Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ajibu ni zaidi ya Clatous Chama?

Drg Ajibu Ibrahim Ajibu

Tue, 8 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Inahitaji moyo kama wa mwendawazimu kwa mtu wa mpira kuja na kauli kama hii. Inahitaji nguvu kubwa sana, inahitaji maelezo mengi sana kutetea hoja hii. Unajua ni kwa nini? Ni rahisi tu.

Chama ana vitu kibao ambavyo ameshathibitisha uwezo wake. Chama ana namba ambazo zinamtetea. Chama ana rekodi ambazo zinaishi. Baada ya kuzaliwa na kukuzwa na Simba, Ibrahim Ajibu Migomba ni mmoja wa watu wenye vipaji vya soka vya hali ya juu sana.

Ni mtoto aliyejaa ufundi mwingi sana miguuni mwake. Ni kijana mwenye miguu ya dhahabu. Ikawa asubuhi, ikawa Jioni Migomba akajiunga na Yanga. Aliikuta Yanga iko chumba cha wagonjwa mahututi. Aliikuta Yanga imepoteza uelekeo. Hohehahe. Taabani. Waleo, wajana.

Yanga walimpa heshima kubwa na kumfanya kuwa nahodha. Kumaliza msimu na pasi za mabao 17 huku kambani akiwa ameingia mara sita, ni namba ambazo kwa haraka utazikuta kwa Clatous Chota Chama.

Kwa kizazi hiki ni Mwamba wa Lusaka tu ndiye anaweza kukupa namba hizo. Ajibu alikuwa fundi kweli kweli. Mpira ulikuwa unatii kwenye miguu yake.

Alikuwa na uwezo wa kuamua ni muda gani mpira utembee. Ni muda gani mpira ukimbie. Ni mara chache sana Tanzania tumezalisha wachezaji wa aina hii na hasa kwa Kizazi hiki. Hapa ndipo swali la Ajibu kumzidi uwezo Chama huwa linakuwa gumu.

Hapa ndipo unapoona utofauti wa mbingu na aridhi baina yao. Mmoja ana namba zinazoongea. Mwingine ana hisia zinazohisiwa!

Siku chache zilizopita, nimemwona Ajibu akisajiliwa na Coastal Union. Ni klabu kubwa. Ni klabu kongwe sana kwenye Soka la Tanzania. Kama Ajibu ataamua kucheza mpira, bado namwona akirudi kwenye ubora wake.

Uzuri wa ligi ya Tanzania, mastaa wake wengi wenye majina makubwa ni wale wenye umri mkubwa. Pamoja na Waafrika kudanganya umri, John Bocco sio mtoto. Pamoja na umri wake mkubwa, bado hakuna mshambuliaji mzawa anayefikia uwezo wake.

Meddie Kagere ni staa mkubwa kwenye ligi yetu lakini ni mtu mzima. Ni mtu ambaye kwa kumtazama tu unaweza kumpa shikamoo. Hata Fiston Mayele mwenyewe sio mtoto. Ni mtu mzima mwenye umri mdogo kwenye pasipoti ya kusafiria. Ndiyo maisha ya watoto wa Kiafrika.

Katika kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni, sijaona mchezaji wa Kitanzania mwenye miguu ya dhahabu kama Ajibu. Hakuna namba 10 ya ufanano wake kwa wazawa. Kama Ajibu angeamua kucheza kwa bidii na nidhamu, pengine Simba wasingemleta Clatous Chota Chama pale Msimbazi. Majukumu ya Chama yangeweza kutimizwa vizuri tu na Ajibu. Najua unahitaji moyo kama wa mwendawazimu kujadili hili.

Leo hii kumfananisha Ajibu na Chama inaonekana kama kuchanganyikiwa! Leo hii watu wanaweza kukuachia kijiwe kama unaleta stori hizi. Unajua ni kwa nini?

Ni rahisi tu. Watu wamemwona Chama akiwalambisha mchanga kwa Mkapa mabeki wa Al Ahly. Watu wamemwona Chama akiwashikisha adabu kwa Mkapa Wakongo wa As Vita.

