Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kwanini Azam wamechelewa kumfukuza kocha?

Abdihamid Moallin Azam Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin

Thu, 1 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Sijashangazwa. Nilipomuona mkurugenzi mtendaji wa Azam FC, Yussuf Bakhresa yuko bega kwa bega na timu nilijua tu lazima watu wakae kwa kutulia.

Ukiona Azam FC wanamsajili kipa ambaye aliwahi kucheza Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) unajua kabisa Kocha Abdihamid Moallin maisha yake ndani ya timu yasingekuwa marefu.

Azam wamefanya usajili mkubwa ambao kila wakimtazama kocha Moallin wanamuona hatoshi.

Kuna kosa moja tu ambalo Azam FC wamefanya ni kuchelewa kuachana na Moallin. Ukitazama malengo ya Azam FC na uwekezaji wake unatarajia kumuona pia kocha mwenye uzito huo akiwa kwenye benchi.

Moallin sio kocha mbaya, lakini malengo ya Azam FC yanahitaji kocha mkubwa zaidi yake.

Kosa kubwa ambalo Azam FC wamefanya ni kuchelewa tu kumuondoa Moallin kwenye benchi la ufundi la kikosi cha kwanza.

Azam FC walitakiwa kuachana na kocha wao Moallin mara tu baada ya msimu uliopita kumalizika. Kitendo cha kuendelea kuwa na naye wakati wa dirisha la usajili, kwenda naye nchini Misri kwa maandalizi ya msimu mpya ni kosa kubwa.

Azam walipaswa kumtangaza kocha mpya mara tu baada ya msimu uliopita kwisha ili apate muda wa kusajili wachezaji. Ili apate muda wa kujiandaa.

Sina tatizo na Azam FC kumtimua kocha wao. Tatizo langu ni wao kufanya uamuzi kwa kuchelewa.

Kama Azam FC wana malengo ya kwenda kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Kama malengo ni kwenda walau hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mabadiliko ya benchi la ufundi yalikuwa hayaepukiki. Lilikuwa ni suala la muda tu.

Kama Azam FC wangekuwa na lengo la kutengeneza timu yao bora ya baadaye kwa kutumia wachezaji wao wa ndani, kocha Moallin alipaswa kubaki kwa sababu hilo liko ndani ya uwezo wake.

Lakini kuipa timu ubingwa hayo ni maji marefu. Lakini kuipeleka timu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kina ni kirefu sana kwake.

Kuna gharama kubwa kwenye kumleta kocha katikati ya msimu kwa sababu kila mtu ana mbinu zake na wachezaji wake.

Akija kocha mpya leo, Abdul Sopu na Tepsi Evance wanaweza wasiwe machaguo yake. Anaweza kuja kocha mpya leo akasema yule kipa Mfaransa hana lolote.

Ndiyo gharama za kubadilisha kocha katikati ya msimu. Lazima Azam FC wawe wamejipanga kwenye hilo. Taratibu wanaanza wenyewe kujitoa kwenye reli. Taratibu wanaanza wenye kujiangusha.

Mechi yao inayofuata ni dhidi ya Yanga, timu ambayo haijafungwa kwenye ligi tangu mwaka jana.

Taratibu Azam FC wanaanza kujikaanga wenyewe. Wamechelewa sana kumfukuza kocha. Uamuzi kama huu ulipaswa kufanyika mapema sana baada tu kuona pilikapilika za usajili wa wachezaji. Baada tu ya kuona mbio za kuleta Wazungu kama wasaidizi wa kocha mkuu, nilijua kabisa kocha mkuu hachomoki.

Azam FC hawana matokeo mabaya kwenye mwanzo wa Ligi Kuu msimu huu. Huenda kocha ameondolewa kwa sababu tu ya malengo ya klabu. Malengo ni makubwa kuliko uwezo na uzoefu wa kocha.

Ukiniuliza unaiona wapi Azam FC msimu huu? Hata mimi sina majibu. Ukiniuliza kama wana uwezo wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, sina majibu.

Ni kama wameanza kujiangusha wenyewe kabla hata ya kwenda kushindana na wapinzani wao uwanjani.

Ukiwatazama Simba SC na Yanga SC unawaonea tu huruma Azam FC. Ni uamuzi mzuri wa kuachana na Moallin, lakini umefanywa kwa kuchelewa.

Hakuna muujiza wowote ambao Moallin angeweza kuwapa Azam FC. Kumpeleka kwenye timu za vijana ni uamuzi mzuri sana kwa pande zote mbili.

Ni kocha anayehitaji muda wa kukua na kujitafuta. Malengo na uwekezaji wa Azam FC ni mkubwa kuliko yeye.

Sina tatizo na yeye kutimuliwa nashangaa amewezaje kukaa muda wote huo mpaka kushiriki mechi mbili za Ligi Kuu msimu huu.

Kazi ya kwenda hatua za makundi Kombe la Shirikisho Afrika inahitaji wanaume haswa na sio wavulana.

Shughuli ya kuutafuta ubingwa mbele ya Simba na Yanga haitaki kocha wa majaribio. Ni vita kwelikweli inahitaji kocha wa mapambano.

Moallin alikuja vizuri mwanzo alipotua Azam FC, lakini ni hakika alipaswa kubakia katika timu za vijana kulekule.

Azam FC ni miongoni mwa timu kubwa hapa nchini na inapaswa kuonyesha msuli unaofanana na ukubwa wake mbele ya wakubwa wenzake - Simba na Yanga.

Moallin sio kocha mbaya lakini malengo na uwekezaji wa Azam FC ni mkubwa sana kuliko yeye.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz