Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kuna ulazima wa timu zetu kwenda nje?

Simba Misri 7 Kikosi cha Simba kipo nchini Misri kikijiandaa kwa msimu mpya 2022/2023

Thu, 21 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

NI kawaida sana kipindi kama hiki cha maandalizi ya msimu mpya kuwaona Liverpool na FC Barcelona wakiwa nchini Marekani.

Ni kawaida muda kama huu kuwaona Manchester United wakiwa barani Asia wakicheza mechi za kirafiki. Timu hizi ni za watu ambao kipindi kama hiki wanajitanua dunia nzima kwenye kutafuta masoko. Hawa ni watu ambao kila kona ya dunia imejaa mashabiki wao. Kumekuwa na tabia pia kwa timu zetu za Simba na Yanga kwenda nje ya nchi kujiandaa. Sidhani kama ni jambo baya, lakini mashabiki wa timu hizi zaidi ya asilimia 90 wako Tanzania.

Unadhani kuna ulazima kwa timu zetu kwenda nje ya nchi kufanya maandalizi ya msimu mpya? Nitumie maoni yako kwa kutuma ujumbe mfupi kuipitia namba yangu ya simu hapo juu. Nawaelewa sana Chelsea wakienda Marekani kujiandaa na msimu mpya. Naelewa sana Real Madrid wakifanya hivyo. Hizi ni Klabu zenye mashabiki kila kona ya dunia. Kipindi kama hiki wanakitumia kusogea karibu na mashabiki wao.

Kipindi kama hiki wenzetu wanakitumia kibiashara zaidi. Sio kipindi cha kuandaa timu kimbinu. Sio kipindi cha kutengeneza muunganiko wa timu ni kutafuta mashabiki kila kona ya dunia. Kumekuwa na habari kwamba Yanga walitaka kwenda Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya. Tayari Wekundu wa Msimbazi, Simba wako Misri. Ukiniuliza kama Yanga ina masha biki Uturuki jibu langu ni hapana.

Ukiniuliza kama Simba ina shabiki hata mmoja nchini Misri, jibu langu ni hapana. Kwa nini timu zetu bado zinaendelea kwenda nje ya nchi kipindi kama hiki cha maandalizi ya msimu mpya? Sina jibu la moja kwa moja. Labda kwenda nje ya nchi kwetu ni ufahari. Labda kwetu mchakato wa kibiashara sio muhimu sana. Simba na Yanga kama wanataka kukua kibiashara Tanzania ni eneo lao zuri sana la kuweka kambi. Wanaweza kutengeneza mikoa yao kama 10 hivi kila m-si-mu ya ku-ite-mbelea kibiashara.

Wanaweza kwenda kucheza kwenye kila mkoa mechi moja ya kirafiki na hasa kwenye mikoa ambayo ina watu wengi nchini na ile ambayo haina kabisa timu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Fikiria kama Simba wangeamua kubaki hapahapa nchini huku wakitembelea mikoa kama Kigoma, Tabora, Singida, Shinyanga. Wangepiga pesa kiasi gani? Wangeuza jezi kiasi gani? Usinipe Jibu.

Fikiria kama Yanga wangeamua kufanya kambi yao hapa kwa kuipeleka timu mikoa kama Iringa, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Manyara. Wangepiga pesa kiasi gani? Wangeuza jezi kiasi gani? Usinipe jibu. Wenzetu kipindi kama hiki ni muda kwao wa kukuza biashara. Wenzetu muda kama huu wanautumia zaidi kusogea karibu na mashabiki zao, sio kipindi tu cha kuandaa mbinu timu ni biashara zaidi.

Simba na Yanga kibiashara wanaweza hata kutengeneza ziara ya maandalizi ya msimu kwenye ukanda wetu wa Cecafa. Ukipata mechi dhidi ya bingwa wa Rwanda pale Kigali, ukienda Uganda pale Kampala kucheza na bingwa wa msimu huu, ukaenda pale Kenya kucheza na bingwa wa msimu huu kibiashara utakuwa umeanza kuiteka Afrika Mashariki. Uzuri nchi zote za Cecafa pia zinaongea Kiswahili. Uzuri wa nchi za Cecafa zina wachezaji wanaocheza Simba na Yanga. Kuna umuhimu wa timu zetu kwenda Misri na Uturuki? Naomba maoni yako kwa kujiandikia ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Ukipata mtaalamu wa maandalizi ya timu akakupangia vizuri safari ya Simba kwenda nchi tano za ukanda wa Cecafa utafurahi. Ukipata mtaalamu wa masoko akakupangia vizuri mchoro wa kwenda kucheza hizo mechi tano za ugenini kibiashara klabu zetu zingekuwa mbali sana.

Wenzetu hawasafiri tu kwenda kupata sifa. Wenzetu hawaendi tu Marekani na Asia kuuza sura wanakwenda kutengeneza masoko. Wanakwenda kufanya biashara.

Ukiipeleka Yanga Uturuki haiendi kufanya biashara yoyote. Ukiipeleka Simba Misri haiendi kufanya biashara yoyote. Ni bora kuandaa ziara za ndani. Ni bora kuandaa ziara za ukanda wetu wa Afrika Mashariki.

Huu ni wakati wa kutafuta masoko, lakini kutengeneza utimamu wa miili wa wachezaji. Jukumu la kuulinda mwili wa mchezaji ni la mchezaji mwenyewe. Ndiyo maana hata ukiona mechi za maandalizi ya msimu utaona Manchester United kipindi cha pili wanaweka watoto wadogo tu wa akademi. Huu sio muda wa kutafuta pointi tatu. Ni muda wa biashara na masoko. Soko la Simba na Yanga haliko Uturuki wala Misri. Liko hapahapa kwa Mama Samia Suluhu Hassan. Liko hapa hapa kwenye ukanda wa Cecafa.

Timu zetu zinahitaji watu wa kuangalia zaidi masoko na biashara kipindi kama hiki. Hata wachezaji wapya walipaswa kutambulishwa kwenye jezi mpya za msimu na sio jezi za msimu uliopita. Tunahitaji kusonga mbele.

Columnist: Mwanaspoti