Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kila bao la Yanga lilikuwa muhimu

Kennedy Musonda CAF Kila bao la Yanga lilikuwa muhimu

Thu, 23 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga wakamaliza wikiendi wakiwa na furaha kuliko watu wote duniani. Ni baada ya kuwachapa TP Mazembe katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika Jumapili.

Siku moja nyuma, walikuwa na sherehe nyingine. Wababe na watani zao wa Kariakoo walikuwa ‘wamelowa’ mbele ya waarabu wa Morocco, Raja Casablanca.

Hakuna furaha kubwa kwa shabiki wa Yanga inayozidi ile ya timu yake kushinda halafu Simba wapoteze tena ndani ya saa 24.

Kinyume cha kauli hii ni sawa pia kwa shabiki wa Simba. Tuna msemo wetu maarufu wa ‘Soka letu kivyetuvyetu’.

Mabao matatu waliyofunga Yanga yalikuwa muhimu kuhakikisha wanapata ushindi wa kwanza wa uhakika nyumbani.

Ushindi ambao utawajengea ujasiri katika mechi mbili za nyumbani zilizosalia.

Kama wamemfunga kigogo kama Mazembe, kwa nini wawashindwe wengine? Itakuwa rahisi hata kwa viongozi wao kuhamasisha mashabiki katika mchezo ujao dhidi ya Real Bamoko.

Ingekuwa ngumu kidogo kwa viongozi kufanya hamasa kama wasingepata matokeo mazuri Jumapili. Ni kama ambavyo Simba watapata ugumu kufanya hamasa katika mchezo wao wa nyumbani wa ligi ya mabingwa unaofuata dhidi ya Vipers.

Si tu ujasiri na urahisi wa kufanya hamasa lakini pia ni ushindi wa kuwafunga midomo watani zao Simba. Kwa muda mrefu, Simba wamekuwa wakitamba juu ya umahiri wao wa kutumia dimba la Mkapa na kuwabeza Yanga huwa hawafanyi vizuri nyumbani.

Sasa Yanga wanaweza kuongea kushinda nyumbani si kitu cha ajabu sana, ukizingatia pia walipata ushindi muhimu ugenini dhidi ya Club Africain kule Tunisia.

Ni kama ambavyo Yanga watapata cha kujitetea baada ya mshambuliaji wao mpya Kenedy Musonda kupachika bao la kwanza katika ushindi wao wa Jumapili. Musonda, ambaye kwa mtazamo wangu alikuwa katika eneo la kuotea alipachika mpira katika wavu mtupu akimalizia mpira mzuri wa adhabu wa Shaban Djuma.

Tangu acheze mchezo wake wa kwanza akiwa na jezi ya Yanga, Musonda amekosolewa sana kwa kutokufunga. Simba walianza kuwatania Yanga wamepigwa na taratibu Yanga walianza kuogopa labda ni kweli wamepigwa. Bao lake na pasi nzuri aliyoipeleka kwa Mudhathir Yahya aliyefunga bao la pili ni kielelezo Musonda ni mchezaji mzuri anayeingia taratibu katika mfumo.

Bao la pili lililofungwa na mchezaji mwingine mpya wa Yanga nalo lilikuwa na umuhimu wake. Kwanza katika mchezo, liliwapa Yanga utulivu kwa kuwa walitanua wigo wa mabao hivyo kujiamini kuliongezeka zaidi.

Cha pili ni jinsi ambavyo Mudhathir alicheza kwa umaridadi mkubwa sana katika eneo la kiungo mshambuliaji. Kwa miaka mingi akiwa na jezi ya Azam FC pamoja na ile ya timu ya Taifa, tulimzoea Mudathir akicheza kama kiungo wa ulinzi au kiungo wa kati.

Hatukumzoea katika eneo la kiungo mshambuliaji mpaka tulipomwona juzi.

Kumbe miaka yote Azam waliteseka kumtafuta namba 10 wakati walikuwa na Mudathir Yahya? Japo bado ni mapema sana lakini kumbuka Feisali Salum ‘Fei Toto’ alianza kuchezeshwa namba 10 na Nabi kama masikhara.

Leo Fei Toto kila mtu anamtamani katika timu yake acheze namba 10. Hilo moja, pili lile bao lilikuwa ujumbe kwa Feisal Toto, kumbe Yanga wanaweza kumtengeneza namba 10 mwingine na akafanya vyema bila uwepo wake.

Bao la mwisho la Tuisila Kisinda nalo lilikuwa na majibu yake. Kwanza liliwahakikishia Yanga ushindi na alama tatu muhimu za nyumbani.

Kumbuka Mazembe walikuwa wanahitaji bao la kusawazisha na roho za Yanga zilikuwa mkononi. Tuisila alihakikisha mechi inaisha salama kwa upande wa Yanga. Pia, alifanya kitu ambacho Nabi anahitaji akifanye siku zote. Kasi yake inahitajika katika mashambulizi ya kushtukiza kama yale.

Kilichovutia zaidi ni ule umaliziaji wake. Kama kulikuwa na mgeni uwanja wa taifa siku ile, asingeamini huyu ndiye mshambuliaji anayetukwana na Yanga siku zote.

Baada ya lile bao Yanga watakuwa wamemsamehe na watasahau mpaka atakaporejea katika maudhi yake. Kwa sasa Tuisila anaweza kupumzika salama baada ya muda mrefu.

Mabao matatu ya Yanga yalikuwa muhimu kila moja kwa kona yake.

Columnist: Mwanaspoti