Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kiiza 'Diego' niliyemuona Taifa zamani na Kaitaba juzi

Kiixza Diego Kiiza 'Diego' niliyemuona Taifa zamani na Kaitaba juzi

Thu, 10 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takribani miaka 11 iliyopita, nilikuwa juu ya kiti katikati ya mashabiki wastaarabu wa jukwaa kuu Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Mkapa) nikitazama mechi ya kirafiki kati ya Yanga na URA ya Uganda.

Licha ya kwamba ulikuwa ni mchezo wa kirafiki, mchezaji aliyeongoza safu ya ushambuliaji ya URA hakuwa na urafiki na mtu yoyote.

Baada ya kumtazama kwa muda mrefu, baadae nilifanikiwa kulifahamu jina lake kupitia kwa mwandishi mmoja wa Uganda.

Aliniambia anaitwa Hamis Kiiza ‘Diego’.

Kiiza alimkosha kila mtu aliyekuwa ameketi jukwaa kuu siku ile. Alikuwa na maarifa mengi na kasi ya ajabu. Angeweza kwenda winga ya kushoto kuchukua mpira kisha angemtambuka beki na kulikimbilia sanduku la Yanga kama hana akili timamu.

Angetisha kama anatoa pasi kisha angepiga shuti kali, alikuwa hatari kuliko hatari yenyewe. Baada ya dakika kama 70 uwanjani, kocha wa URA alimpumzisha na kumuingiza mchezaji mwingine.

Huo ulikuwa mwanzo wa macho yangu kumshuhudia Kiiza na kumkubali ndani ya dakika sabini tu nilizomshuhudia akiiteketeza Yanga.

Dirisha la usajili lililofuata sikushangaa kuwaona Yanga wakimalizana na klabu yake na kumshusha jangwani.

Hawakuhitaji kujiuliza juu ya uwezo wake wakizingatia mateso aliyowapa mabeki wao zile dakika sabini jioni ile pale kwa Mkapa. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kumshuhudia Nadir Haroub akimkimbia mshambuliaji.

Yanga hawakukosea kwa Hamis Kiiza. Yale makali alioyaonyesha dhidi yao pale Lupaso aliyahamishia kwa timu zingine za ligi kuu. Kiiza aliiiongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga kwa miaka minne. Alikuwa mshambuliaji hatari aliyewahakikishia mabao kila msimu.

Haikunishtua nilipoona ‘wikipedia’ wakisema Kiiza amefunga mabao 56 katika mechi 80 alizovaa uzi wa Yanga. Ni wastani wa bao moja kwa kila mechi mbili.

Kiiza wa miaka ile asingeshindwa kufanya hivyo.

Baadae Yanga walimsajili Amis Tambwe aliyetemwa na Simba. Yanga wakaamua kulichinja jina la Hamis Kiiza siku ya kufunga dirisha la usajili kwa kigezo cha utovu wa nidhamu. Inadaiwa Kiiza hakuwa anapatana na Kocha Mbrazil, Marcio Maximo. Kiiza akarudi nyumbani Uganda kupumzika. Simba hawakupoteza muda, walienda Uganda na kumrudisha Kiiza nchini.

Simba walimsajili Kiiza kwa sababu mbili, kwanza walikosea kumwacha Tambwe na hawakuwa na mshambuliaji wa kati anayewapa mabao ya uhakika. Pili ni kwa sababu kipindi akiwa Yanga Kiiza alikuwa anawafunga sana.

Hii sababu ya pili ilimpa nguvu zaidi, Kiiza hakuikuta Simba imara sana lakini bado alifanikiwa kupiga mabao mengi kama alivyokuwa Yanga. Kwa mujibu wa Wikipedia tena wanadai Kiiza alifunga mabao 24 katika mechi 30 za Simba.

Kwa uwezo aliokuwa nao Kiiza miaka ile sina shaka na takwimu hizo. Kiiza aliondoka nchini na kuzurura klabu kadhaa kabla ya kurejea tena majuzi.

Mechi yake ya pili tu aliwalaza waajiri wake wa zamani na viatu.

Simba wakaondoka Kaitaba vichwa chini kwa bao la Kiiza, Kilichonishtua ni kumwona Kiiza anacheza kwa ubora mkubwa sawa na vijana wadogo baada ya miaka mingi kupita.

Kwa mujibu wa Wikipedia, Kiiza ana miaka 31, nilipoona takwimu za mabao ya Kiiza sikubisha lakini kwenye umri nilipata wasiwasi kidogo. Kama Kiiza hatari sana nilimwona miaka 11 iliyopita, ina maana miaka ile alikuwa na miaka 20 tu. Ni kweli Kiiza alikuwa na ukomavu ule akiwa na miaka 20 tu? Hapana! Lazima ni mwendelezo wa maisha ya wachezaji wa kiafrika na umri. Licha ya hivyo bado tunaweza kumuona Kiiza akicheza kwa ubora mkubwa kama tulivomwona katika mechi zake mbili za kwanza kwa sababu ya ushindani wa ligi yetu.

Tunapaswa kuumia moyo kuona mchezaji ambaye umri umekwenda anatisha katika ligi yetu. Wachezaji wazee wanapaswa kukimbia kwasababu ya ushindani mkali wanaokutana nao na si kuja kwasababu wanaona hapa ndipo wanaweza kupumzika katika umri wao wa uzee.

Pia tunapaswa kumpongeza Kiiza. Katika umri wake tunaotilia shaka bado anaweza kucheza kwa ubora mkubwa katika ligi aliyotisha miaka 10 iliyopita.

Si wachezaji wote wanafanikiwa kujitunza kama yeye, kwani wapo wapi wachezaji vijana wa Kitanzania waliopaswa kucheza katika nafasi yake?

Columnist: www.tanzaniaweb.live