Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Simba, Biashara wametuonyesha safari tuliyonayo kufika nchi ya ahadi

Simba Data Mchezo wa Simba dhidi ya Jwaneng

Thu, 28 Oct 2021 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna mambo yanakera sana. Yanakera sana. Unapopata hisia kwamba tumepiga hatua moja mbele kuelekea katika mwelekeo sahihi, ghafla linatokea tukio la ajabu la kukuvunja moyo linaonyesha kwamba bado tuna safari ndefu sana ya kwenda. Inakera sana.

Ilikuwa wikiendi ngumu na chungu kwa Simba na Biashara United baada ya wote wawili kuondoshwa kizembe katika michuano ya kimataifa. Siwazungumzii Azam kwa sababu kwao hakukuwa na uzembe uliofanyika, walifanya kila walichoweza, lakini mwisho wa siku timu bora ilishinda na kusonga mbele. Tofauti ya Pyramids na Azam FC ni kifo na usingizi. Pyramids wamewaacha mbali sana Azam. Leo tuwajadili kidogo Simba na Biashara.

Tuanze na nani? Tuanze mbali kidogo na Dar es Salaam kwa wanajeshi wa mpakani, Biashara Mara. Baada ya ushindi wa mabao mawili kwa bila nyumbani, waliondoshwa baada ya kushindwa kufika uwanjani mchezo wa marudiano. Kisa cha kushindwa kufika uwanjani kwa wakati? Walishindwa kusafiri kwa wakati, kisa cha kushindwa kusafiri kwa wakati? Walikosa fedha za kuwasafirisha.

Hapo ndipo masikitiko yanapoanzia. Timu inayoshiriki Ligi Kuu katika karne ya 21 tena ikiwa kati ya nne bora nchini inakosa vipi pesa ya kusafiria? Jibu lake linaonyesha ni kwa kiasi gani klabu zetu ni maskini. Ndiyo! Maskini! Mnisamehe kwa kutumia lugha ngumu kidogo. Umaskini wa klabu unasababisha tuwe na ligi maskini. Ligi maskini inasababisha kila mtu na kila kitu kuwa maskini. Ligi maskini inazalisha wachezaji kuwa maskini, waamuzi maskini, makocha maskini, viongozi wa timu maskini na kila mtu maskini.

Huu umaskini ndio unafanya kelele za rushwa zisiishe katika mpira wetu.

Lakini hapohapo tunagundua ni kwa kiasi gani sisi ni maskini wa utawala na mipango. Biashara United walifahamu kuwa watashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu ligi ilipomalizika miezi minne iliyopita. Advertisement

Walifahamu kuwa watasafiri kwa ajili ya mechi za mtoano. Walipaswa kujiandaa mapema, hata kama ingekuwa kutembeza bakuli ilimradi kukwepa hii aibu iliyolikumba taifa.

Siamini kama Biashara ingekosa wahisani wa kuisafirisha. Kama wapo walio tayari kutoa pesa ili Biashara wamfunge Simba siamini kama wangeshindwa kutoa mchango wa kufanikisha safari ya Biashara. Nafunga mjadala nikikubali kukosolewa kwamba wametupa nje ya Shirikisho kizembe.

Zaidi ya kilomita 1000 kutokaa Mara, Simba nao waliondoshwa kizembe nyumbani Dar es Salaam baada ya kushinda kwa mabao mawili kwa bila ugenini, kisha kwenda mapumziko wakiongoza bao moja kwa bila walikubali kufungwa mabao matatu ndani ya dakika 45 kipindi cha pili na kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya kuona wanaongoza kwa tofauti ya mabao matatu wachezaji wa Simba waliamini mechi imeisha, wakaamini wapinzani wao ni wepesi. Kilichotokea wapinzani wao wakakimbia mara mbili zaidi yao kisha wakafanikiwa kuwafungua Simba na kuweka kambani mabao matatu yaliyowafikisha hatua ya makundi.

Hapo unajiuliza swali. Kwa wachezaji wa timu kubwa kama Simba unatumbukia vipi katika mtego wa kumdharau mpinzani wako kabla mechi haijaisha? Unaweza kusalimika kama utamdharau mpinzani wako katika Ligi Kuu Bara, lakini siyo Ligi ya Mabingwa Afrika. Kule lazima utalipia adhabu ya dharau zako.

Masikitiko mengine yalikuja baada ya mechi ya Simba kutamatika na baadhi ya viongozi kumwaga lawama katika mitandao ya kijamii. Tajiri aliongoza shutuma kwa kudai yupo mchawi aliyesababisha Simba kufanya vibaya na kutupwa nje na anaomba uongozi wa Simba umuwajibishe. Kwa mantiki hiyo haamini walistahili kutolewa na Jwaneng Galaxy, labda ni kweli Simba hawakustahili kuondoshwa na timu ya hadhi ile ya Jwaneng, lakini kwani lazima iwe wamehujumiwa? Kwani hauwezi kukubali kwamba tuliondolewa na timu bora zaidi kiufundi? Tuseme ni kweli lipo tatizo la hujuma ndani ya Simba, je tatizo linaisha unapolalamika katika mitandao ya kijamii?

Mwisho wa siku tukubali ukweli kwamba, tuna safari ndefu sana ya kwenda kisoka kama taifa. Kuanzia kwa wachezaji, uongozi, mashabiki, ligi na kila mtu na kila kitu. Tuna safari ndefu ya kwenda.

Columnist: Mwanaspoti