Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Tuwape wanawake uongozi uchaguzi 2020

E6389ea0313b121fe766036159cab4f5 ‘Tuwape wanawake uongozi uchaguzi 2020

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TANZANIA imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya kimataifa yanayotoa haki kwa kila mtu kushiriki katika utawala wa nchi, haki za kisiasa na kiraia na mikataba mingine inayotoa miongozo ya ushiriki sawa wa kijinsia.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, wanawake ni wengi nchini kulinganisha na wanaume kwani ni asilimia 51.

Hata hivyo, ni asilimia 30 tu ya wanawake wanaoshiriki katika uongozi kwenye vyama vya siasa, serikalini, bungeni, kwenye mahakama na katika nafasi nyingine za uongozi katika jamii.

Pamoja na dhamira ya Serikali ya kufikia usawa wa kijinsia katika uongozi, yaani asilimia 50 kwa 50, hali halisi inaonesha bado wanawake wako nyuma katika nafasi za uongozi.

Mkuu wa kitengo cha wanawake katika Umoja wa Mataifa, Dk Phumzile Mlambo-Ngcuka, aliwahi kusema: “Usawa baina ya wanawake na wanaume ni ndoto ambayo bado inakwepa.”

“Ni katika mazingira hayo sisi viongozi wa dini na viongozi wa kamati ya amani tupo mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa kutekeleza kwa vitendo juu ya nafasi ya uongozi kwa mwanamke,” anasema Mwenyekiti wa Kamati za Amani Tanzania, Shehe Alhad Mussa Salum wakati wa kutoa wasilisho la kamati hiyo kwenye warsha ya viongozi wa dini na viongozi wa siasa.

Warsha hiyo iliyotoa nafasi kwa makundi hayo kujadili na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kufanya uchaguzi wa haki, kuheshimiana, amani na utulivu na pia jamii kuona namna ya kuzingatia nafasi ya mwanamke, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kiliwakutanisha viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa kujadili nafasi ya mwanamke katika uchaguzi wa 2020.

Alhad anasema ni ukweli ulio wazi kuwa wanawake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali hasa katika uwakilishi wa nafasi za uongozi kutokana na mfumo dume uliojengeka miongoni mwa jamii.

“Wengi tunashuhudia sehemu kubwa ya jamii inamwangalia mwanamke kwa dhana tofauti na wakati mwingine kumtolea hukumu na kuonekana kama kiumbe kisichoweza kuleta maendeleo katika jamii yake.

Jambo lililo ni kinyume hata na mafundisho katika vitabu vyetu vitakatifu,” anasema.

Akitoa mfano, Shehe Alhad Salum anasema maandiko ya Biblia yanashuhudia kwamba katika historia ya ukombozi nafasi ya mwanamke imeonekana jinsi alivyoshiriki katika utume na kukamilisha historia ya ukombozi wa mwanadamu.

“Kama tunavyoweza kuona mifano mbalimbali ya wanawake jasiri na wenye uthubutu kama vile, Debora, Ester, Mariamu Magdalene na wenzake na vivyo hivyo kwa upande wa Kurani tukufu nayo ina akina Khadija.”

Alhad Salum anasema zipo sababu nyingi zenye kumkwamisha mwanamke katika nafasi ya uongozi baadhi zikiwa ni mfumo dume ndani ya vyama vya siasa, nguvu ndogo ya mwanamke kiuchumi, rushwa, lugha dhalilishi, mila potofu, na wakati mwingine hii imesababisha baadhi ya wanawake washindwe kujiamini katika kukabiliana na vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia.

“Vyama vingi vya siasa vinawatumia wanawake katika shughuli za uhamasishaji katika kuongeza idadi ya wanachama na kueneza sera za chama lakini kwa asilimia kubwa havimwoni mwanamke kama ni mdau kwa ajili ya nafasi ya uongozi na kushika nafasi muhimu ya kimaamuzi.”

Anasema pamoja na changamoto hizo bado kuna wanawake ambao walipata fursa ya kuongoza, na wameongoza kwa kwa ustadi na weledi mkubwa wakati mwingine kuliko hata wanaume.

Anataka miongoni mwao kuwa ni Makamu wa Rais, Tanzania, Mama Samia Hassan Suluhu, Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, aliyekuwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya na Balozi Asha-Rose Migiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wengineo.

“Hii inadhihirisha wanawake ni watu wenye nguvu na uwezo katika uongozi hivyo wapewe nafasi kwa kuwachagua kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili, tukiamini wazi wataendeleza vita ya rushwa, ufisadi, dawa za kulevya na mengine mengi kwa ustawi wa Taifa letu ikiwamo kusimamia haki za wanyonge.

“Kamati ya Amani tunaamini wanawake wakichaguliwa katika nafasi za uongozi watakuwa na fursa ya kutunga sera na kushiriki katika vyombo vya uamuzi, hivyo basi ni wazi maendeleo na mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika Taifa letu pendwa la Tanzania yatatokea,” anaongeza.

