Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

UBISHI WA MZEE KALIUA: Picha nyingine kubwa nyuma ya mikono imara ya Manula

FOT5yAjWUAMlYm6 Picha nyingine kubwa nyuma ya mikono imara ya Manula

Thu, 24 Mar 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Simba waliteketea tena ugenini dhidi ya ASEC Mimomas kwa roho mbaya. Haishtui sana Simba kupoteza ugenini. Mara zote wanakuwa wajanja kwa Mkapa kuliko viwanja vya watu.

Sifahamu kwa nini huwa wanashindwa kutamba ugenini. Klabu nyingi Afrika hazifanyi vyema ugenini lakini Simba imekithiri kiasi. Wanazidisha unyonge kupita kiasi wanapokuwa nje ya nchi.

Bado nawapa nafasi ya kusonga mbele kwa sababu mechi ya mwisho wataimalizia Kwa Mkapa. Nina uhakika mechi ya mwisho ya Simba, langoni atasimama Aish Manula. Labda awe katika majeraha au matatizo binafsi lakini anapokuwa ‘fiti’ kwa asilimia zote, lango la Simba linakuwa salama chini ya usimamizi wake kama lilivokuwa salama kule Benin walipocheza na waivori wa ASEC Mimomas.

Achilia mbali mikwaju miwili ya penalti aliyookoa, Jumapili ilikuwa moja ya zile jioni bora kumshuhudia Manula ndani ya jezi ya Wekundu wa Msimbazi, Simba. Manula amekuwa akililinda vyema lango la Simba kwa miaka ya usoni.

Hapana! Manula amekuwa akiyalinda vyema malango ya Simba na Taifa Stars katika miaka ya usoni.

Yupo wapi kipa mwingine aliyesimama katika lango la Stars miaka ya karibuni? Mara ya mwisho alisimama mkongwe Juma Kaseja kipindi kile timu ya taifa ikinolewa na Etienne Ndayiragije. Baada ya hapo hakuna kipa mwingine aliyempa changamoto Manula.

Jumapili alikuwa mchezaji pekee wa Simba aliyetoka uwanjani akijipiga kifua ametimiza majukumu yake kwa kiasi kikubwa. Aliitoa Simba katika aibu kubwa.

Kwanza alifuta vyema mikwaju miwili ya penalti, kisha aliokoa michomo mingi hatari iliyoelekezwa katika lango lake. Pengine Simba wangeweza kufungwa mabao tano au sita na bado Manula asingelaumiwa kwa aina ya mashambulizi yaliyoelekezwa langoni kwake, lakini alisimama imara kuzuia Simba kuaibika.

Manula alikuwa katika kiwango bora sana ambacho kilipaswa kuwaumiza Simba kuliko kuwafurahisha.

Swali wanalopaswa kujiuliza ni kwa nini kipa wao alikuwa mchezaji bora wa mechi kwa upande wao?

Kwa sababu aliokoa michomo mingi. Kwa nini aliokoa michomo mingi? Kwa sabababu Simba hawakuzuia vyema.

Mwendelezo wa Simba kutokuzuia vyema katika mashindano ya kimataifa ndio kuliendelea kumpa sifa Manula.

Lakini tukiwa hapo kwenye kiwango bora cha Manula, unaweza kujiuliza nini kimeongezeka zaidi kwake?

Nakumbuka kipindi fulani Simba walikuwa wakilalamika tatizo kubwa la Manula ni kuruhusu mabao ya mbali. Kipo kipindi alipoteza namba yake kwa Deo Munishi ‘Dida’ baada ya kutunguliwa bao la mbali na kiungo wa Yanga anayesota benchi kwa sasa, Mapinduzi Balama. Kipi kimeongezeka kwa Manula?

Nafikiri tunakishuhudia kiwango bora zaidi kwa Manula kwa sababu ya uzoefu alioupata katika mashindano ya kimataifa aliyoshiriki akiwa na jezi ya Simba na timu ya taifa kwa miaka ya karibuni.

Manula anakumbana na changamoto ya kuokoa michomo mingi hatari anapokuwa katika mashindano ya kimataifa. Mara nyingi katika ligi kuu anakuwa likizo kwa sababu Simba hutawala mchezo na ‘purukushani’ kwao zinakuwa chache. Haitokei nafasi ya kipa kuimarika katika timu ambayo haikumbani na mashambulizi.

Ni kama ambavyo ilikuwa kwa kipa wa zamani wa Barcelona ya Pep Guardiola, Victor Valdes. Manula ameimarishwa na mashindano ya kimataifa kama ilivyo kwa mabeki wake wa pembeni, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala.’

Kitu pekee kinachonifikirisha mpaka sasa ni kwa nini Manula haitajiki na klabu kubwa nje ya Tanzania. Mara nyingi natazama klabu bingwa Afrika na kuwaangalia kwa makini makipa wa klabu kubwa, bado namwona Manula akiwa na nafasi katika milango ya baadhi ya timu kubwa Afrika.

Uzuri wa kipa hauhitaji mambo mengi kutambua uzuri wake. Unatazama tu jinsi anavyopanga ukuta wake na yeye anavojipanga golini kwake kisha jinsi anavyookoa michomo, unajua kabisa huyu ni kipa imara. Pengine Manula anastahili kucheza klabu kubwa zaidi ya Simba.

Sikiliza tetesi za wachezaji wanaohitajika nje miaka yote, huwezi kusikia jina la Manula. Kwa nini? Haonekani? Au wamesimamizi wake wameshindwa kumuuza? Bado sina jibu sahihi.

Kitu pekee kinachomwangusha ni umbo lake. Ni kipa mrefu asiyejaa vizuri golini. Kama tulivyo watanzania wote, Manula anaingia katika kundi la makipa wasio na miili mipana. Ni mrefu lakini hajatanuka vizuri.

Ni kama ambavyo wachezaji na Watanzania wengi hatujai vyema misuli hata tunapokuwa watu wazima. Tatizo huwa ni nini? Asili au lishe? Niandikie jibu kupitia namba iliyopo hapo juu. Advertisement

Columnist: Mwanaspoti