Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tuzike mjadala wa 'Goat' kwa Lionel Messi?

Messi Mkls.jpeg Lionel Messi

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Huwa nabishana sana na kijana wangu mmoja unapokuja mjadala kuhusu mchezaji bora wa muda wote. Yeye akiwa askari mtiifu kutoka kambi ya Lionel Messi, mimi nimekuwa upande wa Ronaldinho Gaucho kwa miaka mingi. Nitamzungumzia Gaucho siku nyingine, leo twende kwanza na Messi. Kwamba Messi ndiye mchezaji bora wa muda wote kwasababu ametwaa Kombe la Dunia?

Rafiki yangu mmoja alieleza vema mahali kwamba anafikiri hata kama Messi asingetwaa ubingwa wa dunia bado anaamini angeendelea kuwa mchezaji bora wa muda wote. Kombe la Dunia limepiga tu msumari wa mwisho katika jeneza la waumini wa soka la zamani ambao wamekuwa wakimkataa Messi kuwa mbele ya Maradona na Pele kwasababu hakubeba Kombe la Dunia.

Rafiki yangu mwingine asiye na kazi kwa sasa kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo, Haji Sunday Manara, yeye alibandika picha ya Pele katika mtandao wa Instagram na kusema Pele ndie mchezaji bora wa muda wote. Kisa? Pele ametwaa mataji matatu ya Kombe la Dunia. Halafu akamalizia kwa kusema, “Hakuna kitu chochote kinachofanyika sasa hivi ambacho Pele hakufanya.”

Bado sijakutana na Haji tangu ipigwe fainali siku ya Jumapili. Lakini nitakapokutana naye nitageuza maelezo yake nimuulize, “Kipi kilifanyika zamani na Pele ambacho Messi hajafanya?”

Kwa sasa mzani unaonekana kuwa kati ya Pele na Messi. Naona hata mashabiki wa Ronaldo wa Ureno wamehamia kwa Pele kwasababu wanaona mzani unaelemea kwa Messi zaidi. Zamani mjadala ulikuwa kwamba Messi hana taji la dunia, sasa hivi wameibuka na haya mataji matatu ya Pele kujitetea nayo. Hapo kwa Pele tunaweza kujiuliza maswali kadhaa kama kutoa hukumu.

Kwanza Pele amecheza soka lake nyumbani kwao Brazil kwa miaka mingi kabla ya kwenda Marekani. Hakuwahi kufika Ulaya ambapo soka limekuwa la ushindani mkubwa kwa miaka mingi. Hapa tunaweza kumtetea kwamba alicheza zama ambazo haikuwa rahisi sana kuvuka ng’ambo. Lakini tukumbuke aliondoka na kwenda Marekani akiwa bado na nguvu za kutosha kucheza soka la ushindani.

Lakini hapo unazitazama takwimu za Kombe la Dunia ambazo zinatumiwa kutoa hukumu, Pele amefunga mabao 12 katika mashindano yote ya Kombe la Dunia aliyoshiriki. Messi amefunga mabao mangapi? Mabao 13 katika mashindano matano.

Kwa hiyo tayari Messi amemuacha Pele kama tutaamua kutazama mabao. Lakini hapo tukumbuke tayari bwana mdogo Kylian Mbappe amefikisha mabao 12, sawa na Pele. Hapohapo tukumbuke Pele ana mabao 77 ya kimataifa sawa na Neymar ambaye bado ataendelea kuichezea Brazil. Pia Ronaldo ana mabao 118 akiwa na timu yake ya taifa ya Ureno hivyo amemuacha mbali Pele katika orodha hii. Lakini Messi pia ana mabao 98 ya kimataifa akiwa na Argentina hivyo amemuacha mbali Pele katika orodha hii.

Nafikiri makombe matatu ya dunia aliyotwaa Pele ni kwasababu alikuwa na timu imara na alizungukwa na mastaa makubwa kama kina Mane Garincha. Haikuwa kwasababu ya jitihada zake binafsi. Hata mara hii Messi amefanikiwa kutwaa Kombe la Dunia kwasababu nyuma yake alikuwa na timu inayocheza kwa ajili yake.

Hakuwa na timu imara sana kama ile ya 2014 au kama walivyo Ufaransa lakini alikuwa na watu waliokuwa tayari kupigana kwa ajili yake. Mara nyingi mataji ni suala la timu zaidi kuliko mchezaji binafsi.

Nafikiri Kombe la Dunia la Messi limefanikiwa tu kuwaziba midomo wale waumini wa soka la zamani ambao wanaamini kila kitu kilikuwa zamani. Lakini kama ni suala la ubora Messi alishalithibitisha muda mrefu uliopita na ubingwa wa dunia hauongezi chochote kikubwa katika ubora wake.

Bado naamini wanaomkataa Messi mbele ya Pele ni wale watu wasioamini katika dunia ya kisasa. Ni wale watu wanaoamini kila kitu kizuri kilikuwa zamani. Ukiwauliza kuhusu muziki wanakuambia muziki ulikuwa zamani.

Mavazi yalikuwa zamani na soka lilikuwa zamani. Pengine miaka 30 ijayo hili kundi kubwa linalomkataa Messi sasa hivi watakubali kwamba Messi ndie mchezaji bora kuwahi kutokea katika historia. Tupo katika dunia inayopenda zamani.

Columnist: Mwanaspoti