Amekuwa muhimu kwenye kuiwezesha Simba kushinda mataji ya ndani. Amekuwa muhimu kwenye kuipeleka Simba hatua ya robo fainali mara kadhaa.

Hii ndiyo tofauti kubwa ya Ajibu na Chama. Kwa kutazama kipaji Kwa Wachezaji wote wawili, naweza kubishana hadi asubuhi.

Lakini kwa kutazama namba na mafanikio, naishia kujisonya tu mwenyewe! Ni mbingu na aridhi.

Ajibu ameachwa pakubwa mno. Unahitaji moyo kama wa mwendawazimu kuwafananisha.

Coastal Union sio timu ndogo. Wagosi ni Wafalme wa Tanga. Bado ufundi wa miguu ya Ajibu uko pale pale. Saido Ntibazonkiza ameibuka Geita Gold FC na kuja kuwa mfungaji Bora wa Ligi Kuu akiwa na Mnyama Simba.

Wachezaji wetu wazama wengi wanacheza kwa kujisikia. Kuna wachezaji wachache sana wa kigeni wanaowazidi uwezo na kipaji wazawa wetu.

Tofauti kubwa ya wachezaji wa kigeni na vijana wetu ni kujituma na nidhamu ya kazi. Hakuna kitu kingine. Wageni wengi wanakuja kupambana.

Wanajua fika hawana maisha ya kudumu hapa kama hawataonyesha kiwango bora. Wazawa wetu wengi ni vipaji kweli kweli lakini hawana nidhamu! Hapa ndipo tobo lilipo. Hapa ndipo mwanya wa wageni na wazawa ulipo.

Ni vigumu sana kumlinganisha Chama na Ajibu kwa sasa. Ni vitu viwili tofauti lakini kama ungewaona wote miaka 10 nyuma, huenda Ajibu alikuwa eneo moja na Mwamba wa Lusaka.

Wagosi wana heshima kubwa kwenye Soka la Tanzania. Bado nahisi Ajibu ana kitu. Kutoka Simba, Yanga, Azam hadi Singida na baadaye Coastal Union, ni kushuka kidaraja.

Lakini ni nani ambaye hajawahi kushuka kwenye eneo lake? Hakuna. Kila mtu kwenye kazi yake huenda amewahi kushuka. Ndiyo maisha yalivyo. Kushuka sio kuanguka hata kidogo. Bado naamini kama Ajibu akiamua anaweza kurudi kabisa kwenye ubora wake.

Unamkumbuka Jonas Mkude wa misimu yake ya mwisho pale Simba SC? Ni kama alikuwa amekwisha kabisa.

Umemwona mechi ya Yanga vs Kaizer Chiefs pale kwa Mkapa akiwa na jezi ya Yanga? Ni kama amezaliwa upya. Ni kama miaka yote 13 aliyocheza Simba, nyumbani kwao palikuwa Yanga. Ni Ajibu tu kuamua.

Bado ana umri wa kuendelea kucheza bila kikwazo chochote. Bado zile pasi 17 za mabao alizopiga akiwa na Yanga misimu mitano nyuma anaweza kuzipiga leo. Bado ule ubora aliokuwa nao msimu 2018/2019, anaweza kuupata leo.

Kwa mtu ambaye amemwona Ajibu akishindwa kutamba na Azam FC, atakupiga makofi akiona unamfananisha na Mwamba wa Lusaka. Atakupiga akisikia unasema hawa wawili wana kipaji chenye mfanano.

Unahitaji moyo kama wa mwendawazimu kuwalinganisha kwa sasa. Utofauti ni mkubwa sana. Chama ana Unyama mwingi sana.

Nakukubali sana Ajibu. Mimi ni shabiki yako mkubwa. Nakutakia heri hapo Tanga. Wape furaha Wagosi wa Kaya.

Columnist: www.tanzaniaweb.live