Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuukumbatie urithi aliotuachia Hayati Magufuli

9138d2f2029bbf8ef23df8bd39b0f62b Tuukumbatie urithi aliotuachia Hayati Magufuli

Mon, 29 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

ALIYEKUWA Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli ameitwa na Mwenyezi Mungu na ametuacha Watanzania tukiwa na majonzi mazito.

Hata hivyo uzuri ni kwamba, Magufuli hakutuacha mikono mitupu Watanzania, bali ametuachia urithi wa kudumu utakaokuwa na faida kubwa kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Urithi aliouacha kwa Watanzania ni wa aina mbili. Kwanza, ni urithi wa miradi mikubwa aliyoianzisha itakayomfanya akumbukwe na vizazi vijavyo.

Hii ni miradi mbalimba ikiwamo mikubwa kama Bwawa la Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha Mega Watt 2115.

Mingine ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kupitia Morogoro itakayoenda hadi Mwanza mpaka katika mataifa jirani kama Rwanda kupitia Isaka hadi Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Aidha, ipo miradi kama ya upanuzi wa viwanja vya ndege na uhuishaji wa Shirika la Ndege Tanzania kwa ununuza wa ndege 11 zikiwamo nane ambazo tayari zipo nchini.

Mingine iliyoacha alama ya kumkumbuka Magufuli ni barabara za juu kama Kijazi (Ubungo), Mfugale (Tazara) na daraja la baharini la Salenda.

Urithi wa pili ni usimamizi na ulinzi wa rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Magufuli alionesha kuwa hilo linawezekana, hivyo Watanzania tuzisimamie kwa umakini rasilimali za umma kwa maslahi ya nchi.

Hayati Magufuli ametufundisha kuchukia rushwa na ufisadi kwa vitendo, kuchukia uonevu na mateso kwa wanyonge. Hili ni funzo kubwa ambalo tunapaswa kuiga msimamo wake.

Kwa msingi huo, Watanzania tuendeleze upendo miongoni mwetu kama Magufuli alivyotupenda bila kubagua ndiyo maana alionya dhidi ya kubaguana kwa misingi ya dini, kabila wala vyama kwani maendeleo hayana chama.

Katika uhai wake, Magufuli alikuwa muwazi na mkweli hali iliyomwezesha kufanya uamuzi papo kwa papo bila kumwonea mtu.

Aidha, alitufundisha kuchukia ubadhirifu wa mali ya umma na kuchukua hatua madhubuti kuuzuia kwa kuwawajibisha na kuwatumbua hata rafiki zake walioonesha ‘sura za ubadhirifu” wa mali ya umma.

Watanzania tupige vita uzembe kazini kwa kuendeleza nidhamu katika ofisi za watumishi wa umma kama alivyofanya Magufuli.

Huu ni urithi tunaotakiwa kuulinda kwa nguvu zote vinginevyo, tunaweza kurudi tulikotoka.

Urithi mwingine tulioachiwa Watanzania ni uchapaji kazi kwa wananchi wote bila woga.

Alikuwa mfano bora katika kufanya kazi na ndiye aliyeondoa uzembe tuliokuwa nao Watanzania na kupenda vya bure bila kufanya kazi.

Hayati Magufuli ametuonesha kuwa Tanzania ni tajiri na inawezekana kupata maendeleo yake bila kutegemea mataifa ya nje.

Ameonesha na kutuaminisha ukweli kuwa Tanzani sin chi maskini na matumizi sahihi ya rasilimali za ndani yanaweza kuijenga Tanzania na kuifikisha katika malengo yake.

Kimsingi, Magufuli umeachia urithi usiofutika. Ndiyo maana ninasema: “Pumzika kwa amani JPM. Mungu akipenda tutaonana.”

Columnist: www.habarileo.co.tz