Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Nani atavaa tena jezi namba 10 ya JPM

Kaliua Pic Data UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Nani atavaa tena jezi namba 10 ya JPM

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KILA Shetani na Mbuyu wake, kila zama na Mfalme wake. Hizi zilikuwa ni zama za JPM na jezi namba 10 mgongoni lakini ndiyo hivyo tena, vizuri havidumu.

Tanzania imempoteza aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya tano, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wiki iliyopita na nchi iko kwenye giza nene, ni huzuni kila kona, ni vilio kila pembe ya nchi. Jezi Namba 10 kwenye mchezo wa soka haivaliwi na kila mtu, inavaliwa na mtu mwenye kitu cha ziada, inavaliwa na mtu mwenye ushawishi zaidi kikosini. Bila shaka yoyote mtu huyo kwenye zama hizi alikuwa ni Hayati Magufuli.

Tanzania ilikuwa inakwenda kutimiza miaka 40 bila kushiriki Afcon lakini chini yake, nchi imeshiriki, halikuwa jambo dogo na wala halikutokea kwa bahati mbaya. Ni mipango madhubuti na kujitoa kwa Watanzania wakiongozwa na Jezi namba 10 mgongoni ya Magufuli. Tangu Taifa la Argentina lilipoipoteza jezi namba 10 ya Diego Armando Maradona, iliwachukuwa muda sana kumpata namba 10 mwingine Lionel Messi.

Tangu Ufaransa impoteze namba 10 wao, Michel Platini iliwachukuwa muda sana kumpata mwingine mpaka walipokuja kina Zinedine Zidane na sasa, Kyllian Mbappe. Kuna kazi kidogo.!

Ni rahisi kuvaa jezi namba 10, lakini kuna ugumu kwenye kutimiza majukumu yake. Wakati mwingine namba 10 hawatengenezwi, namba 10 wanazaliwa tu, sio kila nchi inakuwa na namba 10, wengine jezi hiyo iko Kabatini tu, bado haijapata mtu anayetosha kisawa sawa, bado haina mtu mwenye dhamira ya kuibeba jezi hiyo.

Nchi iko kwenye giza nene, nchi iko kwenye msiba mkubwa, akiwa na jezi namba 10 mgongoni, JPM amekubali sasa michezo iwe somo rasmi na watoto wetu waanze kufundishwa Rasmi.

Ni rahisi sana kupata milioni 70 kwa Mtumishi wa Umma kama pesa ya kustaafu, lakini ni rahisi sana kupata pesa hiyo kwa usajili mmoja tu wa mchezaji wa soka.

Kama tukikipanga vizuri, michezo muda si mrefu inaweza kuja kuwa chanzo kizuri tu cha mapato ya nchi. Majirani zetu Uganda katika maeneo waliyotuzidi, ni msukumo na mipango ya michezo walivyoipa uzito mashuleni. Kuleta wazo la kuifanya michezo kuwa somo ramsi ndiyo maana halisi ya kuwa na jezi namba 10 mgongoni.

Ndiyo maana halisi ya kuwa mchezaji tegemeo zaidi kikosini, unapokuwa Kiongozi tegemeo lazima uwe mtu unayeweza kuona mbele, ni lazima uwe mtu uliyebeba maono. Kwa nchi kama Tanzania ambayo haina akademi za kulea na kukuza vipaji, msingi wake wa kuzalisha wachezaji lazima utoke shule, huko ndiko waliko U-17 wa ukweli, huku ndiko waliko U-20 wa ukweli, umri wa kucheza kwa mazingira ya nchi yetu unapaswa kuwa shuleni, tunahitaji namba 10 mwingine wa kuja kutuvusha katika hili.

Wakati Brazil inampoteza namba 10 wao Pele, wakati Brazil inampoteza namba 10 wao Ronaldinho Gaucho, hakuna aliyejua kama Neymar JR ataibuka. Lakini katika ulimwengu huu, hakuna linaloshindikana. Tutamkumbuka namba 10 wetu JPM kwa kutazama pia maendeleo ya klabu zetu.

Katika kipindi cha Magufuli tumeshuhudia timu zetu zikifanya vizuri Kimataifa, kuruhusu uwekezaji hasa kwenye Klabu kongwe za Simba na Yanga ndiyo msingi wa kuimarika huko.

Katika utawala wa JPM tunashuhudia Simba na Namungo FC wakizidi kuchanja Mbuga Kimataifa, sina shaka na Yanga , watanyanyuka tu. Wananchi hawajawahi kushindwa wakilitaka lao, mpira wa kisasa unahitaji uwekezaji mkubwa na muda wa kutosha, kwa kufungua milango ya uwekezaji, muda si mrefu ufalme wa soka la Afrika unaweza kubisha hodi Tanzania.

Ataivaa nani tena jezi namba 10 ya JPM? Unaweza kunijibu kwa kuniandikia kwenye namba yangu ya simu hapo juu. Francesco Totti, Roberto Baggio, Michael Owen waliwahi kuwa namba 10 wazuri sana duniani lakini wakati ni ukuta. Muda ulipofika walijiweka pembeni. Lakini Mataifa yao yamefanikiwa kupata namba 10 wengine wa kiwango kile? Unaweza kunisaidia majibu. Kila Mfalme na zama zake na hizi zilikuwa zama za JPM.

Tunajua kulikuwa na mpango wa kujenga Uwanja mkubwa wa soka pale Dodoma, bila shaka yoyote nia bado ipo. Tunahitaji kuwa na miundombinu ya kisasa kwenye kila kona ya nchi yetu, tunahitaji kuona michezo inachezwa kwenye kila kona ya nchi yetu.

Nchi imefikwa na Giza nene lakini asubuhi itafika tu, katika kipindi cha JPM, tumeshuhudia timu zetu za vijana zikitamba Kimataifa. Timu yetu chini ya miaka 17 (U-17), kwa mara ya tatu sasa mfululizo imepata nafasi ya kufuzu michuano ya Afrika, hili sio jambo dogo. Huku ndiko msingi wa timu ya Taifa ya baadaye unakojengwa, ni fahari kuona mchezo wa ngumi nao unazidi kuchanja mbuga. Ni fahari kumuona Hassan Mwakinyo akizidi kuwa bondia tishio zaidi kutoka Tanzania. Ni fahari kuona Dullah Mbabe anazidi kuwa Mbabe zaidi. Hizi zilikuwa ni zama za namba 10 mgongoni kutoka kwa Dkt Magufuli. Kila Mfalme za zama zake. Kila mtu na majaaliwa yake. Asante kwa kila kitu JPM, umetuachia jezi namba 10 nzito zaidi kuibeba mgongoni. Pamoja na mambo mengine ya jezi hii, wanamichezo tutamkumbuka JPM kwa uwajibikaji wake na umakini katika kila jambo alilokuwa akilifanya na vilevile alikuwa ni mtu jasiri anayesimamia kile anachokiamini hata kama aliona kwamba kuna baadhi ya watu walikuwa wana wasiwasi kwenye nyuso zao.

Alikuwa ni namba 10 aliyependa kufanya mambo kwa mpangilio na kusisitiza uwajibikaji, yaani kila mtu kwenye nafasi yake awajibike kadri na hata zaidi ya uwezo wake.

Ametuachia funzo kubwa sana kwenye jamii yetu ya wanamichezo kuanzia kwa wachezaji wenyewe, viongozi, wadau na hata mashabiki. Kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa nafasi yake na tuache ujanjaujanja na kutaka njia za mkato kwenye mafanikio ya michezo. Namba alifanikiwa kwavile alikuwa na mipango, tujipange.

IMEANDIKWA NA OSCAR OSCAR

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz