Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: GSM na matajiri wengine waheshimiwe

GSM (600 X 488) Ghalib Said Mohammed, mmiliki wa GSM

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Niliwatazama Yanga wakiwasambaratisha KMC kule Songea nikakumbuka kisa fulani. Nitakueleza ni kisa gani hivi punde. Niliwatazama tena wakiwasambaratisha Azam pale kwa Mkapa kwa soka safi la kitabuni nikakikumbuka kile kisa.

Mashabiki wa Yanga katika ubora wao chini ya tajiri Yusuph Manji waliwahi kujisahau ‘wakaropoka’ maneno fulani ya kejeli kwa Manji. Walisema Yusuph Manji anawahujumu na hapaswi kuwa sehemu ya Yanga. Walienda mbali na kusema Manji awaachie Yanga yao. Mambo yanaponyooka binadamu tuna tabia ya kubweteka na kusahau tulipotoka. Manji alipata matatizo na serikali akaamua kuondoka nchini. Akawaachia Yanga wenye Yanga yao. Tabu ikaanza rasmi Jangwani.

Baada ya hapo ulifuata msururu wa sinema zisizokwisha ndani ya Yanga. Kila kitu kilivurugika. Wachezaji walivurugika. Mashabiki walivurugika. Viongozi walivurugika. Kila kitu kilivurugika - tatizo la kuvurugika? Pesa.

Timu haikuwa na uwezo wa kujiendesha. Ukosefu wa pesa ndio ulileta ile kampeni ya kutembeza bakuli. Nyakati hizo ndipo Yanga waliitambua thamani ya Manji pale Jangwani. Bahati mbay, wale watu walioitaka Yanga yao kutoka kwa Manji na wao hawakuonekana. Walitokomea kusikojulikana.

Yanga ikabaki tabani hadi alipotokea tajiri aitwaye Gharib Said Mohamed. Yeye mwenyewe anajiita ‘Simba’. Taratibu alirejesha utulivu ndani ya Yanga. Hakukuwa na miujiza yoyote aliyoifanya zaidi ya kuweka pesa.

Pesa aliyoiweka ndiyo ilileta utulivu Yanga. Kama unakubali GSM ameibadilisha Yanga nitumie ujumbe mfupi kwenye namba yangu ya simu hapo juu.

Baada ya Yanga kupata utulivu akamwaga pesa zake tena kuirejesha Yanga kwenye makali yake. Hili lilichukua muda zaidi na haikuwa rahisi kuifikisha Yanga hapa ilipofika leo. Haikuwa rahisi kupata wachezaji waliowapata leo iliwalazimu Yanga kufanya makosa kadhaa kuwasajili kina Yikpe ili kufika hapa walipo.

Pesa yote ya usajili ilikuwa inatoka mfukoni kwa GSM. Kando ya pesa ya usajili bado sehemu kubwa ya pesa ya matumizi ya Yanga ikiwemo mishahara na gharama za usajili ilitoka GSM. Kazi kama hii Mo Dewji ameifanya na bado anaifanya sana pale Msimbazi.

Kuna kipindi baadhi ya viongozi walitaka kuwakosea GSM. GSM wakaandika barua ya kujiweka kando na shughuli zote zilizo nje ya mkataba wao na Yanga. Watu wa Yanga walikuja juu kweli ilibidi uongozi ufikie uamuzi wa busara kuwafuta kazi watu waliomtibua tajiri.

Hii ilionyesha ni kwa kiasi gani mashabiki wa Yanga wameelewa umuhimu wa matajiri kushikilia klabu. Ile misemo ya kwamba atuachie klabu yetu haikusikika, walishaonja joto ya jiwe bila Manji. Walishaona maisha yalivyo mepesi kwa wapinzani wao wa karibu Simba kwa sababu ya pesa za Mo Dewji. Hawakuwa tayari kumpoteza GSM kwa sababu walijua ugumu wa kuishi bila pesa za msaada kutoka kwa wafadhili. Ndiyo! Pesa za msaada.

Kuna ujinga wa watu kujidanganya kwamba hawa kina GSM ni wadhamini wa klabu na si wafadhili. Ukweli ni kwamba, hawa ni wadhamini lakini wanaishi zaidi kama wafadhili kuliko wadhamini.

Mdhamini ni yule anayeingia mkataba na klabu wa kumtangaza kisha yeye analipa pesa na kukaa pembeni, lakini hawa kina GSM wanalipa pesa walizozisaini katika mikataba lakini bado wanatoa pesa nyingine nyingi za pembeni kuendesha klabu.

Yote haya yanatokana na klabu kukosa vyanzo vya kueleweka vya mapato. Kama unaamini GSM ameibadilisha Yanga kwa kiasi kikubwa niandikie maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Klabu kubwa duniani zinategemea zaidi wadhamini kuliko wafadhili. Klabu kubwa duniani zinaingiza pesa kupitia vyanzo vikuu vinne - kwanza ni haki za matangazo ya televisheni kama inavyofanyika kwa sasa na Azam TV. Pili ni mdhamini anayewekwa kwenye jezi, tatu ni mauzo ya jezi na nne mapato ya mlangoni.

Huku kwetu tuna chanzo kimoja pekee cha kueleweka - pesa inayotokana na haki za matangazo ya televisheni. Hivi vingine bado tunaombeana Mungu, bado tunahitaji kuhamasisha mashabiki kwenda viwanjani. Bado tuna mashabiki wanaovaa jezi feki kwa sababu wanakwepa gharama za kununua jezi orijino za klabu. Bado klabu zetu hazina ushawishi mkubwa wa kibiashara kiasi cha kusaini mikataba minono na wadhamini wanaoweka majina yao kwenye jezi. Ni kwa sababu hiyo bado mapato ya klabu zetu ni duni. Ndiyo sababu bado tunawahitaji na kuwategemea sana wafadhili kama GSM. TUWAHESHIMU.

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz