Mtu mmoja alinitingisha mtaani akaniuliza namna ninavyomtazama mshambuliaji mpya wa Simba, Kibu Dennis. Amekuwa akicheza mara kwa mara katika siku za usoni. Kwa miaka ya usoni Simba haijawa nyumba salama sana kwa wachezaji wazawa wanaocheza eneo la ushambuliaji. Kando ya John Bocco hakuna mchezaji mwingine wa ndani anayeweza kusema amepata nafasi ya uhakika katika kikosi cha Simba kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Labda Hassan Dilunga ambaye amekuwa akiingia na kutoka. Ni habari njema anapotokea mzawa kama Kibu na kufanikiwa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Simba.
Kibu amekuwa akicheza vizuri katika siku za karibuni. Hapana. Siyo siku za karibuni. Kibu amekuwa akicheza vizuri tangu akiwa na uzi wa dhambarau wa Mbeya City kule Nyanda za Juu Kusini, tatizo letu tunapenda kuwatazama wachezaji wanapofika Simba na Yanga.
Wakiwa nje ya hapo hakuna anayejali habari zao. Kama nilivyosema hapo awali Kibu amekuwa akicheza vyema, lakini nilikuwa na mawazo tofauti kidogo juu ya uchezaji wake.
Zaidi ya kile kitu anachokifanya uwanjani sasa kuna kitu kimoja natamani angekifanya zaidi. Labda angekuwa mchezaji hatari zaidi ya hapa.
Kwanza kabisa Kibu anapaswa kuelewa uimara wake mkubwa upo wapi. Kila mchezaji kama ilivyo kwa kila binadamu ana uimara na udhaifu wake. Katika hali ya kawaida ni rahisi kuimarisha uimara wako kuliko kupunguza udhaifu wako.
Inashauriwa kuweka nguvu kubwa katika kuukuza uimara wako kisha ufanye kazi nyingine ya ziada kupunguza udhaifu wako.
Ni rahisi zaidi kufanikiwa kwenda juu kwa kufanyia kazi uimara wako kuliko kupunguza udhaifu wako. Haibadiliki kwa wachezaji.
Mchezaji anapaswa kuufanyia kazi zaidi uimara wake. Kwa mfano mshambuliaji mzuri kwenye kufunga lakini dhaifu katika kupiga chenga anashauriwa kufanyia kazi zaidi uwezo wake wa kufunga kuliko kufanyia kazi uwezo wake wa kupiga chenga. Bila shaka tumeelewana.
Nafikiri uimara mkubwa zaidi wa Kibu upo katika mwili wake. Kibu ni kati ya wachezaji wachache wazawa waliobarikiwa miili yenye nguvu. Ana mwili mzuri uliojengeka kiuchezaji. Ana misuli iliyojaa chakula.
Kwa sababu hiyo mwili wake unamruhusu kucheza soka la nguvu. Anaweza kwenda katika vita ya ‘kushindana ugali’ na mabeki akaibuka mshindi.
Kibu anapaswa kucheza soka la nguvu zaidi. Ninavyoutazama uwezo wake sio aina ya mchezaji anayeweza kucheza soka maridadi la chenga kama Bernard Morrison.
Kibu anapaswa kuacha kufikiria soka la chenga nyingi kama anavyojaribu kufanya sasa kwa sababu hana wepesi na ubongo wa kucheza hivyo.
Tatizo kubwa la nchi yetu ni kwamba tunaamini mchezaji mzuri ni yule anayekusanya mtaa na ku-ondoka nao akipiga chenga nyingi na kufanya mbwembwe nyingi hata kama haziisaidii timu.
Cristiano Ronaldo aligundua uimara wake upo katika kufumania nyavu akabadili maisha yake kuwa mfungaji - maisha yaliyomfanya kuwa mchezaji bora wa dunia mara tano.
Ronaldo hakutaka kuwa mtu wa kupita katikati ya msitu kama Messi na bado alifanikiwa. Kibu anahitaji fikra kama hizi. Chagua uimara wako kisha ufanyie kazi.
Ni mawazo ya aina hii wanayoishi nayo wachezaji wa DR Congo wanaotamba kwa sasa katika Ligi Kuu Bara. Wakongomani hawana vipaji vikubwa sana, bali wamechagua mambo kadhaa wanayoweza kisha wakayafanyia kazi.
Ni mambo hayo yanayowafanya waonekane ni wachezaji wa maana sana. Wenye nguvu wamechagua kucheza kwa kutumia nguvu kubwa kama anavyofanya Tonombe Mukoko na Mkongomani mwenzake anayemuweka benchi kwa sasa pale Yanga, Yanick Bangala.
Kule Simba yupo mtumiaji mwingine mkubwa wa nguvu kutoka DR Congo anaitwa Henock Inonga. Wakongomani wenye mbio wameamua kucheza soka la kasi kama ilivyokuwa kwa Tuisila Kisinda na sasa Jesus Moloko.
Fiston Mayele anajua kufumania nyavu, lakini ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira ndiyo maana amechagua kuisaidia timu icheze zaidi mchezo kuliko kufunga peke yake.
Chris Mugalu anajua kusumbuana na mabeki na mara zote anafanya hivyo hata kama hatafunga. Ni mambo kama haya Kibu na wachezaji wetu wote wanapaswa kuyaelewa na kuyafanyia kazi. Hauhitaji mambo mengi ili uwe bora.