Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tusisubiri maagizo toka juu, tuandae madarasa mapema

16907c7c7430afb609386cf7560265e8 Tusisubiri maagizo toka juu, tuandae madarasa mapema

Mon, 21 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HIVI karibuni Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lilitangaza matokeo ya mitihani ya Darasa la Saba iliyofanyika mwaka huu lakini pia wiki hii, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo alitangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwakani.

Wakati akitangaza wanafunzi watakaojiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwakani, Jafo alisema jumla ya wanafunzi 759,706 sawa na asilimia 91.1 ya wanafunzi waliofaulu wakiwemo wavulana 368,174 na wasichana 391,532 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021.

Pamoja na hayo, Jafo pia alisema jumla ya wanafunzi 74,166 sawa na asilimia 8.9 wakiwemo wavulana 34,861 na wasichana 39,305 hawakupangiwa shule katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa, huku akiitaja mikoa ya Kagera, Katavi, Lindi, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Songwe na Tabora kuwa imeweza kuwapangia shule wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani.

Hoja yangu katika hilo ni kwamba inakuwaje wanafunzi 74,166 washindwe kuanza masomo kwa wakati kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa ilihali kila mkoa unajua idadi ya watahiniwa wa darasa la saba hivyo kujua mahitaji ya madarasa na miundombinu mingine na kujiandaa mapema badala ya kusubiri kukimbizana katika wakati ambao wanafunzi walipaswa kuanza masomo.

Mfano mzuri ni kwa mikoa hiyo tisa ambayo Waziri Jafo ameitaja kuwa imefanikiwa kuwapangia shule wanafunzi wote waliofaulu kwenye mikoa yao hali inayoonesha kwamba walijiandaa mapema kwa kujua mahitaji halisi ya vyumba vya madarasa kutokana na idadi ya watahiniwa waliyonayo.

Kutokana na hilo, nadhani kuna haja sasa kwa mamlaka husika ngazi ya mkoa ua manispaa au halmashauri kuona namna bora ya kuondokana na kadhia hiyo ya kusubiri dakika za mwisho za kutangazwa matokeo na ndipo zianze kukimbizana kutatua changamoto ambayo ingeweza kutatuliwa mapema.

Natambua kuwa mimi siyo mtaalamu wa saikolojia, lakini wataalamu wa saikolojia wanaweza kukubaliana nami kwamba jambo hilo linaweza kuwaathiri watoto hao kisaikolojia pale wanapoona wenzao wakianza masomo kwa wakati na wao wakitakiwa kusibiri mwezi mmoja au zaidi.

Ili kuondokana na kadhia hiyo, wito wangu ni kwa mamlaka husika kuandaa miundombinu ya vyumba vya madarasa, vyoo na miundombinu mingine inayohitajika mapema ili kuondoa usumbufu wa kisaikolojia kwa watoto hao lakini pia kuwapa fursa ya kuanza masomo yao ya sekondari kwa wakati.

Kama mikoa tisa imeweza kuwapangia shule wanafunzi wake wote, naamini hata mikoa mingine nayo inaweza kwa kuwa kila mkoa unajua mahitaji ya vyumba vya madarasa kulingana na idadi ya wanafunzi wa darasa la saba ilionao kila mwaka.

Columnist: habarileo.co.tz