Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kipi kiliwaangusha Simba mechi ya mtani?

Azizi Ki Kipi kiliwaangusha Simba mechi ya mtani?

Thu, 18 Aug 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kama kulikuwa na kitu kigumu kwa Waandishi wa habari za michezo na wachambuzi kutabiri kwenye mechi ya Simba na Yanga, basi ni kumjua mshindi. Mechi ya watani ilikuwa haieleweki kabisa.

Mara nyingi sana timu isiyopewa nafasi kubwa kwenye mechi ya watani, ilikuwa inashinda. Siku za hivi karibuni, Simba ameanza kuwa mteja kwa Yanga.

Dabi ya Kariakoo sasa imeanza kutabirika. Taratibu Yanga imeanza kuwa mfalme wa derby hii. Ukitazama mechi nane za mwisho, utagundua Yanga ameshinda mechi nne, Simba moja na mechi tatu zimemalizika kwa Sare. Siku hizi ni rahisi sana kujua Yanga anakwenda kushinda.

Kipi kinawaangusha Simba kwenye mechi za mtani? Sina majibu. Kama una maoni yoyote usisite kuniandikia ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Wikendi iliyopita nimeshuhudia Simba akifungwa tena na mtani kwa Mkapa! Wikiendi iliyopita nimeshuhudia Simba akinyanyaswa tena na Yanga. Ni kama ameanza kuwa kibonde sasa kwa mtani. Ni kama anaifanya sasa dabi ya Kariakoo kuanza kutabirika.

Unadhani ni kwa nini Kocha Zoran Maki alimtoa Cloatus Chota Chama dakika ya 60? Mimi bado sina Jibu. Kimsingi Chama ndiyo alikuwa mchezaji hatari zaidi kwenye eneo la kushambulia. Ndiye mchezaji ambaye mpira ukiwa kwenye miguu yake, Yanga wanaingia presha.

Namna alivyokuwa anapiga pasi zake za mwisho nadhani alipaswa kuendelea kusalia uwanjani. Baada ya kutolewa kazi ya walinzi wa Yanga ilikuwa rahisi sana. Hakukuwa tena na mtu hatari uwanjani. Yanga walitawala karibu kila kitu kipindi cha pili.

Kipi kinawaangusha Simba kwenye mechi za Mtani? Sina majibu. Ukirudi nyuma kipindi cha kwanza, utawaona Simba wakiwa huru sana. Wakitawala mchezo. Wakifunga bao pia la mapema lakini mechi inakwisha kwa kichapo.

Kama Simba wangekuwa na watu bora sana kwenye eneo la kushambulia, wangeweza kuimaliza mechi kipindi cha kwanza.

Wangeweza kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza 3-0. Kila kitu kilikuwa upande wao.

Mabadiliko aliyofanya kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ndiyo yaliyopeleka msiba Msimbazi. Baada ya kumtoa Farid Mussa na Sure Boy, moto wa Bernard Morrison na Jesus Moloko uliwatoa Simba mchezoni. Azizi KI anaonekana balaa sana kama atacheza nyuma ya mshambuliaji. Kumtumia pembeni ni kumpotezea muda tu. Alikuja nyuma ya Mayele na kufanya kila kitu kuwa rahisi. Ndiye mchezaji aliyekuwa na akili kama Chama kwa upande wa Yanga. Ndiye mchezaji aliyefanya dabi kuwa nyepesi. Simba anafungwa kwa mara ya nne Mtani ndani ya mechi nane za mwisho, sio jambo la kawaida.

Nilikuwa nautazama ukuta wa Simba, namwona Mohamed Ouattara na Henoc Inonga wote kama mabosi pale nyuma. Hakuna anayetaka kumtuma mwenzie. Wote wanaonekana wanacheza kwenye staili moja. Nadhani Joash Onyango bado anahitaji sana kuleta utofauti. Ouattara na Inonga, mmoja kwenye mechi dume itabidi aanzie benchi. Unahitaji mtu Mbadi, Onyango ndani ya kikosi kuleta utofauti.

Nimtazama Dejan Georgijevic, pamoja na utani mwingi lakini jamaa anajua boli. Ni Mzungu ambaye kama atapewa muda na nafasi, atakuja kuwafanya watu kitu kibaya.

Natamani kumwona akiwa sehemu ya kikosi cha kwanza akicheza juu ya Chama. Ni Mzungu mwenye mikimbio mizuri. Ni Mzungu anayejua namna bora ya kujiweka kwenye nafasi. Kipi kinawaangusha Simba za Mtani? Naomba maoni yako kwa ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Natarajia kuona mabadiliko makubwa sana ya kiuchezaji kwa Simba kwenye mechi za ligi.

Inaonekana wamesajili wachezaji wazuri lakini bado wanahitaji muda kidogo kukaa sawa. Pamoja na kujitaji muda, wanatakiwa pia kushinda. Ukiruhusu kuachwa pointi nyingi mapema ni kazi sana kuzirudisha mzunguko wa pili. Ligi ya msimu huu, sio ya timu mbili tena. Kuna farasi wengine wameongezeka. Wale Azam FC ni moto. Wale Singida Big Stars nao ni balaa. Wakati Zoran anatengeneza Muunganiko mzuri wa timu yake ni lazima awe anashinda pia mechi zake.

Ukiniuliza kwa sasa kama dabi ya Kariakoo haitabiriki, nitakataa. Mechi za watu za siku hizi zinatabirika. Yanga amekuwa Mfalme mpya wa dabi hii. Simba amekuwa mnyonge sana. Kuna kitu kinatakiwa kuwekwa sawa. Mnyama amekuwa Mteja mno wa mechi za Watani wa Jadi.

Kipi kinawaangusha Simba kwenye mechi za Mtani? Naomba nitumie maoni yako kwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Columnist: Mwanaspoti