Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuwatafakari kwa kina Sawadogo na Mudathir

Sawadogo Dsf Tuwatafakari kwa kina Sawadogo na Mudathir

Wed, 15 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba walipomsajili kiungo anayeitwa Ismael Sawadogo nilikuwa na uhakika walikuwa wanajua jambo wanalofanya. Hapa katikati kulikuwa na malalamiko mengi kwamba Simba walikuwa hawajafanya vyema katika madirisha ya usajili ya hivi karibuni.

Mwanzoni tu mwa msimu aliyekuwa kocha mpya wa Simba, Zoran Mark ambaye alikwenda na timu Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya alikuwa analalamika kwamba wachezaji wengi wapya walikuwa hawana hadhi au uwezo wa kuichezea Simba.

Hii ilikuwa nafasi nyingine kwao kujirekebisha. Niliamini alikuwa mchezaji mzuri. Sio tu kwa sababu alikuwa anatokea Burkina Faso, lakini tazama timu mbili alizopitia. Alikuwa amepitia klabu ya ENPPI ya Misri pamoja na Difaa El Jadida ya Morocco ambayo staa wetu, Simon Msuva alipita.

Hauwezi kucheza Misri na Morocco kama hauna kitu mguuni. Tatizo ni kwamba baada ya kuondoka Jadida haionekani ni wapi Sawadogo alikwenda. Inaonekana kama vile hakucheza soka tena kwa muda mrefu. Kwanini? Alikuwa ameumia au? Hatujui.

Mchezaji wa kiwango chake aliyetoka Misri kisha Morocco anashindwa walau kucheza katika timu ya Ligi Kuu ya Burkina Faso kwa ajili ya kujiweka fiti na kucheza tena nje ya nchi yake? Hapa wengi hatuna majibu kwanini hakucheza muda mrefu.

Tunachofahamu ni kwamba mchezaji anayekuja katika dirisha la katikati ya msimu anapaswa kuongeza kitu katika timu yake. Anakuja kwa ajili ya kucheza na kutia nguvu katika upungufu ambao umeonekana baada ya msimu kuanza.

Jonas Mkude anaonekana hayupo sawa. Nassor Kapama na Victor Akpan walionekana kutokuwa vizuri kucheza Simba. Hii inawaacha viungo wachache pale Simba. Viungo wanaoaminika wanabakia kuwa Sadio Kanoute na Muzamiru Yassin. Hao ni katika eneo la chini ambalo ni muhimu achilia mbali viungo washambuliaji kina Clatous Chama.

Kwa nilivyomtazama Sawadogo hawezi kuwasaidia Simba msimu huu. Ni mzito na amejikuta katika ligi iliyochangamka kuliko yeye alivyochangamka. Bado sijauona ubora wake katika maeneo yoyote yale. Sio katika kupiga pasi, kukaba wala kuunganisha timu.

Nilipomtazama Mudathir Yahya katika pambano lake la kwanza la Yanga mchuano wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Singida Big Stars nilikumbuka kitu. kwanini Simba hawakumsajili Mudathir? Walifanya makosa mawili au matatu kwa mpigo.

Mudathir ingawa hakuwa na pumzi kubwa kwa sababu na yeye kama ilivyo kwa Sawadogo alikuwa hajacheza soka la ushindani kwa muda mrefu, lakini alionekana kuwa kiungo bora zaidi uwanjani kutokana na ubora wake katika kukaba na kugawa mipira.

Ingawa wote wawili hawakuwa uwanjani kwa muda mrefu, lakini Mudathir ni bora kuliko Sawadogo na angeingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza cha Simba kuliko ilivyo kwa Sawadogo. Labda katika vipindi ambavyo wote walikuwa nje Mudathir alikuwa na mazoezi zaidi. Au labda tuseme kwamba Sawadogo alikuwa na majeraha na alituficha.

Vyovyote ilivyo, Simba kama

wangemsajili Mudathir wasingejuta kwa sababu moja kwa moja angeenda kuwa bora kuliko viungo ambao wapo nao kwa sasa. Wakati ule Mudathir na Sure Boy wamepata matatizo pale Azam ilikuwa inaonekana kama vile Mudathir angekwenda Simba na Sure Boy angekwenda Yanga. Wote wangekuwa wamepata viungo wazuri.

Matokeo yake wote wamekwenda upande mmoja. Nasikia Simba walipuuza kumsajili Mudathir. Inadaiwa kwamba kulifan-yika mazungumzo kati ya Simba na mchezaji lakini ni mabosi wa Simba walianza kumpiga chenga mchezaji na kuamini kwamba thamani yake ilikuwa ndogo sokoni.

Mbaya zaidi wakamsahau kwa zaidi ya miezi sita mpaka Yanga walipokuja kumchukua. Kwa Simba kumchukua Sawadogo ina maana kwamba kwanza hawajaimarika, lakini kwa Yanga kumchukua Mudathir inaonekana wameimarika zaidi na kitu kibaya kwa watani wao ni kwamba wameimarika katika eneo ambalo tayari walikuwa imara.

Wakati tukizungumza kuwa katika eneo la kiungo la Simba kuna Kanoute na Mzamiru, tayari eneo la kiungo la Yanga lilikuwa na Khalid Aucho, Aziz Ki, Sure Boy, Yannick Bangala, Fei Toto na Zawadi Mauya. Kwanini uruhusu wamchukue Mudathir?

Katika pambano la Yanga dhidi ya Real Bamako, Yanga walianza na Bangala, Mudathir na Aziz Ki. Juzi nilikuwa nawatazama katika pambano dhidi ya Geita alianza Mudathir tu kati yao. Huo ndio utajiri ambao wamekuwa nao kwa sasa.

Tukiachana na suala la Sawadogo, kuna jambo jingine ambalo limenifikirisha kiasi. Nilikuwa natazama pambano la Dodoma City dhidi ya Polisi Tanzania mara baada ya kumalizika pambano la Yanga na Geita pale Chamazi. Ubora wa wachezaji wetu umepunguza kwa kiasi kikubwa.

Wakati ligi inaendelea na imeshika kasi, ilikuwaje Yanga ikawaza kwenda kumchukua mchezaji ambaye alikuwa nje kwa miezi sita badala ya kutupa jicho lao kwa wachezaji mbalimbali ambao walikuwa wanaendelea kucheza katika ligi yetu?

Hii ina maana wakati Mudathir anafanya biashara zake Zanzibar bado aliendelea kuwa bora kuliko wachezaji wengi wa Ligi Kuu Bara? Kuthibitisha hilo ni kwamba amerudi uwanjani na haonekani kama hakucheza kwa muda mrefu. Au labda kwa sababu anacheza katika timu iliyo na wachezaji bora? Sielewi.

Inavyoonekana hakuna wachezaji wengi wenye ubora nje ya klabu zetu kubwa. Huwa tunazungumza tu kwamba wazawa hawapewi nafasi lakini ukweli ubora wa wachezaji wazawa umepungua tofauti na ilivyokuwa zamani.

Kwa mfano, baadhi ya wachezaji ambao wangeonekana wanafaa kucheza nafasi ile Yanga angekuwa Cleophace Mkandala wa Azam ambaye kabla ya hapo alikuwa Dodoma City na alikuwa anasifika. Lakini leo Mkandala anashindwa kupata nafasi mbele ya kina James Akaminko pale Azam.

Columnist: Mwanaspoti