Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Picha nyingine nyuma ya beki wako Farid Mussa

Fard Mussa Malick Farid Mussa

Fri, 11 Mar 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Maisha yanavyobadilika! Ghafla macho yetu yamemshuhudia Farid Mussa akicheza upande wa kushoto wa Yanga kama beki.

Nani aliwahi kufikiria Farid Mussa anaweza kuanza mechi kama mlinzi? Farid anaingia katika kundi la wale wachezaji tuliowahi kuamini si walinzi wazuri.

Mara nyingi Farid anapocheza kama winga, utasikia watu wakisema tatizo la Farid ni ‘hakabi’.

Wengi tunaamini winga mzuri ni yule anayerudi nyuma kusaidiana na beki wake wa pembeni kuzuia.

Farid hayupo hivyo ndiyo maana inashtua kiasi kumtazama akicheza beki.

Kama tu hafanyi vizuri kumsaidia beki wake wa pembeni kuzuia akicheza kama winga, vipi akicheza beki ambapo jukumu lake mama ni kulinda?

Licha ya hayo, mechi kadhaa alizopangwa kucheza beki wa kushoto, Farid amecheza vyema tu. Yanga hawakukumbuka wanawakosa mabeki wao wa kushoto.

Imekuwaje Farid akamudu kucheza beki wa kushoto licha ya kutokuwa mzuri katika kuzuia?

Sababu kubwa ni ukweli Yanga wana timu imara sana kiasi ambacho wakiwakosa baadhi wachezaji wachache hawateseki.

Yanga wanaweza kumkosa beki yoyote wa pembeni kisha kocha akaamua kumweka uwanjani beki wa katikati na akaingia kwenye mfumo vizuri.

Yanga wanaweza kumkosa Djuma Shaban, kocha akaamua kumchezesha Dickson Job na Yanga isipate matatizo. Ni kwa sababu wana wachezaji wazuri maeneo mengine hivyo wanafukia madhaifu ya mwenzao ambaye anacheza katika eneo ambalo hajazoea kulicheza.

Sababu nyingine ni aina ya mchezo wanaocheza Yanga. Siku hizi Yanga wanatandaza soka safi la ardhini.

Wanamiliki mpira kwa kiasi kikubwa hivyo ni ngumu sana kuwashambulia. Muda mwingi Yanga wanakuwa kwako wakikushambulia au wanakuwa kwao wakiuchezea mpira. Hii inawapa likizo mabeki wao, wanakuwa hawana kazi nzito ya kufanya.

Timu isiposhambuliwa beki anakuwa na kazi gani nyingine ya kufanya uwanjani zaidi ya kutalii?

Hapo unarudi na kumsifia kocha kwa kuitengeneza timu yake kucheza mchezo ambao unaruhusu kutumia wachezaji tofauti.

Pia unamsifia kwa kufanikiwa kuelewa maeneo tofauti anayoweza kumchezesha mchezaji na bado akapata ubora wake.

Si waalimu wote wanakuwa na huu uwezo. Nabi anaonekana kuwa mtaalam zaidi katika hili suala la kubadili nafasi za wachezaji.

Tazama jinsi alivomsogeza Fey Toto kwenye kiungo wa kushambulia. Sasa hivi tunamtazama Fey Toto anavofanya vizuri na kugundua kumbe zamani tulikosea kumchezesha kiungo wa kukaba.

Unamtazama Yanick Bangala anavocheza kwenye eneo la kiungo, unaishia kushangaa unapokumbuka kwamba alikuja nchini kama beki wa kati.

Hadithi ni hiyohiyo kwa beki mwingine wa Yanga anayeuguza mguu wake kwa sasa, Shomary Kibwana aliyesogezwa beki wa kushoto baada ya ujio wa Djuma Shaban.

Lakini wakati unamsifia kocha Nabi, wazo lingine linaweza kukivamia kichwa chako ‘labda Nabi hawaamini sana mabeki wake wa kushoto.’

Unaweza ukamwelewa Nabi zile mechi za kwanza za Farid kwa kuwa hakuwa na beki yoyote wa kushoto. Wote walikuwa wakisumbuliwa na majeraha.

Lakini mechi dhidi ya Kagera Sugar Yanga walikuwa na Yassin Mustapha benchi lakini kocha aliamua kumchezesha Farid. Unaweza kusema ni kwa sababu Yassin alitoka katika majeraha lakini hayakuwa majeraha ya muda mrefu kiasi cha kumshinda kuanza mechi.

Ni kama ambavyo Kibwana Shomari amekuwa akitumika upande wa kushoto wakati siyo eneo lake la asili. Kwa jinsi Fulani unaweza kusema Nabi hawaamini sana mabeki wake wa kushoto.

Hili linapaswa kutoa picha kwa uongozi wa Yanga ya wapi pa kuanzia litakapofika dirisha kubwa la usajili. Bado wanahitaji kumtafutia kocha beki wa kushoto wa uhakika kama walivyofanya kwa Djuma Shaban upande wa kulia.

Walimsajili Bryson David dirisha lililopita lakini inaonekana Nabi bado hajaridhika ndiyo sababu aliamua kumhamisha upande Kibwana.

Tatizo linakuja, watampata wapi beki wa uhakika wa kushoto? Sidhani kama yupo beki wa kushoto wa uhakika nchini Zaidi ya Mohamed Hussein wa Simba ambaye hawawezi kumpata.

Labda wakubali kuvuka mipaka kumtafuta beki wa kimataifa. Bado wana nafasi moja ya mchezaji wa kimataifa.

Watakubali kuitumia kwa ajili ya beki? Ni swali gumu kujibu kutokana na ukweli kwamba tuna tatizo kubwa kama nchi la wachezaji eneo la kiungo na ushambuliaji.

Lakini pia sidhani kama Yanga wenyewe wanafurahi kumwona Farid akicheza beki wa kushoto. Wanahitaji mtu.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz