Wakati Wayne Rooney anaifuta rekodi ya Arsenal ya kutokufungwa kwa mwaka mzima alikuwa na umri wa miaka 16 tu. Jisahaulishe kwanza kuhusu bao lake maridadi alilomtungua kipa wa Arsenal na England, David Seaman kwa shuti kali akiwa mita nyingi kutoka golini kwa seaman, kuna kitu kingine kilikuwa kinavutia kuhusu Wayne Rooney aliyekuwa ndani ya jezi ya bluu ya Everton.
Ni ule mwili wake. Katika umri wa miaka 16, mapaja yake yalishajaa vyema na mikono yake ilikuwa mikubwa kama ana miaka 28.
Alikuwa na uso wa kitoto lakini umbile la kiutu uzima.
Kama angepigwa picha akiwa amefunika uso kisha uambiwe useme nani mkubwa kati yake na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa sasa mwenye miaka 25, bado ungemchagua Wayne Rooney wa miaka 16.
Labda mfano wa Rooney ni mbali sana kwa sababu amezaliwa Ulaya. Tujaribu kuwatazama Waafrika. Nimetazama picha za Didier Drogba na yaya Toure wakati wanaingia Ulaya wakiwa vijana wadogo, nilichokiona kimenitisha.
Drogba alikuwa na sura ya kitoto lakini umbo lake lilikuwa kama kijana wa Kitanzania tunayeamini mwili wake umejaa. Akiwa na urefu wake wa wastani bado misuli yake ilijaa vyema. Ni kama ambavyo miguu mirefu ya Yaya Toure ilionekana kama ya mtu mzima akiwa mvulana wa miaka 20 tu. Advertisement
Nimewatazama Waafrika wengi halisi (wasio na asili ya Asia) waliofanikiwa kutamba Ulaya nikaona tofauti katika miili yao. Wengi ama wana miili mikubwa au warefu au wamejaza sana misuli yao.
Ndiyo sababu wengi wao wameishia kucheza mabeki wa kati, viungo wazuiaji au washambuliaji wa mwisho. Wengi wameishia kucheza maeneo yanayohitaji matumizi makubwa ya nguvu.
Wengi hawajatamba sana katika maeneo yanahohitaji ufundi mwingi au kasi kama viungo washambuliaji, mawinga au mabeki wa pembeni. Huu ni ukweli ambao wengi hatukubali kuumeza.
Nimewaza haya baada ya kumtazama Kelvin Pius John akicheza mechi yake ya kwanza ya timu ya wakubwa ya KRC Genk. Akiwa na umri wa miaka 18 Kelvin John anaingia katika kundi la rundo la wachezaji wenye miili midogo tuliowazalisha kwa miaka ya karibuni.
Kwa sasa tunachoweza kufanya ni kusubiri kuona kama Kelvin John atajazia misuli yake. Sidhani kama atarefuka zaidi lakini walau mwili wake utanuke, mapaja na mikono yajae vizuri, kifua kiwe kuikubwa kisha awe na nguvu ili aweze kucheza soka la nguvu.
Kama nilivozungumza awali, historia inaonesha waafrika halisi wengi wanaofanikiwa kutamba Ulaya wanakuwa na miili mikubwa au wanacheza soka la nguvu. Kama wana miili midogo basi wanacheza soka la akili sana.
Hawa ndio kina Sadio Mane na Mohamed Salah lakini bado huwezi kuifananisha misuli ya Salah na watanzania wengi. Sijui ni kinatukwamisha? Sijui ni lishe au asili yetu.
Kinachonipa moyo kwa Kelvin John ni ukweli amefika Ulaya katika umri mdogo. Amekulia katika misingi ya soka na amefanikiwa kupata malezi sahihi anayostahili kupata mchezaji mdogo anayekuwa.
Hata kama mwili wake hautajaa vyema basi bado ana nafasi ya kufanya vizuri kutokana na mafunzo aliyoyapata katika academy za Ulaya. Hata kule katika mashindano ya vijana, alikuwa akifanya vizuri na mwili wake mdogo. Tuamini mafunzo na malezi aliyoyapta kwa watu wanaofahamu soka.
Bila shaka miaka mitano ijayo atakuwa staa wa Tanzania. Yupo wapi mwingine anayeonyesha dalili za kumpiku? Labda Novatus Dismas. Lakini kivyovyote vile Kelvin John kama ataendelea katika njia hii anayopita atakuwa staa mkubwa sana wa Tanzania miaka kadhaa ijayo.
Ni kipindi hicho ambacho presha itakuwa kubwa sana kwake na watanzania watahitaji aibebe timu ya taifa mgongoni. Hawatatazama watu anaocheza nao bali watataka kuona miujiza kutoka kwake kwa sababu anacheza Ulaya kama ambavyo sasa hivi wanataka kuona miujiza kutoka kwa Mbwana Samata.
Ni kipindi hicho ambacho atahukumiwa kwa matokeo mabovu ya timu ya taifa kama yeye ndiye mchezaji pekee wa Tanzania. Hizi lawama zinamsubiri kwa sababu hana wenzake wanaonekana kuelekea katika njia zake.