Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Simba walipojaribu kumpata samaki ndani ya nyoka kwa Morrison

Barbara Morisson CEO wa Simba ,Barbara Gonzalez akiwa na Morrison

Thu, 17 Feb 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Katika rundo la wale wasanii wa kizazi kipya wanaoimba kwa ile staili ya kufoka, yupo mmoja aliyewahi kusema, “Simba kula mtu ni habari, lakini mtu kula Simba ni habari ya kusisimua.”

Alichomaanisha? Haishtui simba kula mtu. Lakini ni tofauti kama itatokea mtu kumla Simba. Ndivyo unavoweza kusema kwa mchezaji raia wa Ghana aliyevurugana na Simba hivi majuzi, Bernard Morrison. Haishtui sana kusikia Morrison amefanya kituko nje ya uwanja kinyume na taratibu. Inashtua zaidi unapoona Morrison yupo kimya na kila kitu chake kipo sawa.

Morrison hapendi kutoka midomoni mwa watu. Anapenda zaidi kuonekana katika kurasa za mbele za gazeti, kama si kwa uzuri basi ubaya.

Wiki iliyopita alikuwa mbele ya kila kurasa ya gazeti ikiwemo Mwanaspoti baada ya kufungiwa na klabu yake ya Simba kwa kile walichodai ni kutokutii sheria kwa kuondoka kambini kinyume na utaratibu mara kwa mara.

Huyu ni mchezaji wa kimataifa anayecheza soka la kulipwa. Simba wameamua kumchukulia hatua ya kumsimamisha wakati wanatafuta ufumbuzi wa suala lake.

Kabla ya hata kumuhoji Morrison, Simba wana swali la kwanza la kujibu. Kama Morrison amekuwa na tabia ya kutoka kambini kinyume na utaratibu mara kwa mara kama taarifa inavyosema, je alichukuliwa hatua gani mara zote alizofanya kitendo hicho? Haiwezekani mchezaji afanye kosa hilo hilo kila siku kama anapatiwa adhabu kali.

Lazima Morrison amekuwa akifanya hivi mara kwa mara na Simba wamekuwa na tabia ya kumfumbia macho. Kinachotokea sasa hivi ni matunda ya kile walichokipanda mapema.

Najua jibu watakalotoa Simba watakapoulizwa kama walimchukulia Morrison hatua huko nyuma.

Watakuambia tumempatia onyo kali mara nyingi. Lakini ukweli unabaki klabu kubwa nchini zina tabia ya kukumbatia na kuficha dhambi za mastaa wake.

Huwa nidhamu inakuwa ya mwisho kabisa kuizingatia kwa mchezaji.

Inapotokea mchezaji anafanya vizuri uwanjani basi matendo yake ya nje ya uwanja huwa hayazingatiwi hadi ‘mambo yanapofika maji ya shingo.’

Matokeo yake ndiyo mchezaji anafika hatua ya kuipanda timu kichwani kama ilivotokea kwa Morrison.

Lakini hapo unageuka na kumtazama Morrison mwenyewe.

Mchezaji wa kulipwa unaishi vipi maisha ya kihuni ya kutokuheshimu taratibu?

Kwa Morrison jibu ni rahisi tu amegundua Tanzania ‘tunaishi kisela sana.’

Amegundua ukishakuwa staa kwenye timu una haki ya kufanya chochote kwa sababu utatetewa na kila mtu. Mashabiki na viongozi wanakuwa watetezi wako kwa kila unalofanya- cha muhimu wewe wape raha ndani ya uwanja.

Ni maisha ya kisela ambayo yanampa kiburi na nafasi mchezaji kutokufuata taratibu.

Wachezaji wa kulipwa kote duniani wanaishi maisha magumu chini ya sheria. Si kwamba kina Ronaldo sio watukutu lakini wanalazimika kuficha makucha yao kutokana na mishahara wanayolipwa. Wanalazimika kuheshimu kitita cha pesa wanachopokea kila mwisho wa wiki.

Ni kama ambavyo zimewahi kutokea baadhi ya kesi za wachezaji nchini ‘kuripoti kambini wakiwa wamevaa miwani’. Hakuna tabu yoyote kwa mchezaji kukata kinywaji.

Tabu inapokuja pale kinywaji kinaposababisha ushindwe kutimiza majukumu yako ya kikazi kama mchezaji.

Hata akina Jordan Henderson wa Liverpool ni walevi wazuri na wanatii kiu zinazosumbua makoromeo yao lakini kamwe hawawezi kuukubali kinywaji kiharibu kazi zao. Ni kuelewa unapaswa kufanya nini na kwa wakati gani.

Nini kifuatacho kwa Morrison? Nadhani mmoja kati ya Simba na Morisson anaweza kumpatia mwenzake talaka. Morrison amebakiza miezi isiyozidi sita katika mkataba wake na Simba.

Simba wanaweza kukubali aondoke kwasababu ya usumbufu ambao amekuwa akiufanya.

Swali litakalofuata ni anaelekea wapi? Simuoni Morrison akivaa jezi ya timu kama Namungo kwa sasa. Kama atasalia nchini basi atabaki Azam au Yanga. Je Yanga wapo tayari kumsamehe?

Bila shaka Yanga wanaweza kufumba macho na kumrejesha jangwani, tabu ni je wataweza kuishi naye?

Alikwisha waonyesha makucha yake miaka miwili nyuma kabla ya kwenda kwa majirani zao walioamini wanaweza kuibadilisha tabia yake.

Je Yanga wataweza kumbadilisha? Sidhani kama nyoka anaweza kubadilika kuwa samaki hata ukimfuga nyumbani kama samaki.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz