Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE KALIUA: Yanga SC walivyoweka upande wao mechi ya derby

Simba Yanga Mb.jpeg Yanga waliibuka na ushindi wa goli 1-0

Thu, 2 Jun 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Jinsi Feisal Salum alivyokimbia pembeni kwenye kibendera akiwa ameziba uso wake kushangilia bao la mbali alilomtungua kipa wake wa zamani, Beno Kakolanya ni jinsi hiyohiyo alikuwa amekimbia na kuziba ndoto za Simba za kutwaa walau taji moja la msimu.

Jinsi maisha yanavyobadilika ghafla katika ardhi yetu tuna Simba iliyobaki kuonyesha Kombe la Mapinduzi kama taji pekee msimu huu.

Ni Simba hawa waliokuwa wababe wa Tanzania miezi kadhaa nyuma, lakini leo wameufyata mkia mbele ya Yanga. Majuzi pale CCM Kirumba - Mwanza walikuwa na nafasi ya mwisho kuwafunga mdomo Yanga, lakini shuti la ‘kilomita 1000’ la Fei Toto liligonga msumari wa mwisho katika jeneza la unyonge wa Simba msimu huu.

Lilikuwa bao zuri kutoka Fei Toto, lakini likiwa na maswali mengi kwa Simba. Kwanza ni jinsi viungo wa Simba walivyomruhusu Fei Toto kukanyanga hatua zote zile bila kumpatia bugudha yoyote. Fei Toto alipata muda wote aliohitaji duniani kufanya uamuzi alioutaka.

Mmoja kati ya viungo wa Simba alipaswa kumpatia usumbufu Fei Toto ili asipate umakini alioupata wakati anafanya uamuzi wa kutembea na kupiga kutokea umbali ule aliokuwepo.

Viungo walipaswa kumsumbua na kumlazimisha kucheza pasi au kukosa utulivu na mpira. Ajabu ni kwamba Simba walianza na viungo watatu wazuiaji.

Lakini, hapo bado unakaa chini unatazama jinsi Simba walivyopoteza mpira katikati ya uwanja. Kulikuwa na uzembe mkubwa jinsi Simba walivyoporwa mpira na kumruhusu Fei Toto kuwatungua.

Pasi hafifu ya Mzamir Yassin ilipozuiwa kumkuta Chris Mugalu, Mzamiru alirudi nyuma akikimbia kivivu badala ya kuwa wa kwanza kumzuia Khalid Aucho aliyempasia Fei Toto. Huu ni mwendelezo wa mabao ya mbali ambayo Yanga wamekuwa wakiwatungua Simba kwa miaka mingi.

Hivi majuzi, Mzamiru huyuhuyu alipoteza mpira kisha kiungo wa Yanga, Balama Mapinduzi akafunga kutoka mbali na kumuachia Aishi Manula kesi nzito.

Msimu huohuo Fei Toto huyuhuyu alimtungua tena Manula kutokea mbali katika Kombe la Shirikisho, lakini bao lake lilisahauliwa kwa sababu Yanga walipoteza kwa tofauti kubwa ya mabao.

Zamani sana, April 1992, beki wa kushoto wa Yanga, mbabe Keneth Mkapa aliwahi kumtungua Mohamed Mwameja wa Simba kutoka umbali mrefu. Juzi Fei Toto alikuwa akiendeleza kile ambacho Yanga wamekuwa wakiwafanyia Simba kwa miaka mingi.

Kando ya hapo ni jinsi kocha wa Yanga alivyofanikiwa kumkamata kwenye mbinu kocha wa Simba, Pablo Franco. Nilikuwa nikizungumza na rafiki yangu kabla ya mechi kwamba, kocha atakayekuwa na ujasiri wa kubadilika na kumshangaza mwenzake atakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Ndicho alichofanya kocha wa Yanga, Nasreedine Nabi. Kwanza kule nyuma alianza na mabeki watatu wa katikati. Hapo akawapa Yanga faida ya kuwa na walinzi wengi wanaposhambuliwa.

Katikati Nabi aliamua kucheza bila winga akiwapa nafasi viungo wake watatu. Hapo Yanga wakawa na utulivu mkubwa katikati ya uwanja wakifanikiwa kuumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa.

Kisha kule mbele aliamua kucheza na washambuliaji wawili, lengo likiwa kuwaweka matatani mabeki mawili wa katikati wa Simba, wapate kazi ya kupambana na washambuliaji wawili. Ni sababu hii ilimfanya Mayele acheze zaidi tofauti na mechi mbili za ligi.

Kipindi cha pili Simba walionekana kuutawala mchezo lakini hiyo ni kwa sababu Yanga waliamua kurudi nyuma na kulinda bao lao wakisubiri kuwashambulia Simba kwa kushtukiza.

Mtu mwingine anaweza kusema ni kwa sababu Simba walimuingiza Rally Bwalya ambaye aliifanya itembee katikati, lakini ukweli ni kwamba Yanga waliamua kupoza mchezo na kulinda bao lao moja ambalo lilitosha kuwafikisha fainali.

Mwisho kabisa nafikiri Pablo anaweza kuwa amekaribia kuufikia mlango wa ‘exit’ Simba. Bahati mbaya kwake ameichukua Simba iliyotoka kufanikiwa kwa muda mrefu. Ni rahisi kuhukumiwa kwa kile walichokifanya waliopita.

Haionekani kama Simba inaweza kunyanyuka chini ya Pablo. Hadi leo bado hajaeleweka anacheza vipi na haionekani kama akipewa wachezaji wazuri zaidi ya hawa atafanikiwa. Itakuwa bahati kubwa kwa Pablo kama ataachwa kuwa kocha wa Simba msimu ujao.

Columnist: Mwanaspoti