Kuhusu dhana iliyojengeka katika jamii kuwa katika Uislamu, mwanamke hapaswi kuongozia, Alhadi Salum anasema dhana hiyo sio sahihi kwa Tanzania na kuwa inafanyakazi katika nchi ambayo utawala wake ni wa kufuata sheria za Kiisilamu.

Mkurugenzi wa Tamwa, Rose Reuben anasema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kuhimiza jamii, kuondoa mila na mitazamo potofu inayochochea ushiriki duni wa wanawake katika siasa na katika ngazi za uamuzi.

“Viongozi wa dini wanategemewa kuhubiri amani na mshikamano katika kipindi cha uchaguzi na amani hiyo itapatikana iwapo makundi yote maalumu wakiwamo watu wenye ulemavu na wanawake, watashiriki kikamilifu katika uchaguzi,” anasema.

Anasema kwa kuwa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika siasa na mikataba mbalimbali ya amani, ni muhuimu mambo kadhaa yakazingatiwa ili kuondoa vikwazo vyote vinazouia ushiriki wa wanawake katika siasa.

Mosi anasema taasisi za dini zinapaswa kutoa elimu kuhusu ushiriki wa wanawake katika siasa na kuondoa mitazamo yote potofu inayokwamisha ushiriki wao na kutoa mafundisho katika Kurani na Biblia yanayomwonesha mwanamke kama shupavu na mleta mabadiliko ili kuwajengea wanawake kujiamini.

Pili, anasema anasema Serikali na viongozi wa dini wana wajibu wa kukemea na kuwachukulia hatua wanaotoa lugha dhalilishi kwa wagombea wanawake wakati wa uchaguzi.

“Vyama vya Siasa vitambue kwamba vina wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha haki na usawa wa wanawake ndani ya vyama vyao na katika jamii kwa ujumla, kwa kuwa wanawake ndiyo kundi kubwa la wapigakura Tanzania.

“Vyama vya siasa vizingatie mchakato wa uteuzi wa wagombea kwa kuzingatia mrengo wa jinsia, kama Sheria Mpya ya Uchaguzi inavyoainisha. Ruben pia anawaasa wanahabari kutumia kalamu zao kimaadili kwa kuepuka kuchochea lugha dhalilishi na kuidunisha taswira ya mwanamke katika jamii.

Vyombo vya vya habari na wanahabari wanapaswa kupaza sauti zao kuhimiza ushiriki wa wanawake katika siasa na kulinda utu wake ili kuleta amani na ushiriki kamilifu katika uchaguzi.

Anawataka wanawake waondoe dhana chonganishi zinazoenezwa kuwa hawapendani na hawawezi bali waendelee kusimama imara na kujitokeza kwa wingi katika chaguzi.

“Tamwa tunaliombea Taifa likatawaliwe na upendo, amani na mshikamano katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 28.” Naye Mchungaji Timothy

Holela anatoa rai kwa viongozi wa dini kutumia nafasi zao kuwaandaa wanawake kuwa viongozi kwani kwa kufanya hivyo wigo wa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi utaongezeka.

“Tuanze utaratibu wa kuandaa wanawake kuwa viongozi kwenye nyumba zetu za ibada kwa kuwajengea ujasiri, kuwatia moyo na kuwapa miongozo ya kuwa viongozi bora kwa kufanya hivyo tutaongeza idadi ya wanawake na mafanikio yataonekana.

Naye Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu anasema ili kudumisha amani na utulivu ni vyema viongozi wa dini wasiwe mashabiki wa vyama vya siasa.

“Ili kudumisha amani na utulivu katika nchi yetu tusiwe mashabiki wa vyama vya siasa, kila mtu ana chama chake moyoni mwake. Kiongozi wa dini unapokuwa shabiki wa chama fulani hii ni moja ya uvunjifu wa amani.

“Tunatakiwa kujua kuwa waumini tunaowaongoza wana vyama vyao, sasa wewe kiongozi wa dini ukishabikia chama kimoja, mwingine ataacha kusali katika msikiti wako au kanisa lako na kwenda kumtafuta imamu au mchungaji wa chama chake sasa si dhani kama atampata.

Naye Mwenyekiti wa NCCRMageuzi mkoani Dodoma, Hamida Maftaha na mgombea nafasi ya udiwani kata ya Makole katika halmashauri ya Jiji la Dodoma, anasema wanawake wamekuwa na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma juhudi hizi nyuma.

“Mimi nasukuru chama changu kimeniteua na kunipa nafasi ya kuwania udiwani, lakini kuna kazi kubwa sana katika kuania nafasi hii, ikianza ya kijamii ya kuoana kama hatuwezi, na kiuchumi,” anasema.

Columnist: habarileo.co.tz