Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Nchimbi angecheza timu ya Pep Guardiola

Ditram Nchimbiiii UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Nchimbi angecheza timu ya Pep Guardiola

Thu, 18 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

SOKA linabadilika kila siku. Sio mchezo wa namba tena, ni mchezo wa majukumu, soka limebadilika sana sio mchezo tena wa kumtegemea namba tisa tu kufunga mabao.

Viungo siku hizi wanafunga mabao mengi kuliko washambuliaji, walinzi siku hizi wanafunga mabao mengi sana kuliko washambuliaji. Soka limebadilika.

Makipa siku hizi ndiyo watu wanaoanzisha mashambulizi, ukizubaa, utakuta kipa kapiga pasi nyingi zaidi kuliko hata kiungo. Pep Guardiola ni aina ya kocha ambaye angepewa Ditram Nchimbi angemfanya kuwa mchezaji bora.

Watu wengi wanamtaka Nchimbi afunge mabao wakati yeye mwenyewe tangu aanze kucheza soka hajawahi hata kufika mabao 10 ya Ligi Kuu kwa msimu! Guardiola baada ya kumwona Paul Pogba asingemtumia kama mshambuliaji.

Hakuna namna yoyote ambayo Guardiola asingeamini Nchimbi ni mshambuliaji, kwa kutazama utayari wa mchezaji, nguvu na akili yake ya mpira anaweza kupangwa beki wa pembeni kulia na maisha ya kasonga mbele.

Guardiola ni moja ya makocha wachache duniani wenye uwezo wa kumbadilishia mchezaji majukumu, Philip Lahm alikuwa mlinzi wa Bayern Munich na timu ya Taifa ya Ujerumani kwa miaka yote lakini, chini ya Guardiola alicheza kama kiungo wa chini na mambo yakaenda.

Hakuna mtu aliwahi kufikiria hivyo kabla ya Guardiola, mchezaji aina ya Nchimbi anahitaji kocha kama Guardiola kumpa majukumu mapya uwanjani. Nchimbi bado ni mchezaji kijana, ana uwezo bado wa kucheza nafasi zote za ushambuliaji lakini sio mtu wa kumtegemea kwa mabao.

Hajawahi kuwa mshambuliaji mzuri hata msimu mmoja, nawaheshimu sana makocha wetu hapa nyumbani lakini wote wanaonekana wamekariri matumizi ya Nchimbi, kila mtu anataka amtumie kama mshambuliaji.

Hakuna hata kocha mmoja anayejaribu kumtumia kwenye nafasi nyingine tofauti, hakuna anayeweza kumtumia kama mlinzi wa pembeni kulia, hakuna anayetaka kumtumia kama mchezaji wa kiungo cha chini lakini angecheza chini ya Guardiola mambo yangekuwa rahisi.

Labda Guardiola angembadilishia majukumu, labda angembadilisha namba, Nchimbi angeweza kuwa beki bora kabisa wa pembeni kulia wa Taifa hili.

Pengine angeweza kuwa kiungo wa chini mzuri sana, tatizo makocha wote wamekariri, wote wanamtumia kama mshambuliaji, akicheza mwaka mzima bila bao, nchi nzima inataka kumwangukia.

Nchimbi bado mdogo. Umri unaruhusu, nguvu zipo, kasi ipo, nahitaji tu kocha anayeweza kumpa majukumu mengine uwanjani. Bahati mbaya kwake ni watu kama Guardiola hawapo kila nchi, wamezaliwa wachache sana.

Guardiola alimfanya kiungo Phabian Delph kuwa beki wake na kazi ilifanyika, Ashley Young alikuwa Manchester United kama winga lakini aliishia kucheza kama mlinzi wa kushoto, Antonio Valencia alikuwa Winga machachari sana lakini amemaliza soka na heshima kubwa kama mlinzi wa pembeni kulia.

Makocha wenye jicho hilo kwa kizazi cha leo hapa nyumbani, hawaoni, kubadilishwa nafasi kwa wachezaji hata hapa Tanzania imewahi kutokea lakini sio kwa kizazi hiki cha makocha na kuleta tija kwa Taifa.

Nchimbi ni mchezaji mzuri lakini sio kwenye nafasi ya ushambuliaji, anaweza kuwa Beki Bora kabisa wa pembeni kulia, nadhani anaweza kuwa mlinzi mahiri kabisa.

Kwa kutazama umbo lake, umri wake na nguvu zake nadhani hakuna haja ya kumlazimisha afunge mabao, anahitaji kubadilishiwa tu majukumu na nafasi uwanjani.

Mchezaji wa aina ya Nchimbi ni makosa kutomuona uwanjani, ni kweli hana uwezo mkubwa wa kifunga mabao lakini anaweza kutimiza majukumu mengine uwanjani.

Guardiola asingemuacha nje mchezaji wa aina hii, mtu kama Fernandinho tena ukubwani, ametolewa kuwa mchezaji na kiungo na kuwa beki wa kati.

Hakuna kitu inashindikama kwa Guardiola, Nchimbi angecheza kwenye timu ya Guardiola, angekuwa sehemu ya kikosi chake cha kwanza.

Makocha wetu wanapaswa kumtazama mchezaji huyu kwa jicho lingine tofauti, ni mchezaji mzuri lakini sio kwenye nafasi ya ushambuliaji.

Tunahitaji walau makocha wachache wenye uthubutu wa kubadilisha wachezaji namba, makocha wenye kujitoa muhanga kwa wachezaji wetu.

Hatuwezi kuwa na Guardiola lakini tunaweza kuwa na makocha wanaokwenda sambamba na mahitaji ya kidunia, Nchimbi hajawahi kuwa mshambuliaji bora lakini kwa kutazama umri, umbo, kasi na nguvu anaweza kuja kuwa mchezaji bora kabisa wa Taifa hili lakini kwa nafasi nyingine uwanjani.

Kama nchi hii ingekuwa na kocha aina ya Guardiola, Nchimbi angekuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa kilichomaliza mechi zake za kufuzu Kombe la Dunia hivi karibuni.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz