Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuzike siasa za ‘majitaka’

A9d33dcae262bc3c13fa32c7180defee Tuzike siasa za ‘majitaka’

Wed, 28 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

HIVI karibuni wakati akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema anatarajia kukutana na viongozi wa vyama vya siasa nchini ili kuona namna ya kustawisha demokrasia nchini.

Katika hotuba hiyo, Rais alihamasisha wabunge kuikosoa serikali bila woga inapokwenda vibaya, lakini akasema, ukosoaji huo uwe wa busara na wenye lugha ya staha yaani isiyotia maudhi wala kudhalilisha wanaokosolewa wakiwamo viongozi.

Aidha, wakati akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini, Mbunge wa Bunda Vijijini, Mwita Getere, alitoa mfano wa nchi ya Marekani akisema huko kuna vyama vikubwa viwili vya Democratic na Republican.

“Wakati wa uchaguzi, kila chama kinakwenda na ilani yake kuinadi kwa wananchi na kinaposhinda kimoja, kingine kinafunika ilani yake na kuingia katika utekelezaji wa ilani ya chama kilichoshinda huku kikisubiri uchaguzi mwingine baada ya miaka minne,” akasema Getere.

Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema taifa hilo kubwa duniani baada ya ushindi wa chama kimoja, wafuasi na viongozi wa chama kilichoshinda, chama kilichoshindwa na wananchi kwa jumla, hushirikiana na chama nshindi kutekeleza ilani huku wakilinda utaifa wao; wanakuwa ndugu moja kwelikweli.

Mwingine anasema wakati wote wanaungana kutekeleza ilani ya chama mshindi huku pia wakiboresha ilani yao, wote wanakuwa kitu kimoja kuilinda na kuijenga nchi yao; hakuna na hawaruhusu ‘mchwa yeyote kula mbao za nyumba yao’ kupitia usaliti, uhujumu na ukibaraka.

Kimsingi, huo ndio uzalendo wa kweli kwamba, hata baada ya uchaguzi, hakuna kinyongo, masengenyo wala umbea dhidi ya taifa lako na hakuna anayeleta chuki za kidini, kikabila, kimajimbo wala kisiasa; wote wanajenga taifa lao.

Hali hiyo ni tofauti na siasa za nchini kwa baadhi ya vyama na hasa, vyama vya upinzani ambavyo kwao uchaguzi huru, haki na wenye usawa au nchi kuwa na demokrasia ya kweli, ni pale watakaposhinda wao, vinginevyo inakuwa nongwa na kununa na hata wengine ‘kuhamia kwa jirani.’

Kwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani nchini, siasa zao tangu mawio hadi machweo ni uchaguzi, kazi yao ni kuendesha siasa za matusi, maandamano, usengenyi, uzushi, kukataa matokeo na kutafuta huruma kwa watu ndani na nje ya nchi. Hii ni aibu; ni siasa za ‘majitaka’.

Ni kwa mtindo huo, ni kama vile mtu anasema akila nyama inamdhuru, lakini anakunywa supu maana wengine hata wanakosoa ujenzi na ununuzi wa miundombinu ya usafiri kama ndege, nao wanazipanda na kuzitumia kwa usafiri.

Wanakosea kusema serikali inajikita katika maendeleo ya vitu na kusahau watu. Hao, wanashindwa kujua kuwa, hakuna maendeleo ya watu kama hakuna maendeleo ya vitu.

Watu wanatafuta umaarufu kupitia mambo ya hovyo kama matusi kwa viongozi bila aibu na wengine kutaka kuwawekea masharti viongozi na taifa kwa jumla kama kwamba wao ndio taifa; ajabu kweli.

Wanasema wanatetea demokrasia, lakini wanatumia ‘domoghasia’ kuitafuta huku wakiwa na ajenda za siri mifukoni; wanapigania demokrasia nje ya vyama vyao, lakini ndani ya vyama vyao ndio wanaoibemenda maana hawataki kupisha wengine katika uongozi, hawataki kukosolewa na wanafanya vyama kama kampuni binafsi.

Azma ya Rais Samia kukutana na viongozi wa vyama, iwe fursa ya viongozi hao kusafisha siasa zao ili zitoke katika mfumo wa majitaka na kuwa katika mfumo wa siasa za majisafi na salama zenye uongozi bora.

Vyama vya siasa vitumie fursa na uungwana wa Rais Samia kujijenga na kunenepesha demokrasia kwa kujisafisha vyenyewe kwa ndani kabla ya kutazama usafi wa nje ya glasi.

Vyama visipojifunza ushauri wa Rais wa kukosoa kiungwana, kwa staha na kwa nidhamu, vijilaumu vyenyewe kwa kuona kila kukicha Watanzania ‘wanavitema mate’ kisha vinafuata mkumbo wa mbaazi kukosa maua akasingizia jua hata kama kulikuwa na masika vinginevyo, vitazidi kujimemenda katika kila uchaguzi.

Vijue kuwa, Watanzania sasa wamefumbuka macho; wanaona na hawaendeshwi kwa siasa za mihemuko, bali siasa wanazoona zina tija kwa maisha yao na maendeleo ya taifa kwa jumla.

Kutolikulijua au kutolizingatia hilo, ndiko kulivifanya vyama vya upinzani hata vinavyojidhani ni bora kuliko vingine, vikaangukia pua kwa anguko la aibu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hali iliyovifanya vifunike nyuso kwa viganja vya mikono kuficha aibu mbele ya wafadhili.

Hii ni kwa kuwa vipo vilivyojidanganya na kujiamini kutokana na umati uliojitokeza kwenye mikutano ya kampeni. Havikujua kuwa msibani kila mmoja analia kwa jambo lake; kwamba hata kwenye mikutano hiyo, walikuwapo waliokwenda kushuhudia ubingwa wa matusi, lawama na uzushi wa baadhi ya wanasiasa.

Kadhalika, walikuwapo waliokwenda kuwaona watu wanaosikia wanafanya vitu vya ajabu kwa taifa lao na kubwa, walikuwapo pia waliokwenda kushangaa namna mtu anayegombea kuliongoza taifa, anavyooneshja chuki za waziwazi kwa taifa hilo ili kuwafurahisha mabeberu.

Msibani kila mmoja ana lak linalomliza.

Ndiyo maana ninasema, sasa vyama vya siasa hasa vyama vya upinzani, vifufuke kiuzalendo; vijifunze kuendesha siasa za majisafi na salama, siasa za kistaarabu zenye tija kwa taifa vinginevyo, usemi aliowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 1995 akiwa mjini Tarime kwamba vyama vya upinzani bado vichanga, viachwe vikue ili vikomae vipate uzoefu, utasizdi kusimama na kuonesha uhalisi kuwa bao uko hai.

Kwa msingi huo ninasema, kwa vile Rais Samia kwa upendo wake kwa Taifa na watu wake wote bila ubaguzi ukiwamo wa kiitikadi, ameamua kuendelea kustawisha zaidi demokrasia nchini na kutangaza azima ya kukutana na viongozi hao, waendee na ajenda au hoja zenye maslahi ya kitaifa.

Katu kisiwepo chama kitakachodhani kinastahili kubembelezwa na kuweka masharti ya hovyo kwa Rais wa Nchi maana ‘bosi hanunuwi’ na kufanya hivyo, ni sawa na kupiga ngumi ukutani kunakoumiza mkono wako mwenyewe.

Uamuzi wa Rais Samia mintarafu namna ya kukutana na viongozi hao, uachwe kwake; kama ni vyama vyote kwa pamoja, sawa; kama ni chama kimoja kimoja haya na kama ni chama kimoja kimoja kisha vyote yote, hayo aachiwe Mkuu wa Nchi mwenywe aamue utaratibu.

Kusiwe na jaribu la chama chote kutaka umaarufu kwa shinikizo la kutaka upekee katika kukutana na mkuu wa nchi.

Ninasema hivyo kwa kuwa kama ilivyo ada, kipo chama ‘Fulani’ ambacho kama kawaida, kimeanza kutaka upekee huo kama sharti la kukutana na Rais; namuomba Rais asikubali tabia ya chama hicho ianze kuchipua katika kipindi cha uongozi wake; kinataka kuanza kumjaribu. Watanzania hawataki hilo lipate nafasi.

Ndiyo maana ninasema, vyama visijaribu kumjaribu Rais kwa kufuifua siasa za maji taka, bali vichote hekima za kizalendo kwa kutanguliza siasa za majisafi zenye shukrani, utu na uzalendo kwa taifa.

Viendeshe siasa za kiungwana za kuipongeza na kusifia mambo mazuri yanayofanyika na penye dosari, vioneshe njia mbadala kwa adabu na utu na si kukimbilia maandamano, migomo, natusi, jazba, kususa na kutafuta huruma kwa mabeberu.

Vizaliwe upya ili unapotokea uchaguzi wowote, viingie katika kinyang’anyiro vikijua kuwa katika mashindano, kuna kushindwa na kushinda hivyo, lolote laweza kutokea.

Vioneshe ungwana wa kukubali na kupokea matokeo kama vimeshinda, viingie madarakani na kama vimdeshindwa, vipongeze kilichoshinda na kukipa ushirikiano kimalize kipindi chake.

Ndiyo maana ninasema, ‘Tuzike siasa za ‘majitaka’ tufufue za ‘majisafi.’

Columnist: www.habarileo.co.tz