Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tusingeshtuka ya Tshabalala, Kapombe tungekuwa Taifa la ovyo sana

Mohammed Hussein M15 Mlinzi wa Simba/ Taifa Stars, Mohammed Hussein

Tue, 28 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Timu ya taifa ya soka, Taifa Stars kesho itajitupa tena uwanjani kucheza mechi ya nne ya Kundi F ya michuano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023), ikiwa na matumaini makubwa baada ya kuichapa Uganda kwa bao 1-0 na kukusanya pointi nne kundini.

Sasa iko nyuma ya vinara wa kundi hilo, Algeria ambao wamefikisha pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu za kwanza.

Ushindi huo muhimu, pia ulichangiwa na mchezo mzuri ulioonyeshwa na mabeki wa pembeni, Novatus Dismas na Dickson Job, ambao walilazimika kucheza nafasi hizo kutokana na mkakati wa Kocha Adel Amrouche. Novatus ni mchezaji wa kiungo, lakini katika klabu yake nchini Ubelgiji amelazimika kucheza pembeni katika siku za karibuni, wakati Job ni beki wa kati.

Baada ya kutangazwa kikosi cha Stars ili kuikabili Uganda, wengi walihoji kuhusu kuachwa kwa baadhi ya wachezaji, lakini hasa mabeki wa pembeni wa Simba, Mohamed ‘Tshabalala’ Hussein na Shomari Kapombe, ambao viwango vyao bado ni vya juu kwenye klabu yao na hivi sasa wako kwenye michuano mikubwa ya klabu ya Afrika wakiendelea kung’ara.

Wako wachezaji wengine walioachwa kama Clement Mzize, ambaye baadhi wanasema kutokana na jinsi anavyoanza kuchipuka, ilibidi awemo hata kama hategemewi kucheza ili kuanza kupikwa kwa ajili ya baadaye, kama mastaa wengine ulimwenguni wanavyoandaliwa na nchi zao.

Pamoja na Kapombe na Tshabalala kuachwa, Stars iliibuka na ushindi huo mzuri wa ugenini kwa bao lililofungwa na Simon Msuva alimalizia krosi ya chini ya Job.

Ushindi huo umeibua tena mijadala, ‘Sasa Kapombe na Tshabalala, wangecheza wapi’, huku wengine wakisema huenda tulikuwa tunafanya vibaya katika mechi za mwanzo kutokana na uwepo wa wachezaji hao.

Sidhani kama kuna haja ya kubeza waliohoji kutoitwa kwa nyota hao wawili ambao wamekuwa wakilitumikia taifa tangu wakati wakiwa vijana wadogo na hawakuwahi kupata doa lolote la kutocheza kwa kujituma wakati wote wakibeba bendera ya taifa. Wengi wanabeza kana kwamba walioohoji hawaelewi mpira na pengine walikuwa na mambo yao.

Lakini kwa taifa ambalo lina watu makini wanaofuatilia kila hatua ya maendeleo ya mpira, kuhoji kutoitwa kwa baadhi ya wachezaji wanaoonyesha kiwango cha juu uwanjani na kisicho na shaka yoyote, hicho ni kitu cha kawaida. Kwamba ni lazima kuwepo sababu za msingi na mazingira yanayoonyesha umuhimu wao umepungua na hivyo ni wakati sasa wa kuanza kupisha wengine.

Si kawaida kwa makocha wa timu za taifa kuzungumzia sababu za kutoita baadhi ya wachezaji kwa kuwa walio nje ya kikosi ni wengi kuliko walioteuliwa, hivyo huona umuhimu zaidi wa kuzungumzia wachezaji waliowaoita kwa sababu inawezekana.

Lakini makocha wengine hulazimika kutoa maelezo ya sababu za kuwaacha nyota magwiji kwa ajili ya kujenga heshima ya timu na kuwafanya mashabiki waiunge mkono badala ya kuiona kuwa ni kikundi cha mtu au watu fulani.

Kama taifa linaona sawa kwa wachezaji wake nyota kuachwa timu ya taifa bila ya sababu au mazingira yanahalalisha, basi linakuwa taifa la ovyo sana. Kwamba lisubiri kutajiwa kikosi, halafu litulie kusubiri kitakachotokea—iwe kupoteza michezo au kushinda. Huko ni kuwa taifa la hovyo sana.

Wakati fulani msomi maarufu wa nchini Uganda, Wadada Nabudere alitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Enzi hizo baadhi ya vuguvugu za kisiasa zilianzia chuoni hapo au harakati za kudai haki zilichagizwa na Jumuiya ya UDSM.

Hivyo, hata wasomi waliofika chuoni hapo kutoa mihadhara walizungumzia sana umuhimu wa kuisimamia serikali kwa kuhoji mambo mengi na Wabudere akakomelea msumari kwa kusema ni muhimu ‘ku-criticise everything’, ili kutolewe majibu ya kutosha. Alikuwa akisisitiza taifa halifai kukaa kimya kila uamuzi fulani unapotangazwa na kusubiri matokeo yao. Wakati mwingine baadhi ya maamuzi yanakuwa maafa kwa jamii, hivyo ni lazima kuhoji na kukosoa ili yanyooshwe.

Ndivyo inavyotakiwa kuwa na ari hiyo kwa sababu kuhoji na kukosoa si kupinga, bali kuonyesha kushtushwa na uamuzi fulani na hofu uamuzi huo unaweza kuwa majanga kwa taifa.

Ungetegemea Shirikisho la Soka (TFF) limshauri Amrouche aongee na vyombo vya habari kutoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya timu ya taifa kuelekea mchezo huo ili kuweka sawa fikra za Watanzania wote. Unaweza kutegemea matokeo ndio yatoe majibu, lakini pale matokeo yanaposhindwa kutoa majibu, ni vigumu sana kuinuka na kuanza kutoa ufafanuzi wa ambayo yangeweza kuelezwa kabla ya madhara.

Siku zote makocha wa timu za taifa huwajibika kwa wananchi au mashabiki na si viongozi wa vyama pamoja na ukweli kinadharia ndio waajiri wao.

Mashabiki wasipokuwa na maelezo ya kutosha kuhusu timu yao ya taifa, uungaji wao mkono hauwi mkamilifu na unakuwa wa kusubiri matokeo. Lakini wakiwa na maelezo ya kutosha, matokeo si kitu kibaya sana labda yawe mabaya kwa muda mrefu.

Ni lazima tujenge huu utamaduni wa kuwaweka mbele mashabiki katika kila kitu ili waiunge mkono timu. Pengine kujitokeza kwa watu wachache viwanjani wakati timu ya taifa inacheza kunatokana na mashabiki kujiona si sehemu ya timu ya taifa ndio maana tunalazimika kutumia nguvu nyingi kushawishi watu wajazane viwanjani kumbe kulihitajika akili kidogo tu.

Nimeeleza hayo yote kutaka kuonyesha kulikuwa na kila sababu ya baadhi ya wananchi kuhoji uteuzi wa baadhi ya wachezaji na kuachwa kwa nyota ambao wamekuwa na timu kwa muda mrefu, hawajaanza kuchuja na hawajawahi kuwa na dosari yoyote katika kipindi wameitumikia timu ya taifa.

Kuhoji pia kunawafanya waone kumbe taifa linawathamini na kuwafanya walio walio katika timu kuona haja ya kucheza kwa bidii ili mashabiki wawaunge mkono.

Ni taifa la ovyo pekee linaloweza kukaa kimya pale nyota wake magwiji wanapoachwa katika mazingira ambayo hayahalalishwi na chochote.

Columnist: Mwanaspoti