Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tusijikite kwenye majina umakamu wa rais, bali sifa

FLAG TANZANIA Tusijikite kwenye majina umakamu wa rais, bali sifa

Thu, 25 Mar 2021 Chanzo: ippmedia.com

Nafasi hiyo iko wazi, baada ya Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa anaishikilia kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inaweka wazi kwamba baada ya Makamu wa Rais kuapa kuwa rais baada ya rais kuondoka madarakani kwa njia ya kifo kama ilivyotokea kwa Hayati Dk. Magufuli, anatakiwa kuteua jina la makamu wa rais baada ya kushauriana na chama chake kisha kulipeleka bungeni kuthibitishwa na Bunge.

Mjadala wa nani atakuwa makamu wa rais ni sahihi kabisa kuwapo hivi sasa kutokana na umuhimu wa nafasi yake katika uongozi wa kitaifa.

Hata hivyo, haitoshi kwa kutajataja tu majina ya watu wa kushika nafasi hiyo bila kutaja sifa zinazotakiwa. Makamu wa rais ndiye mshauri na msaidizi mkuu wa rais. Pale rais anapokuwa na shughuli nyingi, nyingine humtuma makamu wake kuzifanya au kumwakilisha.

Tukio la kifo cha ghafla cha Dk. Magufuli limekuwa fundisho kwetu na litapaswa kuendelea hivyo kwa vizazi vijavyo. Tunasema hivyo kwa kuwa kama katiba yetu ingekuwa kimya kuhusiana na rais anapofariki dunia, basi hali hiyo ingeweza kuzua mkanganyiko.

Kuhusiana jambo hili, hatunabudi kumkumbuka Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyependekeza kuanzishwa kwa utaratibu wa kuwapo mgombea mwenza (Runing-mate) mwanzoni mwa miaka ya tisini, ambao ulianza kutumika kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Utaratibu huu ambao mgombea urais na mgombea mwenza wanaomba kura pamoja wakati wa kampeni ulianzia Marekani na mataifa mengine kuiga huko, na hakika unaweka mazingira mazuri pale inapotokea rais akaondoka madarakani ghafla, hivyo kuepusha migogoro na migongano ya kugombea madaraka.

Umuhimu wa nafasi ya makamu wa rais pengine ndio maana umezua mjadala huo, huku baadhi ya wanasiasa wanatajwatajwa kuteuliwa. Hata hivyo, jambo la msingi katika mjadala huo linapaswa kuwa ni sifa za mtu sahihi wa kuwa msaidizi na mshauri mkuu wa Rais Samia.

Jambo la kwanza ni kuangalia majukumu ya msingi ya kitaifa yanayomkabili Rais Samia kisha sifa za mtu anayeweza kumsaidia kwa maslahi ya taifa na sio yake binafsi na makundi au mitandao ya marafiki zake.

Mambo mengi tumeshayaeleza ambayo ni aliyoshaanzisha Hayati Dk. Magufuli na mengine ameyaacha kabla ya kuyakamilisha. Kwa maana hiyo Rais Samia anasubiriwa ayaendeleze na kukamilisha mengine hususan miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa kutaja baadhi ya sifa za mtu sahihi kuwa makamu wa rais ni uadilifu, utiifu, kuchukia rushwa, kushehimu haki za binadamu, demokrasia, na utawala bora, mchapa kazi, mzalendo wa kweli, mbunifu, mwenye rekodi nzuri katika utendaji, mkomavu, mtulivu, anayeheshimika sana katika jamii, asiye na ubaguzi wa dini, rangi, itikadi za kisiasa nakadhalika.

Pia tunahitaji makamu wa rais ambaye atamsaidia Rais Samia kutatua kero za wanyonge, kusimamia ukuaji wa uchumi, nidhamu ya utendaji na uwajibikaji serikalini, anayeweza kumsaidia kurejesha uhusiano mzuri na jumuiya ya kimataifa na asiye na matamanio ya kuunda mitandao kwa ajili ya kusaka uongozi wa juu wa nchi.

Tunaamini kwamba Rais samia ambaye ndiye mwenye jukumu la kumteua atazizingatia sifa hizi, ili aweze kukidhi matarajio ya Watanzania baada ya kuondoka kwa Magufuli, ambaye ameacha alama katika uchapaji kazi.

Columnist: ippmedia.com