Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kamati za saidia Taifa Stars tunaunda lini?

Stars Lose 2 Mchezo wa Stars dhidi ya Algeria kwa mkapa, Dar

Fri, 10 Jun 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Hadi kesho nitaendelea kuamini hakuna maana bora zaidi ya mwanasiasa kuizidi ile ya Mjerumani, Max Weber. Katika ubora wake Weber alisema Mwanasiasa ni mtu yeyote asiyefurahi kuona matatizo yanaisha katika jamii halafu ni mtu anayependa kuwa midomoni mwa watu.

Mwanasiasa anahitaji jamii iwe na matatizo ili ayatumie kuonyesha ushawishi wake.

Mtaji wa kwanza wa mwanasiasa ni matatizo yaliyopo katikati ya watu wake; “Nitawaletea maji, nitawajengea shule, nitawahakikishia usalama.”

Ahadi kama hizi haziwezi kutolewa kama hakuna matatizo katikati ya watu. Furaha ya mwanasiasa yoyote yule ni kuzungumzwa na watu, iwe kwa mema au mabaya lakini furaha ya mwanasiasa yoyote yule ni kuwa midomoni mwa watu.

Ndiyo maana zinapokuja fursa za kuwa midomoni mwa watu huwa hawaziachi zipite kando.

Moja ya fursa ambayo hujitokeza nchini ni kipindi inapocheza timu ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars.’ Siyo tu inapocheza timu ya taifa bali inapocheza timu ya taifa na kuonekana kama kuna nafasi ya kufanikiwa kupata chochote.

Huwezi kusikia wanasiasa wameivamia timu ya taifa kama hakuna mwanga wa kupata chochote.

Kwa mfano, juzi kipindi imetokea ‘miujiza’ tukakaribia kufanikiwa kuvuka kundi katika harakati za kwenda kombe la dunia ndipo tuliona imeundwa kamati na ahadi nyingi zikatolewa kama tungefanikiwa kumfunga DR Congo na kuiweka hai ndoto ya kwenda Qatar.

Hapo ndipo unakaa chini na kujiuliza, walikuwa wapi hawa watu wakati tunacheza mechi za mtoano kwenda hatua ya makundi? Hivi tulikuwa tunamaanisha kweli tulipokuwa tunasema, Tunatoboa mpaka Qatar?

Kabla ya hapo zilikuja ndoto za kufuzu AFCON na kupotea ghafla. Baada ya kufuzu mara ya mwisho ilionekana kama kuna nafasi ya kutoboa tena na kurejea AFCON kwa mara nyingine.

Ndipo iliundwa kamati nyingine ya kisasa iliyokuja na ile kauli mbiu ya ‘Tumenogewa, tunarudi tena.’ Tulipoteza dhidi ya Guinea ya Ikweta pale Malabo na ndoto za AFCON zikayeyuka kama ilivoyeyuka kamati yake.

Kamati haikuwahi kukaa chini kujiuliza nini kimetufelisha au tufanye nini kurejea mara nyingine.

Ni maisha tu ya wanasiasa kutotaka kuachwa nyuma katika fursa zitakazowaweka midomoni mwa watu. Si kweli mambo yanafanyika kwa uzalendo bali fursa zinazoonekana kupitia matokeo ya Stars.

Ushahidi wa hili ni kuitazama hali ya sasa ya Stars, sasa hivi Stars inacheza mechi za kufuzu AFCON na hakuna mwanasiasa yoyote anayeitazama. Hakuna ahadi yoyote inayotolewa kama watashinda mechi. Kila mtu yupo kimya.

Kuna jambo moja naweza kulitabiri. Kama Stars watafanya vizuri, tukafika mechi ya tano tukiwa na nafasi ya kutoboa kundi, nina uhakika wanasiasa watajitokeza katika machimbo waliyojificha sasa na kuunda kamati za hamasa za kuisapoti Stars kwasababu wanajua kama tutafuzu AFCON wataachwa nyuma.

‘Nisiwaandame’ sana wanasiasa! Yapo makundi mengi ambayo huibuka baada ya kuona Stars inafuatiliwa au inakaribia kupata mafanikio.

Makundi haya huundwa na wasanii, wanahabari, matajiri, wachambuzi wa michezo na watu wengine wenye ushawishi mkubwa kwenye jamii. Nadhani huu ndio muda muafaka wa kujitokeza na kuisapoti Stars.

Huu ndio muda mwafaka wa kujitokeza na kuonesha ni wazalendo wa kweli wa timu ya taifa. Tusisubiri Stars ipambane yenyewe kisha ikiukaribia mlango wa AFCON ndipo tujitokeze tulipojificha na kujifanya ni wazalendo wa kweli wa timu ya taifa. Kama kuna kamati za hamasa na michango ziundwe sasa kuonyesha kweli tunaisapoti taifa Stars.

Lakini hapohapo wakati tunaunda kamati za hamasa tukumbuke hamasa ina mchango mdogo sana katika mpira wa miguu. Mara nyingi sana mshindi anakuwa yule aliyefanya maandalizi mazuri kuliko mwenzake. Hapo tujiulize Stars imejiandaa vizuri?

Kumbuka maandalizi hayaishi katika kujiandaa na mechi pekee! Kwa mfano kuna timu Afrika hii ilishaweka mipango ya jinsi ya kwenda kuutwaa AFCON ijayo baada ya kufeli AFCON iliyopita.

Sisi leo tunaenda kutekeleza mipango tuliyoiweka lini?

Wale wachezaji tuliwaandaa kwa ajili ya kuitumikia timu ya taifa au wametokea kusipojulikana kwa nguvu zao wenyewe tukaona wanafaa kuitumuikia timu ya taifa.

Wachezaji wote wale tuliwaandaa kwa ajili ya kuitumikia timu ya taifa? Vipi kuhusu George Mpole na Aziz Andambwile wa Mbeya City? Vipi kuhusu wale wanaocheza Uingereza, tuliwaandaa sisi?’

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz