Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ubalozi wa Mandonga na wafuasi wa Fei Toto, Manula

Mandonga Pic Data Karim Mandonga

Thu, 28 Jul 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Majuzi niliona mahali kwamba, bondia aliyechakazwa vibaya sana kule Morogoro katika moja ya yale mapambano ya ufunguzi wakati Twaha Kiduku anapigana kwa mara ya mwisho, Karim Mandonga amepata ubalozi katika moja ya maduka makubwa ya nguo hapa Dar es Salaam.

Kisa? Mandonga ni kati ya watu wanaofuatiliwa zaidi nchini kwa sasa. Ghafla kati ya wale mabondia maarufu tunaowafahamu limeongezeka jina la Mandonga.

Jinsi nchi yetu ilivyo! Bondia aliyepigwa amekuwa maarufu kuliko aliyempiga. Inachekesha na kushangaza kwa wakati mmoja. Unakuwaje maarufu kwa kupigwa?

Mandonga! ‚Mbwatukaji‚ kama alivyo! Anajua ‚kumkoga‚ mpinzani wake kwa maneno na vitisho visivyothamilika. Anazungumza kwa sauti ya juu akiwa amekunja ngumi akipiga kila aina ya mkwara na anataka mpinzani apate ‚meseji.

Ni hiki kitu watanzania wamekipenda kwake. Kwamba Mandonga anazungumza sana halafu hana uwezo wa kutisha. Mgeni akishuka nchini leo na kumsikiliza Karim Mandonga, anaweza kufikiri anamsikiliza Mike Tyson katika ubora wake au anaweza kufikiri Muhamad Alli amezaliwa tena Afrika Mashariki. Kumbe ni mtu tu wa Morogoro aliyewakamata watanzania kwa mdomo wake.

Ni hiki kilichompa Mandonga umaarufu kiasi cha kupata ubalozi. Usidhani anakuwa balozi bure. Lazima anapatiwa kiasi fulani cha pesa kwa matumizi ya jina na sura yake.

Kipindi kama hiki ambacho ana pambano linalomsubiri kule Songea, kila mtu anatamani kumsikia anavopiga mikwara ya kumuua mpinzani wake. Hapo ndipo wafanya biashara wanaona fursa na kumtumia Mandonga kujitangaza. Wao (wafanya biashara) wanapata nafasi ya kujitangaza na Mandonga anapata pesa kupitia sura na jina lake.

Ni hapo nilipokumbuka wachezaji wetu na kujiuliza swali tunalojiuliza kila siku, kwanini hawapati fursa hizi wanazopata akina Mandonga? Tazama wasanii wakubwa zaidi nchini wanavopiga pesa kwa matumizi ya sura zao.

Tazama wachekeshaji na wanahabari wakubwa wanavopiga pesa nje ya kazi zao kwa ubalozi? Nini huwatokea wachezaji wetu?

Nimetazama mtandao wa Instagram kwa haraka ambao kwa sasa ni kama Tanzania inaendeshwa huko, Fei Toto wa Yanga ana zaidi ya wafuasi laki tano. Lakini si balozi wa duka au kampuni yoyote. Jonas Mkude anaelekea kufikisha wafuasi laki saba sawa na Aishi Manula anayekaribia kufikisha wafuasi laki tisa lakini kama Fei tu na wenzao wengi hawapati pesa yoyote kupitia mitandao. Mchezaji pekee aliyefanikiwa ni beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Hussein ‚Tshabalala‚ anayefanya matangazo na kampuni kama tatu hivi zinazoeleweka.

Nini kinawatokea wachezaji wetu? Sijui kama ambavyo tu sijui wafanye nini ili kufaidika na majina yao. Hata Mandonga niliyemzungumza hapa nina uhakika hakupanga kufika hapa bali amejikuta tu watanzania wakiupenda mdomo wake na kumkuza ghafla. Kama tu ambavyo walimpenda Pierre Likwidi na Nabii Tito.

Vyovyote vile bado tuna kundi kubwa sana la wachezaji wasiofaidika na majina yao.

Bado wachezaji wengi wanategemea mishahara na posho kuendesha maisha yao. Naelewa kwamba hata kule Ulaya wapo wachezaji wengi wasiofaidika na majina yao lakini si wengi kama kwetu. Tofauti na Samatta na Tshabalala hatuna mchezaji mwingine anayefaidika na jina lake. Lazima kuna kitu hakipo sawa mahali.

Ni kama ambavyo nimekuwa nikiamini kwamba hatuna wachambuzi wengi waliocheza mpira. Baada ya Amri Kiemba na Ally Mayay kuna wapi wengine? Kule Ulaya studio unakuta mtangazaji amezungukwa na jopo la wachambuzi waliocheza mpira kwa mafanikio makubwa. Hawa ndie akina Jamie Caragher, Roy Keane, Garry Neville, Micah Richards, Rio Ferdinand na wengineo. Shida ni ipi haswa kwetu? Ukifuatlia wachezaji wengine watakuambia hawapewi nafasi, lakini sio kweli. Wengi wanashindwa kuelewa kwamba kucheza mpira hakukufanyi uweze kuuelezea.

Mfano rahisi tu, ni wachezaji wangapi leo wakifanya mahojiano baada ya mechi kumalizika watakuelezea vizuri kwanini wameshinda au kupoteza? Ni katika matukio kama haya unamgundua mchezaji gani anafaa kuwa mchambuzi.

Matokeo yake leo tuna vijana wengi sana waliosoma fani zingine lakini wanakaa studio kuchambua soka na wanachambua kwa umaridadi mkubwa sana. Ni kwasababu wachezaji wamesinzia na kuacha fursa hizi ziwapite.

Wangeamua kujifunza kuuelewa na kuuelezea mpira, tusingekuwa na wachambuzi wengi kutoka mtaani ambao hawajacheza. Hata mimi ningekuwai Kaliua nafundisha kama taaluma yangu inavyonitaka.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz