Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tupunguze lawama pambano la Simba na Yanga

Derby Pic Pambano la Watani wa Jadi

Thu, 9 Dec 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Safu ijayo ya UBISHI WA MZEE WA KALIUA baada ya hii iliyopo machoni mwako sasa itakujia ukiwa na furaha au huzuni ya matokeo utakayopata mbele ya mtani wako wikiendi hii pale Temeke.

Labda pambano litaisha sare kisha wewe na mtani wako mtalazimika kumeza maneno mliyoandaa kutamba nayo baada ya kupata ushindi. Ninasema haya nikiamini katika Watanzania kumi, walau tisa wanashabikia Simba au Yanga.

Wapo wapi watu wanaoshabikia timu zingine nchini? Vyovyote ilivyo, haliji pambano lingine kubwa zaidi nchini kulizidi hili la Simba na Yanga. Halijawahi kuja pambano kubwa zaidi ya hili nchini. Labda halitakaa lije pambano kubwa zaidi ya hili. Labda!

Sijui kitatokea nini uwanjani Jumamosi, lakini ninachojua nitapata kitu cha kubishana hapa Jumatano ijayo. Simba na Yanga hawajawahi kukosa mada ya kuweka mezani tujadili. Sijui nini kitakuwa gumzo zaidi safari hii. Matokeo? Refa? Mashabiki? Viongozi? Wachezaji? Nidhamu? Sijui. Ninachojua kipo kitu kitatokea na tutapata mada ya kubishana wiki ijayo. Mechi kubwa nchini haiwezi kukosa stori.

Kama kawaida, mechi ya Simba na Yanga haiwezi kwisha bila lawama. Anayefungwa lazima atafute wa kumtupia lawama. Lawama nyingi hupelekwa kwa mwamuzi. Kama siyo mwamuzi basi ni mchezaji aliyefanya makosa. Kama siyo mchezaji basi lawama zitakwenda kwa kocha. Mara nyingi lawama kama hizi hazina msingi wowote.

Katika lawama ambazo huumiza masikio yangu ni zile unazosikia mtu akihoji “mechi kubwa kama hii refa anatoaje penalti rahisi vile?” Mwingine utasikia akilalamika “mechi kubwa kama hii refa anatoaje kadi ya pili ya njano kwa mchezaji? Alitakiwa kubalansi mechi.” Shabiki mwingine utasikia akilalamika kwamba ìrefa ametoaje penalti ya mapema vile katika mechi kubwa kama hii?î

Wanachosahau mashabiki wengi ni kwamba ukubwa wa mechi ya Simba na Yanga hauzibadili sheria za soka. Sheria inayotumika kuamua mechi ya Mwadui na Geita ndiyo inayotumika kuamua mechi ya Simba na Yanga. Tusitake sheria za mpira zipindishwe kisa ukubwa wa mechi.

Tunaweza kulalamika lakini tulalamike kwa hoja za msingi. Hata huko Ulaya Mashabiki na makocha hulalamika, lakini huwezi kusikia akilalamikia penalti ya dakika za mwisho kisa ukubwa wa mechi. Refa wa Uingereza, Michael Oliver aliwahi kuwapa Real Madrid tuta la dakika ya tisini na nne katika mchezo wa robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Juventus baada ya rafu nyepesi ya Mmrocco Mehdhi Benatia kwa Lucas Vazquez. Tuta lililoiondoa Juventus katika mashindano.

Carlos Sanchez wa Colombia alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya tatu tu katika mchezo wa makundi ya fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Japan.

Matukio haya yalitendeka katika mechi kubwa zaidi ya Simba na Yanga, lakini sheria haikufumba macho kuangalia ukubwa wa mechi. Mashabiki wa Simba na Yanga wanapaswa kuelewa sheria haipindi kwa sababu ya ukubwa wa mechi.

Watu wengine ambao hushushiwa lawama kando ya waamuzi ni wachezaji na makocha. Hapa mashabiki huwalaumu zaidi wachezaji wa timu yao ambao wamefanya makosa wakaadhibiwa au wamechezea nafasi za wazi.

Kinachochekesha kuhusu lawama hizi ni kwamba, mchezaji anaweza kufanya kosa kama hilo mechi ya Simba au Yanga dhidi Mwadui na mashabiki wasilalamike, lakini mechi ya mtani watamtafuna kwa maneno.

Miaka miwili iliyopita Aishi Manula alichukiwa na kila shabiki wa Simba baada ya kutunguliwa bao la mbali na Mapinduzi Balama. Ajabu ni kwamba ni mashabiki hao walikuwa wanakiri wazi kwamba udhaifu mkubwa wa Manula ni kuruhusu mabao ya mbali. Sijui kwanini walimchukia ghafla wakati waliutambua udhaifu wake.

Makocha hulalamikiwa kuhusu mabadiliko na aina ya wachezaji wanaowachagua kucheza mechi. Tunasahau kwamba wachezaji wote waliopo Simba na Yanga wamesajiliwa ili wacheze. Tukumbuke pia hakuna kocha anayepanga kikosi chake ili apoteze.

Kila kocha anaingiza timu uwanjani kusaka ushindi. Kama hajafanya kama tunavyotaka ni vyema tukaelewa kwamba zipo sababu za msingi kufanya hivyo. Tuache kuwataka makocha, wachezaji na waamuzi kuwa malaika. Tuwapunguzie presha kwa kuacha lawama zisizo na msingi.

Columnist: Mwanaspoti