Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Simba wanarudi vichwa juu, kipi kinafuata?

Simba Orlandooo Kikosi cha Simba SC

Thu, 28 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kazi ilionekana imekwisha kwa Simba pale mwamuzi Bernard Camill kutoka Shelisheli alipoenda pembeni kutazama ‘screen’ za usaidizi kujiridhisha kama kosa la Chris Mugalu lilistahili adhabu ya kadi nyekundu.

Ulikuwa mchezo mbaya kutoka kwa Mugalu na asingepona kwa namna yoyote ukizingatia tayari alikuwa na kadi ya njano ya kwanza.

Hata kama isingekuwa kadi nyekundu ya moja kwa moja lazima angeonyeshwa kadi ya njano ambayo ingekuwa ya pili na ingefuatiwa na nyekundu hivyo lazima angeenda nje.

Tangu hapo mechi ilizidi uzito mara mbili zaidi kwa Simba na dakika moja baadae walikuwa nyuma kwa bao moja. Hata kabla ya kadi tayari walikuwa wakiteseka kuwazuia Orlando Pirates.

Mateso ambayo waliyategemea kabla ya kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Simba walijua watakutana na moto Afrika Kusini kutokana na matokeo ya Dar es Salaam. Walitegemea kukutana na Orlando Pirates inayoshambulia muda mwingi wa mchezo.

Kando ya mbinu za kocha kitu kingine kikubwa ambacho Simba walihitaji ni uvumilivu. Walihitaji kuvumilia kukimbizwa na kushambuliwa mfululizo na kweli walikuwa wavumilivu kwa dakika zote 90.

Tangu mwanzo waliingia wakijua wanapaswa kulinda bao lao moja walilolipata nyumbani Uwanja wa Mkapa.Hiki ndicho kitu cha kwanza mashabiki wa Simba wanapaswa kujivunia. Kuelewa matokeo ulionayo na kujua unatafuta nini katika mechi husika ilikuwa changamoto kubwa inayowatafuna Simba katika viwanja vya ugenini katika mechi za kimataifa.

Simba walikuwa hawaamini kama viwanja vya watu Afrika siyo sehemu ya kujilinda, bado walikuwa wanaamini katika kupishana na mpinzani kutafuta matokeo. Haishtui kuona ambavyo walikuwa wakiruhusu mabao mengi katika viwanja vya watu. Lakini safari hii walionyesha ukomavu kukaa nyuma na kulinda lango kwa nidhamu muda wote.

Sina hakika kama wamejifunza moja kwa moja jinsi ya kucheza katika viwanja vya watu au ilikuwa katika mechi ya Orlando pekee, lakini hata katika zile mechi za makundi awamu hii waliruhusu mabao mengi ila mpango wao mama ilionekana ni kuzuia. Huo ni ukweli wa soka la Afrika ambao Simba walipingana nao kwa muda mrefu. Inaelekea sasa hivi wamejifunza.

Hata Al Ahly na ukorofi wao hukaa nyuma ya mpira wanapocheza ugenini. Kitu kingine walichokikosa Simba ni kile nilichosifia awali, uvumilivu. Unapocheza ugenini katika viwanja vya Afrika unapaswa kuwa mvumilivu kuanzia nje ya uwanja.

Unapaswa kuwa na hakika ya mapokezi mabaya, kufanyiwa fitina hotelini na uwanjani, kupandikiziwa Uviko-19 feki na figisu nyingine nyingi. Baada ya hapo unakutana na mateso ya uwanjani. Unapaswa kujiandaa kukabiliana na yote haya.

Nadhani licha ya fitina tulizosikia bado Simba walionyesha wanaweza kufanya nini pale Soweto. Kutolalamika kwao kunaonyesha ni jinsi gani wamezoea kucheza soka la Afrika. Nafikiri ugonjwa mkubwa wa Simba na Tanzania kwa ujumla ulikuwa katika mipira ya kutenga na ile ya krosi. Safari hii kwa kiasi kikubwa Simba wamepambana kuutibu ugonjwa huo.

Mechi ya Orlando Pirates walishambulia sana kupitia pembeni na walitupia krosi nyingi kwenye sanduku la Simba, lakini Aishi Manula na mabeki walipambana nayo vizuri. Kuongezeka kwa yule Henock Inonga katika ukuta wa Simba kumewaongezea ufanisi wa kupambana na mipira ya juu. Wanachohitaji sasa Simba ni kuanza maandalizi ya msimu ujao mapema. Bahati njema ni kwamba wana uhakika wa uwepo wa nafasi nne walizotengeneza wenyewe.

Hata kama watakosa ubingwa wa ligi ambao unaonekana unakwenda kwa watani zao - Yanga, bado wana uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

Wanahitaji kuanza maandalizi ya kufahamu wachezaji wa kuwasajili mapema na kuwaongezea mikataba wale ambao muda wao unatamatika. Tabu ya kupoteza wachezaji muhimu kikosini kila mwisho wa msimu inakufanya kuanza upya kila siku. Kina Joash Onyango wanapaswa kushawishiwa wabaki na Inonga. Kina Mugalu na Wawa wanahitaji kutafutiwa mbadala. Wanatafutwa lini? Wakati ni sasa kisha kutekeleza dirisha lijalo la usajili.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz