Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

 ‘Tunaweza kuuza nje dawa za asili kama India, China’

492350ad9efd7cf8401d01d92e105473  ‘Tunaweza kuuza nje dawa za asili kama India, China’

Wed, 17 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

JANA tulianza kuangalia mambo yaliyojiri katika Uzinduzi wa Jukwaa la Ubunifu wa Bidhaa Zitokanazo na Mimea Dawa ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kupitia Mradi wa Uvumbuzi katika Mimea Dawa kwa Ustawi wa Watanzania (GRILI).

Tuliona takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Paulo Mhame kwamba Tanzania ina rasilimali dawa nyingi ikijumuishwa mime dawa zaidi ya 12,000.

Pia tuliona kwamba watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini ni zaidi ya 75,000 na kwamba tiba hizi zinatoa mchango wa zaidi ya asilimia 45 katika matibabu ya magonjwa mbalimbali.

Tuliona pia, kwa mujibu wa Dk Mhame, kwamba China na India ni nchi zinazouza nje ya nchi zao dawa za asili ambapo mauzo yao ni takriban asilimia 35 ya biashara ya dawa zote za asili duniani. Anasema tukisimama imara, kutoka na kuwa na mimea dawa lukuki, tunaweza kuuza pia hadi nje.

Naye Mkuu wa Mradi wa Uvumbuzi katika Mimea Dawa kwa Ustawi wa Watanzania (GRILI), Dk Faitha Mabiki, anasema tangu mradi uanze mwaka 2018 umekuwa na mafanikio makubwa kwa wadau wa tiba asili nchini na kwamba mradi huo unalenga kuhakikisha biashara ya tiba asili na mimea dawa inachangia uchumi wa wadau wao na taifa.

Lakini Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa utawala na fedha, Profesa Amandus Mhairwa, anasema lengo la jukwaa hilo ni kuibua ubunifu na kutatua changamoto zilizoko kwenye mnyaroro wa thamani wa biashara ya bidhaa za miti na mimea dawa hapa nchini.

Anasema chuo kikuu hicho kupitia watafiti wake kwenye mradi huo wamefanya tafiti nyingi ambazo zimeonesha kwamba kuna changamoto nyingi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa biashara ya tiba asili na mimea dawa.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko, anawataka waganga wa tiba asili na tiba mbadala kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kupima viambata mbalimbali vinavyopatikana kwenye dawa zao ili kusaidia kuepusha madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa wateja wao endapo dawa itakuwa na viambata ambavyo sio salama.

“Kazi ya ofisi yangu sio kuwazuia nyinyi kupata usajili wa dawa zenu bali tunataka kuona kila dawa mnayoitoa kwa wagonjwa iwe na viambata sahihi ili iweze kutibu vizuri na isilete madhara kwa wateja wenu lakini pia upimaji wetu ndio wa mwisho ili muweze kupata usajili wa dawa, tushirikiane,” anasema Dk Mafumiko.

Anasema lengo ya waganga wa tiba asili na lengo ya ofisi yake ni moja tu, kuhakikisha usalama wa wananchi na watumiaji wa dawa hizo.

Anasema ofisi yake inavyo vifaa na wataalamu wa kutosha kubaini kila kilicho kwenye dawa. Ni kwa msingi huo anawataka wale wachache miongoni mwa matabibu wa tiba asili wanaofanya udanganyifu waache maana watabainika.

Dk Mafumiko anaipongeza SUA na watalaamu wake kwa jitihada kuwa wanazozichukua katika kuwasaidia waganga wa tiba asili kuweza kuboresha huduma ya tiba wanayoitoa kwa jamii ili iweze kuwa bora na yenye viwango vinavyohitajika.

Katibu wa Shirikisho Vyama vya Tiba Asili Tanzania (SHIVYATIATA), Othaman Shem, anaiomba Serikali kuitazama upya sheria namba 23 ya tiba asili ya mwaka 2002, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 kwani imeonekana ni kikwazo kwa wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala.

Anasema miongoni mwa vipengele vya sheria hiyo iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 vinazuia kutangaza tiba asili na imeweka gharama kubwa za usajili wa dawa asili.

Anatolea mfano kwamba kusajili aina moja ya dawa ya asili ili iweze kukubalika kisheria ni Sh milioni 1.5 kiasi ambacho amekitaja kuwa ni kikubwa mno kwa wataalamu wa tiba asili kuweza kukimudu.

“Ni vema serikali ikatazama upya sheria, vigezo na gharama za usajili wa dawa za asali,” anasema Shem.

Katika kuunga mkono dawa za tiba asili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye anawashauri Watanzania kuendelea kutumia dawa zetu za asili na tiba mbadala hasa pale zinapokuwa zimethibitishwa na Mkemia Mkuu.

Sumaye, anasema tiba nyingi za asili na mbadala zimeonesha uwezo mkubwa katika kukabiliana na magonjwa ya aina mbalimbali ikiwemo corona (COVID -19).

Sumaye anasema hayo alipotembela maonesho ya wadau wa tiba asili na tiba mbadala mwishoni mwa Januari mwaka huu 2021 katika eneo la soko kuu jipya la Mjini Morogoro.

Sumaye anasema kwa upande wa corona katika nchi yetu, dawa za asili zimetusaidia sana kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo tofauti na nchi nyingine ambazo zimepigwa vibaya na ugonjwa huo.

“Watu walipoambiwa wajifukize wakawa wanajifukiza kila nyumba, mnywe hizi dawa asili na tangawizi, malimao na vitunguu swaumu wanakawa wanakunywa. Utakuta kwenye hoteli leo kuna chai ya tangawizi inipata.

“Hata mimi nikienda hotelini kama siku hiyo ninahitaji kunywa chai, hakuna shida ninatengenezewa chai ya tangawizi. Vitu vya namna hiyo vinasaidia sana licha ya kuondoa magonjwa lakini vinajenga mwili, unajua dawa nyingi zinazotoka viwandani zinajenga sumu mwilini,” anasema Sumaye.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu anasema dawa za asili siyo za kupuuza kwani karne nenda karne wazee wetu na mababu zetu waliishi na kuendelea kuishi miaka mingi wakitumia dawa za asili.

Sumaye anaishauri Serikali itupie jicho kwa kuongeza uwezo kwa taasisi mbalimbali za utafiti kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kujenga uwezo kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala katika kuboresha huduma zao.

Columnist: habarileo.co.tz