Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Nilivyowaona mashabiki wa Tanzania mechi ya kufuzu Qatar

Senegal Pic 2 Data Nilivyowaona mashabiki wa Tanzania mechi ya kufuzu Qatar

Thu, 7 Apr 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Niliwatazama mashabiki wa Nigeria wakiuvamia uwanja na kuleta vurugu baada ya kuondoshwa na Ghana katika mchezo wa kufuzu kombe la dunia la Qatar nikawakumbuka mashabiki wenzangu wa Tanzania.

Kabla ya hapo niliwatazama mashabiki wa Senegal wakikazana kumulika nyuso za wachezaji wa Misri nikawakumbuka tena mashabiki wenzangu wa Tanzania.

Siku moja nyuma kabla ya haya matukio niliwakumbuka tena mashabiki wenzangu wa Tanzania baada ya kuwatazama mashabiki wa Algeria wakigombania tiketi za kuingia uwanjani kutazama mechi yao dhidi ya Cameroon. Walikuwa wengi ‘kama wale wadudu waitwao kumbikumbi pindi mvua zinakaribia kuisha’

Kwanini niliwakumbuka mashabiki wenzangu wa Tanzania? Nitakueleza. Kitendo cha wanigeria kuvamia uwanja baada ya filimbi ya mwisho huku wakiwafanyia vurugu mashabiki wa Ghana ilikuwa kashfa kubwa kwa taifa la Nigeria.

Lilikuwa tukio lililoshtua dunia na kupigiwa kelele, hata wizara ya michezo Nigeria ilikemea uhuni uliofanywa na raia wake na kuwaomba radhi mashabiki wa Ghana waliodhurika.

Ni hapo nilikumbuka vurugu ambazo hufanywa na mashabiki wa soka nchini haswa wale wa Simba na Yanga. Najaribu kukusanya viganja vyangu nihesabu ni mara ngapi nimeshuhudia mashabiki wa Simba na Yanga wakifanyiana vurugu pale kwa Mkapa, bado sipati idadi kamili kutokana na wingi wa matukio niliyoyashuhudia. Vidole havinitoshi kuhesabu matukio yote ya kihuni niliyoyashuhudia yakifanywa na mashabiki wa Simba na Yanga nchini. Hawa ndio wanaongoza kwa kufanyiana vurugu wenyewe kwa wenyewe, kutupa chupa za maji uwanjani, kutukanana, kung’oa viti na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Kumbe wakati dunia wanaishangaa Nigeria kwa uhuni waliowafanyia Ghana, kwetu sisi ni maisha ya kawaida tulioyazoea.

Ndiyo! Ni maisha tuliyoyazoea. Yanaachaje kuwa maisha tuliyoyazoea kama yanajirudia kila siku? Ni mara ngapi tumesikia TFF wakitoa adhabu kwa klabu kwasababu ya vurugu za mashabiki?

Tumefika hatua ambayo hatushituki tena kusikia adhabu inayotokana na vurugu za mashabiki au kuona taarifa kutoka kwa klabu ikikemea uhuni unaofanywa na mashabiki. Wakati dunia inashangaa uwepo wa matendo ya kihuni kutoka kwa mashabiki sisi bado tunaishi huko na kuona ni kawaida.

Wasenegal na wao walikuwa na kituko chao. Waliingia uwanjani na ‘vitochi’ kwa ajili ya kuzimulika nyuso za wachezaji wa Misri. Kisa? Baadhi ya mashabiki wa Misri waliwamulika wachezaji wa Senegal katika mechi ya kwanza waliyopoteza kule Cairo. Walichokifanya hapa ni kuishi ule msemo wa ‘jino kwa jino.’ Walilipa kisasi kwa roho mbaya zaidi ya walichofanyiwa wao.

Hapo unaweza kukaa chini na kujiuliza, kama mashabiki wa Misri hawakuwamulika wachezaji wa Senegal ile siku kule Cairo, je Senegal wangewamulika wachezaji wa Misri katika mechi ya pili? Jibu ni hapana. Kwahiyo Senegal walihalalisha kufanya kosa kwa kosa walilofanyiwa.

Ni kama ambavyo tumekuwa tukifanya nyumbani Tanzania. Kuhalalisha kosa kwa kosa. Mwamuzi akitoa penalti isiyo sahihi kwa Simba, utasikia mashabiki wa Simba wakisema hata Yanga walipewa penalti isiyo sahihi mechi yao na Namungo.

Mwamuzi akiruhusu bao lisilo halali kwa Yanga, utasikia mashabiki wa Yanga wakisema hata Simba walipewa bao lisilo halali mechi yao na Mbeya Kwanza. Bado tunaishi katika ushamba wa kuhalilisha makosa kwa makosa yaliyowahi kutokea.

Tunasahau kwamba kosa ni kosa, ni sawa na kumuua ndugu wa mtu aliyemuua ndugu yako na kutaka lisiwe kosa kwasababu alitangulia kukukosea wewe. Ni ujinga.

Mwisho kabisa kulikuwa na gumzo la mashabiki wa Algeria. Hawa gumzo lao halikuwa uhuni kama wa wanigeria na wasenegal bali idadi ya waliojitokeza kununua tiketi za mechi yao ilikuwa kufuru. Tiketi za mchezo wao ziliisha mapema sana.

Nilifanya upelelezi binafsi kujua nini kiliwahamasisha kujitokeza kiasi kile nikagundua ni mapenzi waliyonayo kwa timu yao ya taifa. Hata katika mechi za vilabu vyao, waarabu hujaza uwanja kwa kiwango kikubwa bila kuwepo kwa kamati za hamasa.

Ni hapo nilipojifikiria mimi na ndugu zangu watanzania ambao hatuwezi kuingia uwanjani kushangilia timu yetu ya taifa na vilabu vyetu bila ya kuhamasishwa mwezi mmoja kabla. Kumbe zipo sehemu Afrika hii ambayo mashabiki wanaenda uwanjani bila kukumbushwa. Tuna safari ndefu sana kufika huko.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz