Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kuna tatizo makocha wakisajili wachezaji?

Maki Bocco Zoran UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kuna tatizo makocha wakisajili wachezaji?

Fri, 26 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Timu nyingi zinazofanya vizuri hapa nyumbani mara nyingi huwa zimesajiliwa na viongozi. Tatizo la kwanza linaanzia hapa. Tatizo namba mbili litakuja baadaye. Inasemekana ndani ya Klabu ya Simba wachezaji wengi sio chagua la kocha Zoran Maki na anataka kuwaondoa.

Hakuna timu hata moja duniani ambayo usajili wake kwa asilimia l00 ni uamuzi wa kocha. Hakuna. Upo usajili wa kocha na upo wa klabu.

Pale Real Madrid usajili kama wa kina James Rodriguez, Gareth Bale na Eden Hazard haukuwa wa kocha. Ni usajili wa klabu. Pale Manchester United wakati anarudi Cristiano Ronaldo haukuwa usajili wa kocha ni usajili wa klabu. Ndiyo maisha ya mpira yalivyo.

Ninaposikia tetesi kocha wa Simba hawataki sehemu kubwa ya wachezaji Simba aliowakuta nabaki kucheka.

Timu kubwa karibu zote suala la usajili wa wachezaji hazijawahi kumuachia kocha kwa asilimia 100. Kuna muda klabu inaingilia. Kuna muda viongozi wanalinda maslahi ya klabu. Kocha bora siku zote ni yule anayetengeneza mbinu za kumpa matokeo mazuri kwa kutumia wachezaji waliopo.

Kocha Maki ana mkataba na Simba wa mwaka mmoja. Ukimpa uhuru wa kusajili kikosi chake mwakani tu utalazimika kutimua kikosi chote.

Kocha Marcio Maximo aliwahi kuja Yanga na wachezaji wake ndiyo wale kina Jaja. Hakukua na Jambo kubwa sana waliloleta kutoka Brazil. Walikuwa ni Wabrazili ambao hawana tofauti kubwa sana na Waluguru wa Morogoro. Ubora wa kikosi cha Yanga unaouona leo kwa sehemu kubwa viongozi wamesaidia kwenye kusajili kikosi chao. Ni kweli kocha Nasreddine Nabi yupo, lakini ukimpa jukumu kusajili wachezaji hatakupa timu bora kirahisi. Anaweza akachemka vibaya.

Hizi tetesi kuwa kocha Maki anataka kutengeneza timu yake mwenyewe Simba itakuwa ngumu. Hakuna timu inayotoa uhuru wa makocha kuuza na kusajili wachezaji kwa asilimia 100.

Wapo wachezaji watasajiliwa na kocha, ila wapo pia ambao wanasajiliwa kwa manufaa ya taasisi. Maki apige kazi.

Pale Msimbazi kuna wachezaji wengi wa kumpa ushindi. Kocha anaweza kupendekeza sifa za mchezaji anayemtaka na viongozi wakamletea. Hii haina shida hata kidogo, lakini kutaka wachezaji zaidi ya sita kuondoka sidhani kama klabu itamruhusu.

Kuna kashfa ya makocha kupenda kupata asilimia 10 kwenye usajili wa wachezaji wanaowataka wao. Hii kashfa ni ngumu kuithibitisha, lakini inatajwa kila siku. Ukiona kuna jambo kila siku linazungumzwa linakupa hisia za kuwepo.

Inaelezwa kuwa kocha Maki hamtaki John Bocco, Victor Akpan na Nassoro Kapama . Hakuna ubaya kwake kutaka wachezaji watakaoendana na mfumo wake, lakini klabu pia lazima ilinde maslahi yake. Ni kweli Bocco hana uwezo tena wa kuisaidia Simba? Nipe maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Baada ya kizazi cha dhahabu cha hivi karibuni cha kina Luis Miquessone, Clatous Chama, Bocco na Erasto Nyoni taratibu kuelekea ukingoni, Simba wanajaribu kutengeneza kingine ambacho kije kuwa kikali zaidi. Utengenezaji ya kizazi kipya kwenye soka sio jambo la kitoto. Twende polepole mzee Maki. Utengenezaji wa Simba bora hautaki haraka. Sio kazi ya siku moja.

Kocha anaweza kupendekeza wachezaji lakini hawezi kuamua kila kitu kwenye usajili. Wachezaji ni mali ya klabu. Ni mali ya taasisi. Watu wengi wanadhani kuwa makocha wote duniani hupewa jukumu la kusafisha kijiji kama anavyotaka kocha Simba. Ni kweli atakuwa anapewa nafasi ya kusajili, lakini sio timu nzima. Maki ana mchanganyiko mzuri sana wa wachezaji. Kama atafanikwia kupata walau kikosi chake cha kwanza atakuwa mtamu sana msimu huu. Wale kina Peter Banda, Okrah na Sakho kuna siku watawafanya watu maji waite “mma”. Ni vijana wenye uwezo mkubwa sana. Hawa kina Bocco sio kwamba ni watu wabaya sana isipokuwa itabidi wakomae.

Kocha Maki amecheza mechi mbili tu Ligi Kuu tayari tetesi zinasema anataka kupasafisha Simba. Hapana. Twende polepole. Hata pale Yanga kocha hawezi kupewa uhuru wa asilimia 100 kwenye usajili. Hata pale Azam FC huwezi kumpa kocha nafasi ya kufanya hizo timua timua za wachezaji. Kocha ndiye mkuu wa benchi la ufundi na anapaswa kusikilizwa, lakini kwenye mpira hawezi kufanya kila kitu mwenyewe. Huyu kocha Maki asipopata watu wa kumbana kidogo atakuja kusema hamtaki hadi Chama.

Columnist: Mwanaspoti