwango chetu. Mchezaji mkubwa anayeshindwa kutamba Tanzania sababu haiwezi kuwa umri ni kiwango. Utapotea sana kama utatanguliza kigezo cha umri kutabiri ubora wa mchezaji.

Ntibazonkiza ni mchezaji wa kiwango cha juu kwenye ligi yetu. Bado atacheza sana. Ligi yetu haina kasi ya kumshinda. Ligi yetu haina matumizi makubwa ya nguvu ambazo hana. Yuko sambamba na vijana na amewaacha mbali. Kama unadhani Ntibazonkiza ni mzee imekula kwako.

Saido aliachwa na Yanga akiwa mchezaji namba mbili kwa mchango wa mabao nyuma ya Fiston Mayele. Aliwashinda vijana kibao pale Yanga. Saido ameondoka Geita Gold akiwa mchezaji namba mbili kwenye uchangiaji wa mabao na kuwazidi vijana kibao.

Mpira wetu unawahitaji zaidi wachezaji wenye umri mkubwa kama Ntibazonkiza. Vijana wetu bado wana utoto mwingi. Wanachelewa sana kukua. Wanachelewa sana kukomaa. Wale kina Thabaani Kamusoko, Meddie Kagere wote wamekuwa wafalme kwenye ligi ukubwani. Mpira wetu unahitaji zaidi wachezaji wakubwa kuliko vijana.

Ntibazonkiza hajawahi kuwa mchezaji wa kawaida kwenye ligi yetu. Atacheza Simba kwa msimu wake mmoja na nusu na anaweza kurudi tena Yanga au kwenda Azam FC na akacheza. Bado yupo yupo sana tu na tutamuimba sana.

Kuna muda msimu huu Simba iliyumba sana baada ya kumkosa Chama, lakini kwa ujio wa Ntibazonkiza naiona Simba imara zaidi.

Simba wamepata fundi mwingine wa kunogesha idara ya Ushambuliaji. Ana uwezo mkubwa wa kufunga. Ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga.

Hata Moses Phiri atakaporejea anaweza kuanzia pale alipoishia kwenye kucheka na nyavu. Mpishi mwingine wa nafasi za mwisho ameongezeka.

Wachezaji wakubwa ndiyo mastaa wa ligi yetu kwa miaka mingi tu. Fiston Mayele inasemekana amezaliwa Juni 24, 1994. Ni miaka 28 kwenye cheti lakini mkikutana unaweza kumuamkia. Ni mkubwa. Ndiye kinara wa mabao. Una tatizo na umri? Utakuwa na matatizo makubwa.

Ligi yetu wanaoiwezea ni wakongwe. Vijana wameachwa mbali sana kwenye ubora. Uzuri wa Ntibazonkiza ana uzoefu wa kutosha na hizi klabu kubwa.

Uzuri wa Ntibazonkiza tayari anafahamu siasa za mpira wetu. Haitamchukua muda kuwa mwenyeji pale Msimbazi. Siku chache zijazo atakuwa ni kama amezaliwa pale.

Umri mkubwa ni kigezo cha mwisho kwenye kusajili wachezaji wa kuja kucheza ndani ya ligi yetu.

Namuona Ntibazonkiza akizaliwa upya Msimbazi. Namuona Ntibazonkiza akimpunguzia mzigo mkubwa Chama. Naiona Simba ikiwa imara zaidi kwenye idara ya ushambuliaji.

Columnist: Mwanaspoti