Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Feisal kuvaa jezi ya Azam? labda nipo ndotoni

Feisal Salum Winning Goal Kiungo wa Yanga, Feisal Salum

Thu, 8 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kila napomtazama Feisal Salum ‘Fei Toto’ uwanjani huwa nafurahi sana. Fei anafurahia kucheza mpira. Huwa hachezi mpira kwa hasira na hana papara. Hateseki mpira unapokuwa miguuni kwake na hauogopi.

Siku hizi ameongeza kitu kingine katika mchezo wake. Siku hizi anafunga sana akiwa ndani ya jezi ya Yanga na mara kadhaa akiwa na ile jezi ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Juzi tu ameitoa Yanga katika mdomo wa mamba kwa bao lake la dakika za jioni dhidi ya Tanzania Prisons.

Yanga walikuwa safarini kudondosha alama zingine baada ya Ihefu kumaliza ‘unbeaten’ yao lakini Fei aliwaokoa. Kama nilivyosema hapo awali Fei anafurahia mpira.

Nilipomtazama Fei dhidi ya Tanzania Prisons nilikumbuka jinsi ambavyo majuzi Azam FC waliwatishia Yanga kwamba watamsajili na kumpeleka Chamanzi.

Kwamba Azam FC watawashawishi Yanga kwa dau nono ili Fei akavae jezi yao. Inashtua kidogo.

Kwanza ni ukweli kwamba Fei ni kati ya viungo bora wazawa kwa sasa kama sio bora zaidi kuliko wote. Labda unaweza kumuweka Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Jonas Mkude katika kundi hilo lakini kwa sasa mzani unaonekana kuelemea zaidi kwa Fei. Anacheza popote pale eneo la kiungo tena kwa ubora uleule.

Iwe kiungo mshambuliaji, kiungo wa kati au kiungo mkabaji ambapo hajachezeshwa siku za karibuni.

Hapo ndipo swali la kwanza litakuja. Kwa ubora huu Yanga watakubali kumpoteza tena kwa mpinzani wao wa karibu?

Ukiwapa Azam Fei inamaanisha unawaimarisha katika maeneo matatu tofauti.

Kwa hiyo itakuwa rahisi kwa Azam kushughulikia maeneo mengine yaliyo na matatizo zaidi na kuachana na eneo la kiungo kwa sababu tayari wanajua wana mtu anayeweza kucheza popote pale kama watamkosa mmoja wa viungo wao.

Kwa mfano sasa hivi Yanga wanaweza kumkosa kiungo yeyote yule na wasiwe na wasiwasi kwa sababu wanajua Fei yupo na atacheza.

Yanga wanaweza kumkosa Sure Boy wakamchezesha Fei eneo lake. Pia wanaweza kumkosa Aziz Ki bado wakamchezesha Fei eneo lake. Ndiyo maana Yanga hawawezi kufikiria kusajili kiungo kwa sasa.

Yote tisa, kumi tukumbuke huyu Fei tunayemzungumzia ni mchezaji mzawa.

Unapompoteza Fei itakubidi uende nje ya nchi kumtafuta mbadala wa kuvaa viatu vyake. Hapo kumbuka nchini kwetu kuna kanuni ya ukomo wa wachezaji wa kigeni. Kwa hiyo unapompoteza Fei kwa kumleta mgeni eneo lake ina maana unapoteza nafasi moja ya mchezaji wa kigeni.

Kwa hali halisi ya wachezaji wanaopatikana nchini kwetu unapaswa kukazana kuwa na wachezaji bora zaidi wazawa kisha maeneo mengine uyazibe kwa wageni.

Nasikia Fei bado amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na Yanga. Inashtua kidogo.

Ilikuwaje Yanga wakathubutu kumpa Fei mkataba wa muda mrefu kiasi kile? Sijui nani aliwauma sikio Yanga kipindi kile kwamba siku moja atakuwa katika ubora huu alionao sasa. Vinginevyo, kwa ule utaratibu wa kutoa mikataba ya miaka miwili miwili sasa hivi Yanga wangekuwa wanateseka kumzuia Fei asiondoke.

Lakini kwa kuwa bado ana mkataba mrefu, Yanga hawana hofu ya kumpoteza. Ni mikataba kama hii walipaswa kusainishwa wachezaji tangu zamani. Tatizo ni kwamba wachezaji wengi wa Afrika hawaaminiki. Unaweza kumsajili akiwa bora sana lakini akaporomoka uwezo ndani ya miezi sita hadi ukajuta kumsajili.

Vinginevyo nafikiri Yanga wapo salama sana katika suala la Fei kwenda Azam kwa sababu ya mkataba.

Wanachoweza kufanya sasa hivi Yanga ni kumuweka chini na kuboresha maslahi yake kisha wakaongeza muda zaidi katika mkataba wake.

Soka linaweza kuwa biashara, lakini siyo kupoteza silaha muhimu kwa mpinzani wako wa karibu. Yanga wanaweza kufanya biashara ya Fei, lakini siyo kumruhusu aende Simba au Azam. Wanaweza kumuuza Misri, Morocco au Afrika Kusini kisha wakafaidika kwa kupata kitita kikubwa cha pesa lakini sidhani kama wanaweza kumruhusu kuvaa jezi ya Azam. Simuoni Fei akiwa jezi ya Azam siku za usoni.

Columnist: Mwanaspoti