Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kocha wa Yanga atapona kweli msimu ujao?

Kaze Nabi Makocha wa Yanga, Kaze na Nabi

Thu, 14 Jul 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hakuna nchi inajua kuwapamba watu wake wa mpira Afrika kama Tanzania. Mtunisia Nasreddine Nabi kwa sasa anaitwa profesa. Alisomea wapi? Sina majibu. Ukitazama pale katikati ya dimba kuna kiungo Mganda Khalid Aucho, lakini kwa sasa anaitwa daktari. Alisomea wapi? Sina majibu. Ndiyo mpira wetu. Ndiyo timu zetu.

Moja kati ya timu zilizosajili vizuri kuelekea msimu ujao ni Yanga. Karibu kila nafasi iliyokuwa na changamoto msimu uliopita, imepatiwa majibu. Kulikuwa na changamoto kwenye idara ya ulinzi kushoto amekuja Joyce Lomalisa.

Huyu ni mwanaume haswa, amecheza michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2017). Amecheza mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) 2016.

Kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza timu ya taifa la DR Congo sio shughuli ya kitoto. Huu ni usajili unaovutia sana kwa mashabiki, lakini ni kaa la moto kwa mtu kama Profesa Nabi.

Kuna kazi kubwa sana kwa kocha wa Yanga kupona msimu ujao. Matarajio ya Wananchi ni makubwa sana pengine kuliko hata uhalisia. Profesa Nabi anapaswa kukumbuka hilo kwenye kila mechi anayocheza. Wananchi hawana subira.

Msimu 2022/23 kila shabiki wa Yanga atageuka kuwa Kocha. Kila shabiki wa Yanga ataona kama timu yao haistahili kufungwa.

Kulikuwa na changamoto ya Kiungo, tayari ameshushwa Geal Bigirimana mwenye CV ya kucheza soka nchini England. Hili ni deni lingine kwa Profesa Nabi.

Mtazamo wa Wananchi ni kuona timu inaupiga mwingi, matarajio ya Wananchi ni kuona burudani na ushindi vyote vinakuja kwa wakati mmoja.

Sio kazi rahisi kwenye mpira lakini Nabi inabidi aifanye. Kuna tofauti kubwa sana kati ya kusajili wachezaji wazuri na kutengeneza timu nzuri. Wakati mwingine kuwa na timu bora huchukua muda.

Wakati mwingine muunganiko wa timu unahitaji watu waliokaa pamoja muda mrefu. Wananchi wako tayari kuvumilia? Sina majibu. Nikiwaangalia sura zao, wanawaza ushindi tu. Kila ninapowatazama naona wanawaza na wao robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kuna kazi kubwa sana kwa Profesa Nabi. Wananchi wana matarajio makubwa sana kwa timu yao pengine kuliko hata anavyodhani. Ushindi uwanjani hauji kwa sababu tu mmesajili wachezaji wazuri. Kuna mambo mengi sana kwenye soka lakini sidhani kama wananchi watamuelewa Nabi asipowapa furaha.

Kila mtu atapanga kikosi chake, kila mtu atafanya mabadiliko yake. Ni rahisi sana kusikia kuwa timu imekuwa kubwa kuliko uwezo kocha.

Ni rahisi sana kusikia Profesa Nabi anatuchelewesha. Ndiyo mpira wetu ulivyo, ndiyo matarajio ya Wananchi.

Ukiniuliza kama Kocha wa Yanga atapona kweli msimu ujao? Sina Majibu. Kwa namna ninavyowajua Wananchi, sio tu watataka ushindi lakini watataka pia kuiona timu yao ikicheza vizuri.

Watataka kuona unapigwa mpira mwingi uwanjani, haiwezi kuwa shughuli ndogo, ule umati ulijitokeza kwenye Paredi la Ubingwa ndiyo utaojitokeza kila mechi ya Yanga kwa Mkapa.

Hebu fikiria wale watu waje kushuhudia timu yao inafungwa. Fikiria wale watu waje kuona timu inacheza mpira mbovu, fikiria wale watu wanakuja kuona timu yao inaondolewa Kimataifa hatua ya awali!

Kuna kazi kubwa sana kwa Profesa Nabi. Huu ndiyo msimu wakujua kama kweli Nabi ni profesa wa kweli au wa mchongo.

Baada ya Simba kutengeneza heshima kwenye michuano ya kimataifa, wananchi hawana shughuli ndogo. Wanaiona Yanga huko.

Wanatamani kuona Yanga akifika mbali zaidi ya Simba kimataifa. Kwenye mpira sio jambo rahisi lakini linawezekana. Ni lini? Sina majibu.

Simba hawafiki robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bahati mbaya. Wamekamilika ndani na nje ya uwanja. Simba wamekuwa na timu dume hasa kwenye mapambano ya Afrika.

Haikutengenezwa kwa siku moja. Yanga wako tayari kumvumilia Profesa Nabi? Sina uhakika.

Kuna kazi kubwa sana kwa Profesa Nabi kwanza kwenye kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu na FA. Azam FC wamefanya usajili mzuri sana kuelekea msimu ujao. Hawatakuwa wepesi.

Kama watapata kipa mzuri, watasumbua sana. Simba siku zote atabaki kuwa Simba tu. Wanajua namna ya kushindana. Wamesajili watu ambao hawana mafanikio makubwa huko walikotoka, wanataka kuja kufanikiwa wakiwa Simba. Watu wenye ndoto kubwa. Watu wanaotaka na wao waonekane.

Simba ni Simba tu, watasumbua sana. Wananchi wanataka kuiona timu yao walau hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika. Kama timu itatolewa tena hatua za awali kama ilivyokuwa msimu uliopita, maisha ya Profesa Nabi yatakuwa magumu sana Jangwani. Yanga wamefanya usajili mzuri, mashabiki wa Yanga bahati mbaya sio wavumilivu sana. Usajili unavutia lakini unaweza kumuondoa Profesa Nabi mapema kuliko vile watu wengi wanavyodhani.

Kila la heri Nabi, una kazi kubwa sana msimu ujao kuliko kazi kubwa uliofanya msimu huu. Wananchi sio wavumilivu. Wananchi wana matarajio makubwa kwako.

Columnist: Mwanaspoti