Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuzo za EJAT zichangamkiwe

2083612 EJAT.png Tuzo za EJAT zichangamkiwe

Thu, 1 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMATATU iliyopita Baraza la Habari Tanzania (MCT) lilitoa Tuzo za Umahiri wa Waandishi wa Habari Tanzania (EJAT). Hizi ni tuzo zinazotambua umahiri wa kazi za waandishi wa habari nchini.

EJAT inashirikisha waandishi wa habari za magazeti, luninga na redio ambapo washiriki wanapaswa kutuma kazi zao za habari tatu kwa kila kipengele.

Kazi za Habari zinazoshindanishwa ni zinazohusu masuala kadhaa kama vile uandishi wa habari za watoto, jinsi, afya, uchumi, sanaa na michezo, ubunifu, utalii, kilimo, mazingira, hedhi salama, afya ya uzazi na nyinginezo nyingi.

Hivyo, hizi ni tuzo ambazo hakika zinawatambua waandishi wa habari walioandika habari nyingi kuhusu masuala hayo mtambuka yaliyoelezwa.

Ni wazi kuwa wapo wanahabari wengi wameyafanyia kazi matukio yanayoendana na masuala kama hayo, lakini hawawasilishi kazi zao kwenye Shindano la EJAT.

Hapa ndiyo maana ninawasihi waandishi wa habari kuzichangamkia Tuzo za EJAT, kwa kuwa licha ya kuwa zitawafanya kutambulika zaidi, lakini pia zinaiongeza thamani fani ya habari.

Binafsi nimeshiriki katika shindano hilo mwaka huu, lakini nilishangaa kusikia kuwa kuna vipengele ambavyo havikuwa na washiriki kabisa.

Kutokuwepo kwa washiriki katika vipengele hivyo, kuna maana nyingi, ambapo kwanza inaweza kuwa waandishi waliwasilisha kazi zisizokuwa na ubora na hivyo hata majaji hawakuziingiza kwenye shindano au hawakuwasilisha kabisa kazi zozote.

Vipengele vilivyokosa washiriki ni Kipengele cha Picha Bora ya Mwaka na Habari ya Michezo Bora ya Mwaka, vyote kwa upande wa magazeti.

Ninapenda kuwasihi waandishi wote kwa ujumla, kutambua kuwa kwa kuwasilisha kazi za habari zenye sifa stahiki ni kitu muhimu katika ushindi wa tuzo hizo.

Ifahamike kuwa suala sio kuwasilisha tu kazi za habari, ila kuna haja ya kuwa na maandalizi ili kazi inayokuja kuwasilishwa iwe bora na yenye mashiko.

Kwa mujibu wa jaji mmoja wa shindano hilo, Pili Mtambalike, zipo kazi za habari zilizopokelewa na jopo hilo, ambazo zilikosa umakini.

Ukosefu wa umakini huo, upo ulioanzia katika hatua ya kuandaa kazi husika na zipo zilizokuwa hazina vyanzo stahiki vya habari, hazikuwa na ubunifu, uhariri mzuri na kushindwa kukidhi mahitaji.

Hii ni baadhi ya mifano ambayo hakika itufanye wanahabari kuongeza umakini zaidi katika ushiriki wa tuzo hizo. Lakini, pia niwasihi waandishi wa habari za michezo na wapicha picha za magazeti, kuhakikisha kuwa kazi zao zinashirikishwa kwenye mashindano yajayo, yaani kwa maana ya wajipange.

Wito huo pia uende hadi kwa wamiliki wa vyombo vya habari, ambapo nawasihi washiriki kikamilifu kuwaandaa waandishi wao kuandaa habari zenye umahiri wa kushindanishwa.

Simaanishi kuwa habari wanazopaswa kuzipa kipaumbele ni zile kwa ajili ya ushiriki wa tuzo tu, bali nashauri kuwe na habari za kimkakati kwa ajili ya kushiriki kwenye shindano hilo.

Kwa mfano kama kuna habari inayofaa kuandikwa kwenye magazeti au kutangazwa kwenye luninga na redio lakini ipo mikoa mingine, wamiliki wanaweza kuwawezesha waandishi wao wakaziandike ili zije kushindanishwa.

Columnist: habarileo.co.tz