Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Tunapomuomboleza Magufuli tuheshimu alichokipanda sekta za sanaa na michezo

1a1e284074e1806694ab8c919f727cb3 Tunapomuomboleza Magufuli tuheshimu alichokipanda sekta za sanaa na michezo

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATANZANIA tumepata pigo kubwa kwa msiba uliotugusa na kuishtua dunia, wafuatiliaji na wasio wafuatiliaji wa siasa za Tanzania, kutokana na kifo cha Rais John Magufuli.

Rais Magufuli tangu alipopokea kijiti cha kuiongoza Tanzania kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Alianza kwa kuahidi kwenye kampeni zake, pamoja na mambo mengine, kuisimamia ipasavyo sekta ya sanaa na ubunifu kama ambavyo Ilani ya utekelezaji ya Chama Cha Mapinduzi ya 2015-2020, chini ya kipengele cha Tasnia ya Sanaa, kifungu cha 163 inavyoonesha.

Ilani hiyo iliainisha mambo mengi ikiwemo kuanzisha na kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Tasnia ya Sanaa utakaowezesha upatikanaji wa mikopo ya masharti nafuu kwa wazalishaji, watengenezaji, wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo wa tasnia hii nchini n.k.

Niseme wazi, sikuamini kama Rais Magufuli angeweza kutekeleza ahadi alizoahidi kwenye kampeni kuhusu sanaa, nikiamini kuwa hakuwa na ‘interest’ na masuala ya sanaa na michezo.

Niliamini uongozi wake ungejikita kwenye kujenga barabara, reli, uwekezaji, kilimo, mifugo na madini, basi!

Lakini katika uongozi wake hadi mauti yanamfika, Magufuli ameonesha nia ya dhati kuiondoa kasumba kuwa Sekta ya Sanaa inaishia kwenye Utamaduni (kwa ajili ya kujiburudisha) badala ya kuitazama kibiashara na chanzo muhimu cha kiuchumi (new sector with economic potential).

Nilianza kuiona nia ya dhati pale alipounda Baraza la Wawaziri na kuipa sanaa Idara yake kamili kwa nia ya kuhakikisha inakua na kuwa chanzo kikubwa cha ajira na mapato miongoni mwa Watanzania.

Kwa kauli yake alibainisha kuwa tasnia ya sanaa ikiendelezwa vizuri ni chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana, ni njia madhubuti ya kukuza utalii na uchumi wa taifa na wa wananchi kwa ujumla.

Ndiyo maana sikuona ajabu hata pale nilipokuwa namwona akiwaalika wasanii au wawakilishi wa sanaa kwenye kila tukio la kitaifa.

ALIKUWA RAIS WA SANAA NA UTAMADUNI

Kwa mwendo wake, nikaanza kumuona Kim Dae Jung (Rais wa zamani wa Korea Kusini) akizaliwa nchini Tanzania.

Kim Dae Jung ameifanya Korea Kusini iitwe ‘Hollywood ya Asia’ na nchi zingine za Bara Asia, kwani alifanikiwa sana kueneza sanaa zake katika nchi zingine za Asia na hata Afrika kwa sababu ya sera madhubuti, alipoanzisha mradi maalumu na kutenga dola za Marekani milioni 148.5.

Alitumia fursa ya mtikisiko wa kiuchumi uliozikumba nchi za Asia mwaka 1997 kwa kuwekeza katika sanaa na utamaduni kwa lengo la kuzalisha na kuuza nje kama bidhaa. Hakuishia hapo, yeye mwenyewe alipenda kujiita Rais wa sanaa na Utamaduni.

SERA NA SHERIA

Katika kipindi cha kwanza cha Rais Magufuli tuliziona juhudi zake kupitia Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe katika kuharakisha mchakato wa Sera za Filamu, Sanaa na ile ya Utamaduni.

Kutokuwepo kwa Sera imekuwa chanzo cha sekta ya sanaa kuyumba na kukosa mwelekeo. Sera pekee iliyopo ya Utamaduni haiitazami sekta za ubunifu (filamu, muziki na sanaa nyingine) kibiashara bali kama sehemu ya utamaduni.

Na baadaye wasanii wote kupitia vyombo vyao wakaanza kuingia mkataba na Data Vision na kampuni ya CogsNets Technology kwa ajili ya kusajiliwa kwenye mtandao wa kuwafanya wafahamike kitaifa na kimataifa.

Mimi ni shahidi kuhusu juhudi za Magufuli kwa kuwa nimewahi kuhudhuria vikao kadhaa vya kujadili mustakabali wa sanaa na kuiona nia ya dhati ya Rais Magufuli.

UCHUMI WA SANAA

Magufuli alikuwa anasisitiza kuwa na Tanzania ya uchumi wa kati, mbali na kuingia katika uchumi huo na rasilimali nyingi tulizo nazo, pia upo uchumi mkubwa ndani ya sekta ya sanaa, Magufuli ameonesha kuzisimamia kwa vitendo ilani zote za CCM kwa mwaka 2015-20 na ile ya 2020-25.

Sanaa ni fedha, ni uchumi. Inatosha kuwa mkombozi wa bajeti za serikali na kutoa mchango wa thamani katika Pato la Ndani la Taifa (GDP) na jumla katika Pato la Taifa (GNP).

Sanaa ni kilainishi (grisi) cha uchumi wa sekta nyingine nyingi. Kwa mantiki hiyo, mafanikio ya Sanaa na Utamaduni ni msisimko wa uchumi kwa Taifa.

Wasanii wanapofanya biashara na ikapita kwenye mkondo wake barabara, husisimua uchumi wa sekta ya Viwanda na Biashara. Huitangaza nchi na kuchagiza kivutio cha wageni kutembea kibiashara au kitalii, hivyo kuipa nguvu sekta ya Utalii.

Wasanii wanapotajirika, huwezesha kupanuka kwa sekta ya Uwekezaji na kutanuka kwa sekta za Ajira na Elimu.

CHANZO CHA UTALII

Mara kadhaa Rais Magufuli amesisitiza kuhusu vivutio vya Tanzania na kusema kuwa anafahamu Tanzania inashika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, nyuma ya Brazil.

Tanzania tuna maeneo bora kuanzia Bara hadi Zanzibar. Hii ni nchi ya maajabu na vivutio: mlima mrefu Afrika (Mlima Kilimanjaro), mbuga bora yenye wanyama wa kuvutia duniani ya Serengeti, yenye stori ya wanyama wanaohama kila mwaka na kurejea.

Tuna mbuga kubwa na bora duniani, Selous, na bonde kubwa Afrika lililotokana na volcano, Ngorongoro Crater, eneo maarufu duniani, linalofuga wanyama pasipo kuwekwa uzio.

Tuna sehemu nzuri ya kuvua samaki na bandari katika Afrika, labda duniani na mamia ya maili za ufukwe wa Bahari ya Hindi, tuna maziwa yote makubwa, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa (hakuna nchi nyingine zaidi yetu).

Zanzibar pia ni moja ya visiwa vyenye historia ya kutukuka, iliyokusanya wahamiaji.

Maeneo mengine ya kuvutia ni Amani Forest Nature Reserve, Mapango ya Amboni, Bagamoyo, Isimila Stone Age Site, Maporomoko ya Kalambo, Michoro katika mapango ya Kondoa Irangi na Ziwa Natron.

Pia kuna Lushoto, Mbozi Meteorite, Hifadhi ya Mkomazi, Mwanza, Ol Donyo Lengai, Olduvai Gorge, Mfumo wa Mto Rufiji, Ukanda wa Pwani ya Waswahili, Tarangire, Tendanguru, Ujiji na Milima ya Usambara.

Ni wazi kwamba inawezekana kufikia hatua nzuri zaidi na kuona matokeo ya faida ya sanaa katika utalii kama ambavyo nia ya dhati aliyokuwa nayo Rais katika kuinyanyua sekta ya sanaa ilivyobainika.

MICHEZO

Rais Magufuli pia, katika uongozi wake, amedhihirisha kuwa anapenda michezo, alitushangaza wengi kwa kuichangia timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Lesotho katika kuwania tiketi ya kufuzu kwa michuano ya kombe la Mataifa ya Afrika AFCON nchini Cameroon mwakani.

Rais Magufuli alitoa kiasi hicho cha pesa Ikulu, siku alipokuwa anazungumza na wachezaji wa timu hiyo sambamba na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ili kutengeneza hamasa na timu iweze kufanya vizuri.

Kabla ya hapo, mapenzi ya Rais Magufuli kuhusu michezo yalijionesha wazi ambapo alikwenda Uwanja wa Taifa kuwakabidhi timu ya Simba SC kombe la ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2017/2018, katika mchezo wa Simba SC dhidi ya Kagera Sugar.

0685 666964 au [email protected]

Columnist: www.habarileo.co.tz