Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tusichezee uteuzi tuibue wawajibikaji

UCHAGaUZ Tusichezee uteuzi tuibue wawajibikaji

Thu, 16 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MINONG’ONO kuwa ni nani atakuwa mgombea wa urais Bara na Zanzibar imekwisha sasa na kinachoendelea ni kukamilisha uteuzi wa wagombea wa udiwani na ubunge kutoka vyama vilivyosajiliwa vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu ili kuanza mchakato wa kampeni.

Kinachotazamiwa kuanzia sasa ni kuona majina ya viongozi watarajiwa waadilifu na wawajibikaji wakiteuliwa na vyama vyao kugombea ubunge na udiwani ili kufanya kazi si za chama wala matamanio yao bali za kusaidia kuleta maendeleo kwa vijana, wazee, kinamama na wanyonge ili Tanzania isonge mbele.

Tunaona kuwa kazi aliyoifanya Rais John Magufuli kwa miaka mitano inaonyesha kuwa Watanzania wanatarajia kuona mabadiliko siyo kubabaisha, iwe miradi ya maendeleo, utendaji na kwa ujumla kufanyakazi kwa ajili ya wanyonge.

Tunaamini wapigakura wana hamu ya kuona wawakilishi wao na wabunge ambao wataunda baraza la mawaziri lenye mawaziri wanaoshughulikia matatizo ya watu na wanaojibu hoja za wananchi ambao tangu mwanzo wameonyesha nia ya kuona ukweli wa msimamo wa ‘Magufuli for Changes’ ambayo imeifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati.

Wapigakura wamechoka kuona magari ya bei mbaya au mashangingi ama V8 ambayo viti vyake vimefunikwa na vitambaa vyeupe yakiwabeba wabunge wao ambao hawasaidii kubadili maisha yao wala hawawatembelei kujua dhahama zao badala yake wanakuja kipindi hiki cha uchaguzi..

Tuna imani kuwa watakaoteuliwa ni wale watakaoishauri serikali namna bora ya kutatua matatizo ya ukosefu wa ajira, huduma bora za kijamii, lishebora na mengine yanayowakwamisha kuondokana na umaskini.

Wapiga kura wanatarajia kupata wabunge na madiwani watakaoishauri serikali na halmashauri zao namna bora ya kuhakikisha kuwa wamachinga wanaosota kwenye miji mbalimbali wakiuza bidhaa kandokando au ndani ya barabara kuu wanapata viwanja vya kufanyia biashara zao vyenye usalama na miundombinu bora.

Aidha, wanatarajiwa wabunge na madiwani wanaofikiria kuandaa na kushauri serikali na halmshauri mikakati na mbinu za kuboresha maisha ya wananchi, kuondoa uchafu mitaani na kuhakikisha watu hawafi kwa mafuriko kisa wanaishi mabondeni.

Vijijini wanawake wanatarajia kumalizika kero ya kupeleka ndoo za maji, mafuta ya taa ili kuwashia taa na kuni za kujipikia vyakula hasa wajawazito wenye uhitaji wa wataalaumu wanaolazimika kukaa hospitalinni.

Licha ya serikali kugharamia elimu bado mabinti hawasomi wanapata mimba, kuolewa utotoni na changamoto kubwa ni kuendeleza mila na desturi zinazowaumiza wanawake na watoto.

Viongozi watarajiwa wanatarajiwa kuisaidia serikali kuondokana na changamoto hizo na kuweka mazingira sawa ya kijinsia ili kila raia awe na haki ya kupata na kufurahia maisha bora.

Tunaamini viongozi wanaotarajiwa kuchaguliwa wanategemewa kuwa waadilifu na wanaoendana na kasi ya ‘hapa kazi tu’ na kuhudumia wananchi.

Ni wale walio mstari wa mbele kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na kuondoa usumbufu kwa wananchi ili kuzifikisha huduma za kijamii na kupunguza malalamiko ya raia waliowachagua pamoja na umaskini.

Tunaona kuwa awamu hii matatizo ya wananchi yamepunguzwa kwa mfano ukiingia hospitali za umma nyingi zinaelezwa kuwa zina dawa na kinachosisitizwa sasa ni wananchi kuwa na bima ya afya ili kujigharamia matibabu.

Tunahimiza kuwa madiwani na wabunge watarajiwa wanatakiwa wawajibike wawe wasikivu na wanaofuatilia matatizo ya wananchi kama mashine hospitalini mfano x-ray, ultrasound na uwapo wa huduma muhimu kwa umma.

Baraza la mawaziri linalokuja linategemewa kuwajibika siyo la wabishi ambao hata kama wamekosea wanasubiri hadi kuondolewa madarakani na mamlaka za uteuzi .

Columnist: www.tanzaniaweb.live