Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tuseme basi kwa ajali za barabarani 2021

B367291697f49d36cfe6eb083c8abc31 Tuseme basi kwa ajali za barabarani 2021

Sat, 9 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

AJALI za barabarani zimekukuwa tishio nchini na duniani kote licha ya jitihada kadha wa kadha zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha ajali za hizo zinakoma. Watu wanapoteza maisha kila kukicha na wengine kubaki na majeraha au ulemavu wa maisha kutokana na ajali za barabarani.

Hali hii huleta huzuni, mateso na mzigo kwa familia zao, ndugu na marafiki. Baadhi ya ajali hukatisha maisha ya watu hasa wanaume ambao ndio tegemezi kubwa katika familia nyingi kutokana na wengi wao kutoka majumbani kwenda kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akito masimulizi yake hivi karibuni, mmoja wa waathirika wa ajali za barabarani, Joel Kamugisha aliyekuwa akiendesha daladala linalofanya safari zake kati ya Mbagala na Kawe, anasema alipata ajali mwaka 2016 maeneo ya Kawe.

Anasema basi alilokuwa anaendesha lilileta hitilafu hivyo akaingia chini kuchunguza hitilafu hiyo huku akimuelekeza kondakta la kufanya lakini kondokta hiyo akawasha gari bila mpangilio.

Kamugisha anafafanua kwamba gari lilitembea huku yeye akiwa uvunguni kwa kuwa kondokta aliliwashia katika gia.

“Gari lilikanyaga mguu wangu wa kushoto na kusababisha kukatwa,” anasema.

Anasema alihangaika sana na matibabu na sasa sehemu kubwa amekuwa tegemezi ingawa anauza kioski cha biashara ndogo ndogo ili kujikimu.

“Naomba serikali iweke utaratibu wa watumishi wa magari kuwa na bima itakayowalinda ili iweze kuwasaidia katika kupata matibabu pindi wanapopata ajali,” anasema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Watu Walioumia Uti wa Mgongo ambaye ni mmoja wa waathirika wa ajali, Abdulazizi Shambe, anasimulia kwamba alipata ajali kutokana na tairi kupasuka ghafla huku gari likiwa katika mwendo mkali.

Anasema baada ya hali hiyo kutokea dereva aliyekuwa akimwendesha alishindwa kudhibiti gari.

Anasema gari lao lilipinduka mara tatu lakini ‘huduma ya kwanza’ waliyoipata katika eneo la ajali ilikuwa ni kuibiwa vitu walivyokuwa navyo! Anasema alipata ajali hiyo akitoka kusomea ukocha na hivyo, siyo tu kwamba imemfanya mlemavu wa kudumu, bali pia tegemezi kwa kushindwa kufanya kazi aliyosomea.

Anasema alianza kuonja machungu ya ajali hiyo akiwa hospitali alikolazwa kwa muda mrefu baada ya ndugu zake kumtelekeza.

Shambe anasema ni muhimu elimu iendele kutolewa kwa wingi zaidi katika jamii kuhusu namna ya kujikinga na ajali za barabarani.

Anashauri elimu hiyo itolewe pia katika maeneo ya vyuoni ambapo wanafunzi wengi wamekuwa wakimaliza masomo yao huku wengine wakitegemea kununua magari.

Pia anasema kuna haja serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia waliopata ulemavu kutokana na ajali kupitia fedha za Mfuko wa Barabara.

“Huu mfuko unatengeneza barabara na sisi tunavyokwenda vituo vya mafuta tunakatwa fedha kwa ajili ya mfuko wa barabara.

Je, wanatusaidia vipi waathirika wa ajali za barabarani?” Shambe anahoji. Anasema nchi nyingine huwa zinasaidia waathirika wa ajali, hivyo serikali iangalie uwezekano wa kusaidia hata kupatiwa matibabu bila malipo.

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA), Dk Baghayo Saqware, alinukuliwa hivi karibuni akusema: “Biashara ya bima duniani kote imeanzishwa ili kulinda na kukinga wananchi na mali zao dhidi ya majanga, hivyo ni wajibu wa mamlaka kuwakumbusha na kushirikiana na makampuni iliyosajili kuhakikisha wananchi wanafidiwa dhidi ya majanga.

” Anasema mamlaka imewapa uwezo wananchi kuamua juu ya usalama wa maisha yao kipindi wakiwa safirini kwa kuhakiki bima za vyombo vya moto wanavyovitumia; hivyo kurahisisha utoaji wa fidia majanga yanapotokea.

Kwa upande wake, Msuluhishi wa Migogoro ya Bima nchini, Jaji Mstaafu Vincent Lyimo amewaasa wananchini wanaotumia vyombo vya usafiri wa umma kuhakikisha kuwa majina yao yanaandikwa katika orodha ya abiria walio katika basi husika (passengers’ manifest).

