Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tusherehekee Eid -El -Fitri kwa umakini

014b82857baeb91822ef71817480f472.jpeg Tusherehekee Eid -El -Fitri kwa umakini

Wed, 12 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KESHO Alhamisi au keshokutwa Ijumaa, Waislamu nchini wataungana na wezao duniani kuadhimisha Sikukuu ya Eid El Fitri baada ya kukamilisha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Radhamani ambao ni moja ya nguzo kuu tano za Uislamu.

Kwanza, ninawapongeza Waislamu wote waliofunga kwa uaminifu na kuendesha toba makini katika kipindi hiki cha mfungo.

Ninawapongeza nikisema, neema walizopata katika kipindi hiki, waziendeleze hata baada ya mfungo kwa kutenda mema kama dini inavyosisitiza.

Kadhalika, ninawapongeza huku nikihimiza umuhimu wa kila mmoja ama awe Mwislamu, au si Mwislamu kwamba, ipo haja kubwa kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki ama za usalama wa kiafya, kimaadili, kijamii na hata kuhusu usalama barabara

ili sikukuu inapoisha, iache watu wakiwa salama wakiendelea kumcha Mwenyezi Mungu.

Ninasema hivyo kwa kuwa jana katika masoko kadhaa mkoani Dar es Salaam, nimeshuhudia watu wanavyozidi kuongezeka katika maeneo ya manunuzi ya bidhaa mbalimbali zikiwamo za chakula na mavazi kwa ajili ya sikukuu.

Katika maeneo mengi yenye masoko na maduka mengi (mijini) kama Kariakoo, Manzese na Tandika, msongamano wa watu ulikuwa unaongezeka kadiri siku na saa zinavyozidi kuisogelea sikukuu hii.

Kimsingi katika zama hizi ambazo kuna maradhi mengi yakiwamo yanayoenezwa kwa njia ya hewa, si jambo jema watu kuacha kufanya manunuzi yao mapema ya sikukuu, eti wakasubiri ‘kukanyagana’ siku za mwisho wakiwa na watoto.

Hii imekuwa kasumba inayoendelea hata katika sikukuu nyingine za Pasaka na Krismasi.

Kimsingi, hii ni kukaribisha misongamano isiyo ya lazima na ndio maana ninasema, hata itakapofika sikukuu yenyewe, ni vyema waumini wa dini husika kujitokeza katika nyumba na maeneo yao ya ibada kama ilivyo ada, lakini baada ya hapo, waendeleze umakini kama waliokuwa nao katika swala.

Viongozi wa dini, serikali, jamii na familia washirikiane kuhakikisha hata katika maeneo ya burudani na starehe, watu wanasherehekea sikukuu hii muhimu kwa imani, amani na umakini mkubwa ili izidi kuwa na tija.

Katika kumbi za strehe kwa mfano, watoto walindwe na kuepushwa dhidi ya misongamano inayowapotezea umakini na kuhatarisha maisha yao kama ilivyowahi kutokea.

Ikumbukwe kuwa popote duniani, yanapotokea matukio ya msongamano, watoto, wagonjwa na wazee huathirika zaidi hivyo, tahadhari za kutosha hazina budi kuchukuliwa kuwalinda wao na jamii nzima.

Hili ninasema, linahusu hata ulinzi wa maisha na mali nyumbani, barabarani na katika maeneo ya ibada na burudani.

Tuache kasumba ya kuwaacha watoto wenyewe kuzurura barabarani bila uangalizi au uongozi makini.

Kila mmoja atambue jukumu kubwa alilo nalo kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya madhara yanayoweza kutokea yakiwamo ya kiafya kupitia maambukizi ya magonjwa.

Kila mmoja awe mlinzi na balozi wa kuzuia ajali za barabarani, nyumbani na mahali pa kazi.

Jamii ishirikiane kukataa na kuzuia aina zote za uhalifu kutendeka.

Columnist: www.habarileo.co.tz