Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Dilunga Taifa licheke au Simba walie?

94369 Dilunga+pic UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Dilunga Taifa licheke au Simba walie?

Thu, 2 Dec 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KOCHA Pablo Martin Franco kutoka Hispania aliingiza tena jeshi lake uwanjani ‘wikiendi’ iliyopita kuwavaa Red Arrows ya Zambia, katika kikosi chake cha kwanza alilikabidhi bawa la kushoto kwa mtanzania Hassan Salehe Dilunga.

Kwa sasa haishtui sana kuliona jina la Hassan Dilunga katika kikosi cha kwanza cha Simba, hali ilikuwa tofauti miezi sita iliyopita, miezi sita iliyopita Dilunga angewekwa uwanjani na kila shabiki wa Simba angepingana na uamuzi wa kocha wakiamini hastahili kuwa sehemu ya kikosi kinachoanza mechi ya Simba.

Kumbuka tunatokea taifa ambalo mashabiki wanaelewa soka kuliko makocha na wataalamu waliolipa ada vyuoni kulisoma soka lenyewe. Sisi bwana!

Pablo anaingia katika ‘msururu’ wa makocha waliompa imani Dilunga katika siku za usoni, alianza Didier Gomes mwanzo wa msimu, kisha akaja Thierry Hitimana.

Wote wameona Dilunga anastahili kuwa sehemu ya kikosi chao cha kwanza, hili linaweza kuwa jibu kwa wanaohoji uhalali wa nafasi ya Dilunga kikosi cha kwanza, haijatokea kwa bahati mbaya makocha wote watatu wakampa nafasi, lazima kipo kitu cha tofauti wanachokiona au wanachokipata kutoka kwa Dilunga ndiyo sababu wanampa nafasi. Ingekuwa ni kocha mmoja tungeweza kuzungumza vinginevyo lakini si kwa wote watatu.

Mara nyingi wachezaji kama Dilunga ni wachezaji wa kimbinu zaidi, ni aina ya wale wachezaji ambao mashabiki hawavutiwi nao kwasababu hawawaoni wakifunga au wakipiga chenga. Yanahitajika macho ya kiufundi zaidi kuwaelewa.

Mtu mwingine wa aina yake ni Mzamiru Yassin, kule Yanga yupo Deus Kaseke wa msimu uliopita, wachezaji wa aina hii hupendwa na makocha kwasababu ya ufanyaji kazi wao uwanjani, ni mchezaji ambaye ukimpa jukumu fulani uwanjani analitekeleza kwa asilimia zote.

Unaweza usipate vitu vingi kutoka kwake lakini unaweza ukapata kitu kimoja cha uhakika. Bernad Morrison anaweza kukupa chenga za kusisimua, pasi za uhakika na mabao maridadi lakini hawezi akakupa ukabaji wa uhakika. Lazima atawahitaji kina Mzamiru wa kumtafutia mpira.

Lakini mtu mwingine anaweza kukuuliza kwanini Dilunga hakuwa anapata nafasi kikosi cha kwanza misimu iliyopita? Ina maana Dilunga amebadilika ghafla tu kutokea pasipojulikana na kuwa mchezaji wa kimbinu?

Jibu rahisi ni kwamba msimu uliopita alikumbana na upinzani mkali kutoka kwa Luis Miquissone ambaye kwasasa anachechemea kule Misri. Lakini hata hivyo licha ya ushindani mkali wa nafasi uliokuwepo ndani ya Simba, bado Dilunga alifanikiwa kulazimisha nafasi yake kikosini. Msimu uliopita jina la Dilunga lingekuwa la kwanza kukivamia kichwa chako kama Simba wangekuwa wanakwenda kucheza uwanja mgumu moani.

Tukiwa hapohapo, unaweza kuwaza kitu kingine kichungu ambacho viongozi na mashabiki wa Simba hawatapenda kukisikia. Labda Simba hawakufanya usajili wao vizuri sana kuziba pengo la mmakonde Luis ndiyo maana mchezaji ambaye hakudhaniwa kama angepata nafasi ya kucheza leo amefanikiwa kuingia kikosi cha kwanza na kuwa kati ya wachezaji wa kutegemewa.

Kipindi vurugu za usajili zikiendelea nchini Simba walisajili mawinga wengi kuliko wachezaji wa maeneo mengine, walimsajili Peter Banda, Yusuph Mhilu, Duncan Nyoni, Kibu Dennis na Pape Osman Sakho. Hawa wote hakuna aliyefanikiwa kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza, Kibu Dennis amejitahidi kidogo lakini bado hajapata nafasi ya uhakika.

Kwetu sisi kama taifa, hili ni jambo la kufurahia kuona Mtanzania anapata nafasi mbele ya wageni waliofuatwa na kuletwa nchini kwa pesa nyingi. Simba hapajawa sehemu salama kwa watanzania katika miaka ya usoni, eneo la kiungo kuja mbele limekuwa likitawaliwa na wageni.

Ni John Bocco na Jonas Mkude pekee waliofanikiwa kufurukuta na kuchomoza mbele ya wageni tena kwa kusuasua, inapotokea tunapata mtu mwingine wa kutuwakilisha, tunapaswa kufurahi.

Watu pekee ambao ni ngumu kuelewa hali za hisia zao ni Simba. Alipoondoka Luis walitegemea wapate mchezaji mwenye uwezo sawa na wake au amkaribie kwa kiasi, hawakutegemea Dilunga awe mbadala wake licha ya juhudi na kujituma sana bado Dilunga hamsogelei Luis. Kama unabisha tazama takwimu zitakuambia.

Hadi sasa Dilunga hajafunga wala kupika bao lolote, sidhani kama Simba wanafurahia hili, hapo ndipo lile swali nililouliza kule juu linakuja, sisi kama taifa tufurahi kumuona Dilunga ndani ya kikosi cha kwanza Simba au Simba wahuzunike kumuona mchezaji wa uwezo ule akiingia katika kikosi cha kwanza?

Columnist: www.mwanaspoti.co.tz