“Ulipwaji wa fidia za bima hutegemea sana orodha ya majina ya abiria waliokuwa kwenye chombo husika kipindi kinapopata ajali hivyo ni wajibu wa vyombo vya usalama na abiria kwa ujumla kuhakikisha hilo linafanyika,” anasema Jaji Lyimo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), maisha ya watu milioni tano yalitazamiwa kuokolewa katika muongo wa “Hatua maridhawa kwa ajili ya usalama barabarani kwa 2011-2020”.

Lengo la hatua hiyo ilikuwa ni kupunguza kwa asilimia 50 majeruhi na vifo vitokanavyo na ajali za barabarani kuanzia 2011 hadi mwaka uliokwisha wa 2020.

Hatua hiyo ililenga pia kutekeleza juhudi za kutimiza malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s), hususani lengo la afya namba 3.6. WHO inatoa takwimu zinaonyesha kwamba takribani watu 3,400 hupoteza maisha kila siku kutokana na ajali za barabarani duniani kote.

Utafiti wa WHO unaonyesha kuwa asilimia 40-50 ya madereva huendesha kwa kasi zaidi ya kipimo kinachonatakiwa, hali ambayo husababisha ajali moja kati ya tatu zinazotokea barabarani kila siku. Kuna athari nyingi zinazosababishwa na ajali ikiwemo vifo vya ghafla ambavyo huacha kovu la milele kwa familia pamoja na ulemavu wa kudumu ambao huongeza idadi ya mamilioni ya tegemezi kwa njia moja au nyingine.

Mtu alikuwa anatafuta mwenyewe mahitaji yake mara baada ya ajali anageuka kuwa tegemezi. Aidha katika muongo wa pili wa kuleta usalama zaidi barabarani (Second Decade of Action for Road Safety 2021/2030), lengo kuu ni pamoja na kupunguza vifo na majeruhi wa ajali za barabarani angalau kwa asilimia 50 katika kipindi hicho cha kuanzia 2021 hadi 2030.

Halikadhalika nchi wanachama zinahimizwa kuendelea kuchukua hatua hadi mwaka 2030 juu ya malengo yote yanayohusiana na masuala ya usalama barabarani na kuhakikisha yanaenda sambamba na malengo ya Maendeleo Endelevu, hususani lengo la 3.6 Kama ilivyokwisha dokezwa utegemezi ni moja madhila makubwa wanayokumbana nayo waathirika wa ajali.

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) ni miongoni mwa wadau ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wadau wote wa usalama barabarani wanapigia debe maboresho ya sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973.

Sheria hiyo imekuwa na mapungufu mbalimbali likiwemo suala la uvaaji wa kofia ngumu, uvaaji wa mikanda kwa abiria na uwekaji wa vizuizi vya watoto ndani ya gari.

Sheria pia umekuwa na upungufu katika eneo la mwendokasi pamoja na kiwango cha utumiaji wa kilevi (pombe).

Tamwa imekuwa ikitoa mafunzo kwa wanahabari ili kuzidi kuwajengea uwelewa juu ya uandikaji wa habari za usalama barabarani kwa lengo la kupunguza matukio ya ajali ambayo mbali na kusababisha vifo na majeruhi pia yanaharibu mali (vyombo vya moto) na hivyo kuchangia katika umaskini.

Tukiwa tayari tumeingia 2021, ni muhimu kuhakikisha mwaka huu umakini unaongezeka kwa madereva ili kupunguza kama siyo kumaliza kabisa ajali za barabarani.

Ikimbukwe kwamba ajali hizi haziui au kusababisha majeraha kea abiria pekee bali pia madereva. Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2019, takribani madereva 280 walijeruhiwa katika ajali za barabarani huku vifo vikiwa 153.

Hata hivyo, idadi ya kundi hilo la madereva waliopata ajali lilipungua kiasi kwani ni madereva 133 waliojeruhiwa huku waliofariki wakiwa104 kuanzia mwezi Januari hadi Agosti mwaka 2020.

Katika kundi la abiria kipindi cha mwaka 2019, takribani abiria 469 walifariki dunia kutokana na ajali za barabarani na waliojeruhiwa wakiwa 1,608.

Lakini kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti mwaka 2020 takwimu za polisi zinaonyesha kuwa abiria waliofariki dunia walikuwa 912 na majeruhi wakiwa 320.

Kwa madereva wa pikipiki takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2019 takribani madereva 309 walifariki dunia na waliojeruhiwa walikuwa 437, huku kwa kipindi kama hicho (Januari - Agosti, 2020) waliofariki dunia walikuwa 165 huku waliojeruhia wakiwa 221.

Kuhusu takwimu za waendesha baskeli miguu miwili na zile za miguu mitatu, taarifa ya polisi inasema waliofariki dunia walikuwa takribani waendesha maguta 17 huku majeruhi wakiwa wanne kwa mwaka 2019 na kwa mwaka 2020 vifo vya watu hao vilikuwa vinne na majeruhi watano.

“Kundi la watembea kwa miguu waliokufa mwaka 2019 ni takribani watu 381 na waliojeruhia ni 450 huku mwezi Januari hadi Agosti mwaka 2020 waliofariki walikuwa 214 na waliojeruhiwa wakiwa 217,” inasema taarifa ya polisi.

Columnist: habarileo.co.tz